Wairaqw


Wairaqw (pia huitwa Wambulu kutokana na jina la mji wa Mbulu) ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi katika mkoa wa Manyara na mkoa wa Arusha kusini kwa Ngorongoro.
Lugha yao ni Kiiraqw, jamii ya lugha za Kikushi za kusini.
Mwaka 2001 walikuwa 462,000 hivi. Idadi hiyo yaweza kuwa imevuka 1,000,000 kwa sasa.
Asili
[hariri | hariri chanzo]Kihistoria, ni kati ya Wakushi wa kwanza kuhamia eneo la Tanzania ya sasa, ambapo walichanganyikana na Wadatoga na Wabantu, inavyoonekana katika utafiti juu ya DNA. Walitokea Ethiopia katika milenia ya 3 KK na kuelekea kusini kupitia bonde la Ufa.[1]
Nadharia nyingine zinapendekeza kuwa walitokea Mesopotamia ya kale. Hata hivyo hakuna uhusiano na nchi ya Irak (au Iraq), iliyopo katika Asia ya Magharibi, isipokuwa jina la kufanana.[2]
Wairaqw walibadilishana mazao na jamii za Kimasai na kupewa mifugo. Mifugo waliyopata iliendelea kukua na kuongezeka na hii ikawa sababu ya vita kati yao na Wamasai. Wairaqw ni jamii isiyopenda vita hivyo ilipelekea kuhamahama wakikimbia vita sehemu mbalimbali walizojaribu kuishi. Ingawa hawakupenda vita walikuwa na silaha za kujihami kama mikuki, mishale na mawe yenye ncha kali.
Kama ilivyo kwa jamii nyingi za Tanzania, baba na mama hawalali kitanda wala chumba kimoja na hivyo suala la kupata mtoto ni jambo la siri sana na malezi ya watoto yanapewa kipaumbele.
Vijana wa kiume wakifikisha umri wa miaka minane huanza kupata maelekezo ya aina ya kazi na majukumu wanayopaswa kufanya kutoka kwa baba na babu zao. Maelekezo hayo ni pamoja na maadili mema, ukakamavu, mshikamano na mbinu za kujitegemea na kukabiliana na changamoto mbalimbali kama mkuu wa kaya.
Watoto wa kike pia wanapata mafunzo mengi kutoka kwa mama na bibi zao na wanapofikisha umri wa miaka kumi na tano wanatengwa mahali na kuanza kufundishwa majukumu ya kuwa mama na mke katika jamii. Binti anajulishwa mapema athari za kubeba mimba kabla ya ndoa ikiwemo kutengwa.
Mavazi ya asili ya Wairaqw ni ngozi ambazo hulainishwa vizuri na kushonwa kwa mitindo mbalimbali ikiwemo shuka, sketi au kanga. Vazi la kiume ni moja ambalo huvaliwa kwa kujifunika. Vazi la kike ni sketi na mtandio mdogo (ngozi) na wakati mwingine hupambwa kwa shanga.
Ubunifu, muonekano na mpangilio wa nyumba za Wairaqw hufuatana na uhitaji wa usalama hasa wa mifugo. Nyumba ya Wairaqw hujengwa kwa nguzo na fito na kukandikwa kwa udongo wa mfinyanzi. Nyumba hiyo ya mstatili (assemo) ilitumiwa kwa sababu za kiusalama hasa wakati wa vita. Kwa jamii za sasa nyumba hiyo hutumika pia kwa matumizi ya kawaida ya kuishi. Nyumba hiyo huchimbwa kwenye kilima mfano wa handaki na huwa na njia za chini kwa chini kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Wairaqw maarufu
[hariri | hariri chanzo]- Frederick Sumaye - waziri mkuu wa zamani
- Mary Nagu - mbunge na waziri wa zamani
- Willibrod Peter Slaa - mwanasiasa na balozi wa zamani
- Philip Sang'ka Marmo - balozi wa zamani
- Wolfgang Pisa, OFMCap - askofu na rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
- Filbert Bayi - mwanariadha
- John Stephen Akhwari - mwanariadha
- Gabriel Gerald Geay - mwanariadha
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Ikeda, Jiro; Hayama, Sugio. "The Hadza and the Iraqw in northern Tanzania: Dermatographical, Anthropological, Odontometrical and Osteological Approaches" (PDF). Iliwekwa mnamo 30 Machi 2016.
{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Sarah Tishkoff; na wenz. (2009). "The Genetic Structure and History of Africans and African Americans" (PDF). Science. 324 (5930): 1035–44. Bibcode:2009Sci...324.1035T. doi:10.1126/science.1172257. PMC 2947357. PMID 19407144. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2017-08-08. Iliwekwa mnamo 2017-12-07.
We incorporated geographic data into a Bayesian clustering analysis, assuming no admixture (TESS software) (25) and distinguished six clusters within continental Africa (Fig. 5A).[...] Another geographically contiguous cluster extends across northern Africa (blue) into Mali (the Dogon), Ethiopia, and northern Kenya. With the exception of the Dogon, these populations speak an Afroasiaticlanguage[...] Nilo-Saharan and Cushitic speakers from the Sudan, Kenya, and Tanzania, as well as some of the Bantu speakers from Kenya, Tanzania, and Rwanda (Hutu/Tutsi), constitute another cluster (purple), reflecting linguistic evidence for gene flow among these populations over the past ~5000 years (28, 29).
Also see Supplementary Data.
| Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wairaqw kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |