Wambunga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Wambunga ni kabila la watu mwa Tanzania [1] wanaoishi upande wa kaskazini mwa kabila laWapogolo, katika wilaya ya Kilombero (Ifakara), mkoani Morogoro. Lugha yao ni Kimbunga.

Mwaka 1987 ilikadiriwa kwamba idadi ya Wambuga ilikuwa 29,000.[2]

Historia[hariri | hariri chanzo]

Wambunga ni kabila dogo lililotokana na Wangoni baada ya mfarakano wa viongozi wa makundi yao walioingia katika eneo la Tanzania ya leo. Hivyo basi Wambunga ni Wangoni maseko (watafiti) walioingia Tanganyika kupitia kusini mashariki mwa Ruvuma wakiongozwa na kiongozi wa Wangoni Maseko Mputa.

Baada ya kutoelewana miongoni mwa makundi ya Wangoni kukapelekea chuki iliyosababisha viongozi wa makundi hayo kuuana wenyewe kwa wenyewe. Hivyo Mputa akauawa, na mwanae Malunda akawa mtawala wa kundi hilo. Baadaye Malunda akawa na wasiwasi wa maisha yake kutokana na hali hiyo, hivyo akaamua kurudi na kundi la Wangoni Maseko katika Malawi ya leo walikotokea awali.

Lakini katika hilo baadhi yao waligoma kurudi Malawi, ndipo baada ya Malunda kuondoka waliobaki wakahama Songea na kusogea mlima Mbunga ulioko pembezoni mwa mkoa wa Ruvuma. Baadaye, walipoona makundi ya Wangoni wakiendelea kupigana wao kwa wao, wakaamua kuondoka hapo mlima Mbunga na kuambaambaa Ulanga, hasa kwenye bonde la mto Kilombero.

Walijulikana kwa matamshi yao kuwa Wangoni, lakini wao walijiita Wambunga kwani wametokea mlima Mbunga. Hiyo ilitokana na kuchoshwa na vita, maana wote waliwatambua Wangoni kwa kupenda vita, kumbe kwa kusema hivyo wangebaki salama wenyeji wao wasiwadhuru, maana wakati huo Wangoni walishaanza uchokozi wa kivita na Munyigumba, kiongozi wa Wahehe.

Kwa sasa Wambunga wanapatikana zaidi katika maeneo yafuatayo: Ifakara mjini na vitongoji vyake, Kiberege na vitongoji vyake, Kisawasawa, baadhi ya maeneo ya Mang'ula, Mbingu na baadhi ya maeneo ya Mngeta: maeneo yote haya ni katika wilaya ya Kilombero. Wambunga wapo kwa wingi katika kijiji cha Kisaki, Morogoro vijijini, mkoani Morogoro. Pia wanapatikana katika wilaya ya Kisarawe, mkoa wa Pwani. Inasemekana baadhi ya Wambunga wapo katika maeneo ya nje ya Dar es Salaam.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Gorman, Anthony (2009). Stokes, Jamie (mhr.). Encyclopedia of the Peoples of Africa and the Middle East. Infobase Publishing inc. uk. 455. ISBN 978-0-8160-7158-6. Iliwekwa mnamo 14 Aprili 2012.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. "Official census records". Iliwekwa mnamo 14 Aprili 2012.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wambunga kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.