Nenda kwa yaliyomo

Wasafwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Wasafwa ni kabila la watu jamii ya Wabantu kutoka eneo la milima ya mkoa wa Mbeya, kusini mwa nchi ya Tanzania.

Wako hasa katika wilaya za Mbeya mjini, Mbeya vijijini, Mbozi na Chunya

Mwaka 1987 idadi ya Wasafwa ilikadiriwa kuwa 158,000 [1].

Lugha yao ni Kisafwa, lugha yenye uhusiano wa moja kwa moja na Kibantu. Salamu yao kuu ni "Mwagona".

Rangi kuu ya mavazi yao ni njano.

Dini kuu iliyotawala kati yao ni Ukristo, lakini wengine wamebaki kuamini mila zao.

Uongozi wa kimila[hariri | hariri chanzo]

Kiongozi wa Wasafwa huitwa mwene kwa lugha yao.

Mwene maarufu sana alikuwa Mwene Paul Mwashinga aliyekuwa tajiri na msomi; makao makuu yake yalikuwa Igawilo, Mbeya mjini; naye aliaga dunia mwaka 1987; msiba wake ulihudhuriwa na watu mashuhuri sana.

Mwene mwingine ni Mwene Mwalyego wa Mbalizi. Chifu wa sasa (Agosti 2021) ni Roketi Mwanshinga kuanzia mwaka 1987.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Kihistoria Wasafwa ni watu wanaopenda sana kuishi maeneo yenye mvua nyingi na baridi, hii ni kutokana na wao kuwa ni wakulima wa mazao yanayohitaji mvua, kwa mfano viazi mviringo, vitunguu swaumu, mahindi na numbu. Historia inasema kwamba kulitokea vita baina ya Wasafwa na jamii zilizowazunguka wakigombea maeneo ya kilimo. Katika vita hivyo kuliibuka mapigano makali mno ambapo ilionekana kuna watu wanapigwa lakini hawafi. Kwa Kisafwa mtu asiyekufa huitwa au hicho kitendo huitwa ASIFWA, yaani hafi. Kwa maana nyingine ili umuombee mtu mabaya na afe unatamka "asafwa". Na moja kwa moja jamii hiyo ikaitwa Wasafwa.

Asili na chimbuko[hariri | hariri chanzo]

Zipo nadharia nyingi zinazoelezea asili na chimbuko la Wasafwa ambao ndio wenyeji haswa wa Mbeya. Ikumbukwe hawa ni wabantu, hivyo basi ni jamii za Kibantu toka Afrika Magharibi. Lakini nadharia na masimulizi haya yamegawanyika kama ifuatavyo:

1. Wasafwa ni kutoka Ugogo, Dodoma

Nadharia hii inasaidiwa na ukweli hasa kwenye salamu, kuna Wasafwa wakisalimiana utasikia "mwagona gogo", ambapo humaanisha kuwa wao ni kutoka Ugogo, Dodoma.

2. Wasafwa ni kutoka Ukinga, Makete

Hapa napo kuna ushahidi, ambao unaelezea kuwa Wasafwa ni jamii toka Ukinga, nadharia hii inashibishwa na salamu pamoja na Wasafwa waishio kata ya Ilungu, Igoma na Ulenje, Mbeya Vijijini. Katika suala la salamu baadhi husalimiana "mwagona nkinga", wakimaanisha kuwa hujambo mtu toka Ukinga. Pia wao huamini kuwa ni matokeo ya msafwa, mkinga, mnyakyusa na muwanji. Lakini nadharia hii pia inashadadiwa na ukweli kwamba katika kata hizo wapo Wakinga wengi ambao kwa sasa hujiita Wasafwa na wanafuata mila na taratibu za Kisafwa. Ni dhahiri kuwa wapo watu na koo kama Kyando, Swallo, Longopa, Chaula, Enea na nyingine nyingi ambazo ni matokeo ya wazee wao kuhamia Usafwa, hasa tarafa ya Tembela, Mbeya Vijijini.

3. Wasafwa ni kutoka Unyakyusa

Nadharia hii ipo katika salamu, ambapo wapo Wasafwa wanaosalimiana "mwagona hondya", Wakimaanisha hujambo toka Unyakyusa. Ikumbukwe Wasafwa huwaita Wanyakyusa "Wahondya". Nadharia hii inashibishwa na watu waishio tarafa ya Tembela, hasa Ilungu na Igoma. Ushahidi wa nadharia hii unashibishwa zaidi na masimulizi ya wazee yahusuyo watu wa ajabu waliokuWa wanakula watu wenzao, kwa Kisafwa waliitwa "Ayinga". Hawa ni viumbe waliokuwa wanapatikana maeneo ya pembezoni mwa safu za Milima Livingstone, ambao walisababisha jamii za watu wa kule hasa Mwakaleli kukimbilia Mbeya Vijijini hasa maeneo ya Ilungu na Igoma. Mmoja wa wahanga hao ni ukoo wa Mwanginde Mkoma ambao unawakuta Mwakaleli na Ilungu.

4. Wasafwa ni Wasangu

Hapa pia salamu ndio ushahidi na kigezo cha kwanza. Hawa husalimiana "mwagona nsangu au nsango au sango", wakimaanisha hujambo mtu wa Usangu. Hawa ni wengi Uyole, Mswiswi, Igurusi, Inyala na Itewe. Wao huamini kuwa ni matokeo ya Msafwa na Msangu kwa baba. Ikumbukwe kuwa Msangu alishirikiana na Mbena kumshambulia Mhehe ambapo baada ya kushindwa akamvamia Msafwa.

5. Wasafwa ni kutoka Botswana

Nadharia hii inashadadiwa na maelezo ya ufanano wa Wasafwa na watu wa Botswana hasa katika ngoma za asili kama nyimbo na mtindo wa maisha. Inasemekana kuwa Wasafwa walitokea Botswana wakaingilia moja kwa moja njia ya Msumbiji hadi Makete kisha Mbeya. Wengine hudai kuwa waliingilia Dodoma. Ugumu wa nadharia hii upo katika Ubantu maana asilimia kubwa ya jamii za kusini mwa jangwa la Sahara ni Wabantu.

6. Wasafwa ni kutoka nchini Kongo

Hapa ndipo penye maelezo mapana maana hawa ni Wabantu na kwa kuthibitisha hilo zipo shahidi toka koo mbalimbali kama Mwatumbo na Mwanshinga. Wapo wanaoamini Mwanshinga ni Msafwa Mkinga na Mwatumbo ni Msafwa Mwanji. Lakini historia inaonesha kuwa hawa ni wasafwa toka Kongo hasa misitu ya Kongo. Uweli huo unashibishwa na masimulizi ya kurudi nyuma yaani asili ya Wasafwa, kabila toka kundi la makabila yafahamikayo kama Wabantu wanaopatikana hasa kusini mwa jangwa la Sahara na wazungumzao lugha ya Kibantu na muingiliano na makabila mengine ya Kibantu. Hiyo historia inasema Wasafwa na Mwanshinga kwa ujumla asili hasa ni Afrika magharibi hadi Sudan kusini, na baadaye wakahama kwa sababu mbalimbali. Ndipo waliposafiri hadi Kongo ya leo, hasa misitu yake na pembezoni kwayo.

Baada ya miaka mingi walihamia Mbeya kwa misafara miwili, ambapo mmoja uliingilia Sumbawanga - Tunduma na mwingine ulipitia Zambia- Malawi- Msumbiji na kuingilia Makete yaani Ukinga hadi Mbeya, hasa ukoo wa Mwanshinga. Hawa na wengine wengi ndio wale wanaosalimia "mwagona kinga". Wasafwa hawa wengi wao ni koo za kichifu na kwa maana hiyo hata leo chifu wa Mbeya ni wa jamii hii. Baadhi ya shahidi kuwa walitokea Kongo ni uwepo wa majina kama yale yapatikanayo Kongo: Wambi, Ngatele, Mwinga, Mbwiga, Selina, Silyelelo n.k. Pia tabia ya kupenda kuishi maeneo yenye mvua nyingi ni sawa na mvua zipatikanazo misitu ya Kongo.

Misafara hiyo inasemekana ilitengana baada ya kutokea sintofahamu wakiwa njiani toka Kongo, walipofika njiani wengine wakasonga kuelekea Zambia, Malawi, Msumbiji pembezoni mwa ziwa Nyasa hadi Makete ya leo. Huko wakakaa na kuishi wakichangamana na wenyeji, yaani Wakinga na Wawanji, na baadaye watoto wengine kuhamia Mbeya vijijini. Hawa walikuwa wale wanaopenda kuhamahama na kwa kuwa tayari Mbeya kulikuwa na Wasafwa walioingilia Tunduma hadi Mbeya mjini ikawa rahisi kwao kuingia Mbeya kwa kupitia njia ya Makete hasa kata ya Ilungu ambayo ilikuwa kama lango.

