Washubi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Washubi ni kabila mojawapo kati ya makabila ya Mkoa wa Kagera, nchini Tanzania. Washubi wamechanganyika na Watanzania wengine na, ukiacha sehemu kubwa ya kabila hili ambao wanaishi katika Wilaya ya Ngara, wanapatikana kwenye maeneo mengine nchini Tanzania wakijitafutia riziki na ustawi kwa njia moja au nyingine.

Wakati mwingi kabila hilo liliandikwa kama Wasubi badala ya Washubi. Baadhi ya waandishi wa historia waliwatofautisha kwa kuwaita Wasubi wa Magharibi (Washubi wa Milki ya Bushubi - Ngara) na Wasubi wa Mashariki (Wasubi wa Milki ya Usubi iliyoko Biharamulo).

Kabila hili linaongea lugha ya Kishubi ambacho ni Kibantu ingawa Washubi wote si Wabantu. Washubi wanaweza kuelewana lugha na majirani zao Wahangaza, Waha, Warundi na Wanyarwanda na kwa kiasi fulani makabila mengine ya maziwa makuu, ukiacha baadhi ya makabila, kama vile Wasukuma na Wanyamwezi. Mwaka 1987 idadi ya Washubi ilikadiriwa kuwa 153,000 [1].

Historia[hariri | hariri chanzo]

Kabila hili lina historia ndefu kuanzia karne ya 16, wakati Mtawala maarufu kutoka kaskazini mwa Uganda ya sasa, sehemu ya Ankole, aliyejulikana kama Ruhinda, aliposafiri na watoto wake na kuhamishia makazi yake Karagwe.

Baada ya kuanzisha utawala wake Karagwe, watoto wake walielekea maeneo mengine katika eneo la maziwa makuu, maarufu kwa Kiingereza kama Interlucustrine Region.

Mmoja kati ya watoto wa Ruhinda alielekea Bushubi na kuanzisha milki ya kiutawala bila shida yoyote, kama ambavyo ilikuwa kwa maeneo mengine kama Gisaka, Kyamtwara, Ihangiro, Buzinza na kwingineko. Hali hiyo ilitokana na maeneo hayo kukaliwa na wakulima wachache ambao hawakuwa na nguvu za kuwazuia wageni ambao walikuwa na uwezo mkubwa wa silaha na utajiri mkubwa wa mifugo, jambo lililoleta matumaini hata kwa wenyeji.

Jamii ya Washubi iliendelea kuongezeka na kujiimarisha kama milki ya kiutawala ikiwa na mahusiano na milki nyingine jirani, zikiwemo zile za Karagwe (Wanyambo), Buha (Waha), Biharamulo (Wazinza na Wasubi), Burundi (Warundi), Rwanda (Wanyarwanda), Buganda (Waganda) na Ankole (Wanyankole).

Mahusiano hayo yalikuwa pamoja na biashara, teknolojia ya chuma, kuoleana, vita vya kupanua au kulinda mipaka, siasa na imani za dini za asili.

Kabila la Washubi lilikuwa milki kamili wakati Ujerumani ikiitwaa na kuitawala Tanganyika, Rwanda na Burundi. Milki ya Washubi iliendelea kuwepo hata wakati wa utawala wa Mwingereza.

Milki hiyo ilidumu hadi muda mfupi baada ya uhuru, wakati tawala za kichifu zilipoondolewa rasmi na serikali ya Tanganyika ili kuimarisha utaifa miongoni mwa Watanganyika na hatimaye Watanzania.

Eneo[hariri | hariri chanzo]

Kutokana na eneo la kijiografia la Washubi kuwa kubwa kuliko wingi wa watu, eneo hilo lilitawaliwa na uoto wa majani mengi na misitu ya savana. Hata hivyo, kutokana na kuingia kwa makundi makubwa ya wakimbizi kuanzia miaka ya 1960 na hasa miaka ya 1990 na 2000, kulitokea uharibifu mkubwa wa mazingira, kiasi cha kufanya upatikanaji wa nishati ya kuni kuwa shida kwa baadhi ya vijiji.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Kwa miaka mingi, jamii ya Washubi ilitegemea kilimo na ufugaji kwa ajili ya uchumi wao. Baadhi ya maeneo wanafuga mifugo mingi ikiwa ndiyo njia kuu ya uchumi. Aina ya ng'ombe wanaofugwa kwa wingi ni aina ya 'ankole' ambao kwa asili ni wakubwa na wana pembe ndefu. Hata hivyo kwa miaka ya karibuni wafugaji wamelazimika kuanza kufuga ng'ombe wenye pembe fupi ambao wanastahimili magonjwa.

Kwa ujumla unaweza kusema Washubi wanalima kilimo cha mchanganyiko wa mazao ya chakula, biashara na ufugaji. Mazao makuu ni migomba, mahindi, maharagwe, mtama, karanga na mihogo. Mifugo ni pamoja na ng'ombe, mbuzi, kondoo na kuku.

Utamaduni[hariri | hariri chanzo]

Chakula kikuu cha Washubi ni ndizi, ingawa, kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa zao la migomba, sasa ugali unachukuliwa pia kama moja ya vyakula muhimu.

Flag of Tanzania.svg Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Washubi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.