Walambya

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Walambya ni kabila la watu wanaoishi Tanzania katika Mkoa wa Mbeya, Wilaya ya Ileje na Wilaya ya Momba. Pia wako Malawi na Zambia. Lugha yao ni Kilambya.

Inasadikika kabla hawajafika Ileje (Old Bulambya) walitokea milima ya Livingstone (milima ya Ukinga).

Koo za Walambya ni kama: Mwashitete, Nyondo, Senka, Msongole, Mondya, Msomba, Siwale, Mwenitumba, Mwashifungwe, Kapenda, Kayinga, Kajiba, Kasanga, Kaponda, Sichinga, Kalinga, Mulagha, Kayela, Kapange, Kayuni, Simkonda, Mbela, Mbembela, Mwampashi, Shimwela, Simbeye, Kafwimbi, Kaponda, Kanyika, Sinkolongo, Kalagho, Mfungwe, Sinkala, Mushani, Mtambo, Sikwese, Fumbo, Haonga, Mwasenga, Mwazembe, Sichalwe, Silwamba, Siame, Mshiko, Panja, Muyila, Kayela, n.k.

Walambya wanaongozwa kifalme yaani na chifu, ambapo kiongozi wao mkubwa wa kabila huitwa Mwene, maana halisi ni mfalme. Mwene wao wa awali kabisa aliyeunganisha Bulambya na maeneo mengine ya Ileje alijulikana kwa jina la Mwenitumba ambaye alikuwa mkulima maarufu wa tumbaku (kwa Kilambya inaitwa itumba) na ndiyo chimbuko halisi la jina la makao makuu ya wilaya ya Ileje ambayo huitwa Itumba. Pia katika kata ya Itumba kuna mto unaoitwa Mto Itumba kunatokana na jina hilo la tumbaku. Hii pia ni kwa sababu huyo mtawala alikuwa analima tumbaku pembezoni mwa mto huo, hivyo wakaupa jina mto huo kwani tumbaku ilistawi sana pembezoni mwa mto huo. Kwa hiyo kiongozi huyo akapewa jina la Mwenitumba yaani mfalme wa tumbaku. Na toka zama hizo hilo jina likafanyika kuwa jina la cheo cha Chifu mkuu, pia alikuwa na jina la ukoo lililo julikana kama Sinkolongo, ambaye baadaye alimzaa Senka (Simbagaya). Japokuwa Senka si maarufu sana kwenye tawala za Walambya kwa sababu zifuatazo:

1. Senka Sinkolongo alivyokuwa madarakani kama chief inasadikika alipigana na mkoloni (Mjerumani). Hii ilipelekea kupinduliwa na mkoloni akishirikiana na baadhi ya makarani waliokuwa wakifanya kazi kwenye himaya ya Mwenitumba maarufu kama mwene wa Itumba. Baada ya mapinduzi hakukuwa na mtu wakuongoza uchifu wa Mwenitumba. Hivyo ililazimika aongoze kwa muda ndugu yake na Senka Sinkolongo ambaye alimuoa binti yake Senka, ndugu huyo alijulikana kwa jina la Lungwe (Mwampashi).

2. Baada ya mapinduzi ukoo wa Senka Sinkolongo ( Mwenitumba) wengi wao waliuawa na vibaraka wa mkoloni, na wachache walitawanyika kuelekea Chitipa (Malawi), Momba na Mbozi. Wachache walibaki Ileje ambao kwa leo wanapatikana Itumba Buswesi, Yuri, Mlale, Yenzebwe, Ishinga n.k. ukizungukia maeneo hayo utawakuta.

Bila kusahau Walambya ni mahiri kwenye vita vya jadi, kwa maana inasadikika walipigana na Mngoni vita na Mngoni akashindwa na Mlambya akashinda. Hii ni baada ya Mngoni kutoka Afrika Kusini akipita njia ya Malawi na kujikuta kaingia Bulambya (Ileje) na kwa sababu Walambya ni wakarimu wakamkaribisha wakampa hifadhi ng'ambo ya mto Itumba katika kijiji kilichopo katikati ya Yenzebwe na Lufingo kiitwacho Namangoni. Baadaye Wangoni wakaingiwa na tamaa wakataka kumpindua senior chief Mwenitumba, ndipo vilipigwa vita na Mngoni akasalimu amri baada ya kupokea kichapo toka kwa Mwenitumba (sinkolongo)[1].

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Chanzo cha historia hii ni kutoka kwa mzee Msongole, mzee Simbeye wa Mlale, mzee Senka wa Haseketwa Mbozi, mzee Mwampashi wa Mlale n.k.
Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Walambya kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.