Historia hiyo inaendelea kudai kuwa kundi la Wasafwa waliopitia Sumbawanga walikutana na Wafipa wa Sumbawanga wakaendelea na msafara kuelekea mashariki na baadaye wakaja kukutana kwenye mgongano na Wasangu ambapo muda huo walikuwa na mvutano na Wahehe chini ya Mkwawa, hivyo wakaanza kusambaa maeneo ya Mbeya.

Nadharia tano zilizotangulia zina uhalisia kwa asilimia ndogo kutokana na ukweli kwamba zinamezwa na hiyo namba 6. Hii ni kwa sababu zenyewe ni matokeo ya muingiliano wa kijamii baina ya Wasafwa na jamii nyingine. Ukweli ni kwamba vita, njaa na utamaduni vilipelekea Wasafwa kuingiliana na jamii nyingine. Mfano baada ya vita kati ya Merere na chifu Lyoto wa Usafwa mabinti wawili wa Kisafwa walitolewa kama zawadi kwa chifu merere baada ya kushinda. Kwa hiyo Msafwa asili asiye na mchanganyiko enzi hizo ni yule wa Mbeya mjini.

Makundi yaundayo kabila la Wasafwa[hariri | hariri chanzo]

Wasafwa wamegawanyika katika makundi makubwa matano, tena kimaongezi au kimatamshi wamegawanyika katika makundi kumi, kwa mfano ndani ya kata moja unakuta kuna tofauti ndogo kimatamshi. Katika makundi hayo matano kuna:

1. Wamporoto

Hao ni Wasafwa wanaozungumza Kisafwa chenye ladha tofauti na makundi mengine. Hupatikana kwa wingi na kwa kiasi Mwakaleli number one, Kiwira, Isyonje, Ndaaga, Ntokela katika wilaya ya Rungwe na baadhi ya maeneo ya maendeleo, Tembela na Ijombe huko Mbeya vijijini.

Wao ni matokeo ya Msafwa kwa wingi na mchanganyiko wa baadhi ya makabila.

2. Wasongwe

Ni Wasafwa wazungumzao Kisafwa chenye ladha ya kipekee na makundi mengine. Hawa huzungumza na kuelewana zaidi wao kwa wao maana ni Wasafwa wa Songwe. Wanapatikana na kuishi kwa wingi Mbalizi, Utengule Usongwe, Mshewe, Usongwe, Swaya, Igale, Iwindi na maeneo ya wilaya ya Mbozi. Pia wapo Tunduma na Mbeya mjini kwa kuhamia.

Pia Mmalila na Mnyiha kihistoria wote walitokana na koo za Wasafwa ambao walitawanyika kwa lengo la kujihami/kuzuia kushambuliwa na maadui wakati wa mapigano yaliyokuwepo enzi hizo. Wasafwa wa Utengule na Mshewe ndio hasa inaaminika ni matokeo ya Mnyiha wa leo na Mmalila. Kuna mzee alisema Wamalila wametokana na neno "Malila" yaani sehemu ambayo maadui walikuwa wanayoishia na lengo kuu ni kwenda kuzuia maadui sehemu wanazoishia na kwa upande wa "Wanyiha" anasema ni neno lililotokana na sehemu ambako maadui walielekea au kukimbilia wakati wa mapigano; hivyo basi hata matamshi yalikuwa yanabadilika kwa kadiri walivyokuwa wanakutana na kuchangamana na jamii nyingine huko walikoelekea.

3. Wagulukha

Hao wanaishi na kupatikana kwa wingi Chunya, Ikukwa, Ihango, Lwanjiro na Mbeya mjini. Wao ni tofauti kidogo kimatamshi na wale wa maeneo mengine. Hawa wengi wameoa na kuolewa na Wabungu toka Chunya na kiasili ni matokeo ya vita kati ya Merere na chifu Lyoto Mbeya mjini ya leo.

4. Wambwila

Hao wanaishi na kupatikana kwa wingi Ilungu, Igoma, Ulenje, Makete na Mbeya mjini. Hawa huzungumza Kisafwa cha kipekee mno, pia ndio lango kuu la Mkinga kuingia Mbeya mjini. Wanazungumza zaidi Kisafwa kiitwacho Kimbwila. Wengi wao huishi nje ya mji yaani milimani kwenye mvua nyingi kwa ajili ya kilimo, hasa Mbeya vijijini. Moja ya kata zenye Wasafwa waliochanganya damu ni Ilungu, Ulenje na Igoma na tarafa ya Tembela kwa ujumla. Mfano ndani ya kata hizo unakuta kuwa hao ni Wasafwa waliotokana na mchanganyiko wa Wasafwa, Wasangu, Wawanji, Wakinga, Wanyakyusa na Wabena kiasi.

5. Wamalila

Kundi hilo la mwisho lina utata kama ni kabila au kundi ndani ya kabila. Ifahamike kuwa neno Wamalila kwa Kisafwa lina maana ya uchafu mwilini uliowekwa kishirikina yaani "amalila". Sasa ukiwauliza Wamalila wao husema asili yao ni Botswana na wengine husema ni mlima Mbeya. Ila kwa Wasafwa hilo ni kundi lililojitenga na wenzao kwa kiasi. Wanaishi tarafa ya Isangati yote na maeneo ya Usongwe. Katika kundi la Wamalila wapo walio na ushahidi wa kuthibitisha waliendaje kule. Ni kwamba, katika kipindi cha mgogoro na mtemi merere kuna Mmoja kati ya watu wa Kisafwa alipambana kumuua askari mmoja wa mtemi Merere na kukimbilia maeneo ya Mbozi eneo hilo likiitwa Ntandala na baadaye alioa huko ila hakuendelea kukaa, aliamua kurudi ijapo hakufika eneo lake la nyumbani ila huyo shujaa aliweza kuishi maeneo ya Umalila na maisha yake yaliendelea hapo. Alikuwa mtu kutoka ukooo wa Nswila, watu wanaopatikana kwa wingi maeneo ya Iwindi hadi leo na kidogo Umalila.

Ifahamike kuwa Mbeya haswa kulikuwa na makabila au jamii nne tu, nazo ni: Wasafwa, Wanyakyusa, Wasangu na Wanyamwanga. Wajiitao Walambia na Wandali ni matokeo ya Mnyakyusa, Wamalila na Wanyiha ni kutoka Usafwa, Wabungu wa Chunya ni matokeo ya makutano ya kuoana kwa Msafwa, Msukuma na Mnyamwezi kisha kukawepo Mbungu. Baadae wakahamia Wakinga, Wabena na Wawanji toka Iringa.

Ngoma za asili[hariri | hariri chanzo]

Ngoma kuu ya asili ya Wasafwa ni ngoma ichezwayo wakati wa sherehe, matambiko na mavuno. Ngoma hiyo maarufu huitwa "mbeeta". Huchezwa kwa kutumia filimbi, pembe za wanyama, mbegu zilizo ndani ya makopo na vingine vingi. Ngoma za asili huchezwa kwa sasa hasa Itewe, Ikukwa na Ifumbo. Hakika kule bado wanaenzi asili.

Kilimo[hariri | hariri chanzo]

Wasafwa ni kabila la wakulima ambao hulima sana viazi, mahindi, ngano, numbu, karanga, maharage na mazao mengine kama miti maeneo yenye mvua nyingi kama Rungwe na Mbeya vijijini. Wasafwa pia ni wafanyabiashara hasa ya viazi na vitunguu swaumu.

Kutokana na kilimo wametawanyika Tanzania na kwenda maeneo yenye mvua, wapo kwa wingi Arusha, hasa Arusha chini na Meru, wapo Mang'ola Karatu, Muheza Tanga, West Kilimanjaro, Usa Arusha, Mufindi Iringa, Njombe, Makete na Morogoro.

Wasafwa na Mbeya[hariri | hariri chanzo]

Mbeya ni neno litokanalo na lugha ya Kisafwa likiwa linatamkwa ibheya likimaanisha chumvi. Wafanyabiashara walifika Mbeya na kubadilishana chumvi toka Chunya na mlima Mbeya kwa bidhaa nyingine. Ilikua ni ngumu wageni kutamka neno ibheya, hivyo wakajikuta wanatamka imbeya. Baadae mnamo 1927, wakati wa usanifishaji wa Kiswahili, neno hilo likasanifishwa na kuwa Mbeya.

Maneno asilimia 90 ya maeneo ndani ya jiji la Mbeya yanatafsiriwa kwa Kisafwa.

Mifano: neno Mbalizi _ mbalisi

Loleza _ lolezya (sindikiza)

Uyole _ iyoole

Igawilo _ kigavilo (sehemu ya kugawania)

Isyesye _ inzyesye

Iwambi _ wambi

Ijombe _ aina ya mti

Majina ya Wasafwa[hariri | hariri chanzo]

Majina ni sehemu ya utamaduni wa Wasafwa, mtoto hupewa jina kutokana na tukio au kumbukumbu fulani. Mfano mtu akiitwa Nzala, alizaliwa kipindi cha njaa.

Mbwiga _ mtoto wa kiume aliyekua kwa kuumwaumwa na kupewa madawa

Mbozyo _ mtoto wa kike aliekua kwa kuumwaumwa na kutibiwa kwa miti shamba

Pia kuna jina la Kisafwa "Nkundi'. Jina hili anapewa mtoto ambaye watangulizi wake wote wamefariki. Zamani kulikuwa na shida kubwa ya kufa watoto kwa mfuatano katika familia, kwa hiyo basi mtoto aliyekua vyema alipewa jina la Nkundi, maana ya Inkundi kwa Kisafwa ni vumbi. Wazazi walitoa jina hilo kwa kuonesha kukata tamaa kuwa hata huyo aliyezaliwa atakuwa vumbi.

"Esose' kwa Kisafwa maana yake ni kuzaa mtoto asiye na baba rasmi. Zamani hilo lilikuwa tukio la nadra sana na ilionekana ajabu sana kusikia binti wa fulani "asosile umwana".

Vinginevyo siku za baadaye majina hayo yamekuwa yakitumiwa tofauti na maana zake halisi kutokana na ukweli kwamba akina bibi wanarithisha majina yao ili yaendelee kuwepo hata baada ya wao kutoweka.

Wapo watoto sasa hivi wanaitwa 'Matundu' bila maana halisi ya neno hilo.

Matundu kwa Kisafwa ni majani ya mmea wowote. Mtu alipoitwa Matundu ilimaanisha kuwa amepatikana kwa njia za madawa ya majani asilia.

Pia yapo majina ya koo na mengi huwa yanaanza na Mwa...... kwa mfano Mwalingo, Mwanyanje, Mwaihoyo, Mwantinda, Mwandele, Mwanzanga, Mwasote, Mwanzanga, Mwangoka, Mwanandodo, Mwaanzala, Mwanyonga, Mwanzonga, Mwalyambi, Mwajafu, Mwansanga, Mwanguku, Mwaamudu, Mwalyego, Mwandiya, Mwasoni, n.k.

Pia wapo akina Manzozi, Magwilla, Sijanga, Sijonjo, Simwinga, Yilyelelo, Ndabhishe, Masimbani, Lyoto, Lingo, Ngatele, Ndaduu, Ndilwene, Ndangano, Gwilla, Zyoni, Malema, Nzalu, Sewa, Selina, Nsolo, Sambwe, Nzambwe, Mponzi, Zella, Ndongole, Nzongwa, Shitambala, Fwokile, Selela na mengine mengi.

Siku hizi watoto wengi wa Mbeya yaani Wasafwa hupewa majina kutokana na ama baba ni mpenzi wa mchezaji fulani au mwanamuziki. Wapo kwa sasa watoto huitwa Ronaldo, Beckham, Rooney, Nelly, Awilo, Yesu, Lowasa, Kikwete, Messi, Zidane na mengine mengi.

Dini[hariri | hariri chanzo]

Wasafwa wengi ni Wakristo na Wapagani, labda nusu nusu. Ni ngumu sana kumkuta Msafwa Mwislamu. Wale Wapagani husali maeneo ya misitu maarufu kama "maganjo" kama lile lililopo jijini Mbeya. Wengi bado wanaamini katika miungu.

Uchawi mkuu kwa Wasafwa huitwa Itunga na wale wauaji wa kichawi huitwa Mbuda. Mambo hayo ni ya kimila hivyo imekuwa ngumu sana kuwabadilisha baadhi ya watu.

Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wasafwa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.