Wakaguru

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mnara wa saa katika mkoa wa Morogoro

Wakaguru (au Wakagulu[1]) ni kabila la watu wa Tanzania ambalo ni mojawapo ya makabila makuu katika mkoa wa Morogoro[2]. Huko wanaishi hasa katika wilaya za Kilosa na Gairo. Pia wako katika mkoa wa Dodoma (Mpwapwa na Kongwa), Mkoa wa Manyara (Kiteto) na sasa wanatanuka zaidi maeneo ya Handeni na Kilindi mkoani Tanga.

Lugha yao ni Kikagulu.

Mtawala wao hujulikana kwa jina la Mundewa.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Ukifuatilia masimulizi ya wazee, hususan wakati wa sherehe za kumaliza msiba (mwidiki) yanaonesha kuwa Wakagulu walitokea maeneo ya Rwanda na Burundi (ya sasa).

Walitoka maeneo hayo kutokana na ukame uliokuwepo na matatizo mengine ya kivita.

Walipita maeneo mengi yakiwemo Konongo (Ukimbu), Mkoani Rukwa; baadaye walipita maeneo ya Mkoa wa Singida hadi wakaingia Rudi (Kusini mwa Mpwapwa).

Baada ya kuishi hapo kwa muda waliparamia Milima ya Ukaguru, lakini bado walikuwa na mawasiliano makubwa na watu wa Konongo.

Katika kuzunguka hapa na pale huko milimani ndipo zilipojitokeza koo mbalimbali za Wakagulu kutokana na matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiwapata wanawake.

Kwa msingi huo Wakagulu, kama Waluguru, Wakutu, Wazaramo na Wakwere wanafuata mfumojike, yaani ukoo wa mama ndio unaoongoza familia na watoto wote wanahesabiwa kuwa wa ukoo (welekwa) huo. Kwa mfano ukoo wa Wambigo ulipatikana baada ya wahenga kukanyaga maji yaliyokuwa yanajizungusha (Gakubiga) kwenye mto Mkondoa.

Mila na desturi[hariri | hariri chanzo]

Kufikia karne ya 18 mnamo mwaka 1776 kabila la Wakaguru lilikuwa linajulikana uwepo wake likiwa na mila na desturi zake ambazo ndizo miongozo na dira ya maisha ya kuelekeza jamii katika makuzi mazuri.

Vipengele vinavyohusisha mila na desturi za Wakaguru ni kama vile: jando na unyago, tambiko na uchawi, kumaliza misiba (mwidiki), kuzikana, ujenzi wa nyumba, ngoma za jadi na michezo, kusalimiana, elimu, ufundi, biashara na uchumi, kilimo na mazao, ndoa na mahari, ulinzi na usalama, ufugaji, utawala n.k.

Kufikia sasa zipo mila na desturi ambazo zinaendelezwa, wakati nyingine zimeachwa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na kuingiliwa na tamaduni nyingine. Humu huchambuliwa kwa undani kidogo ili kufahamu utamaduni wa Wakaguru tokea mwanzo na kuona mila zipi zinatakiwa ziendelezwe na zipi zipigwe vita kwa maana zimepitwa na wakati.

Jando na unyago[hariri | hariri chanzo]

Jando na unyago ni mafunzo ya jadi yanayotolewa kwa vijana wa kiume na wa kike kuwaandaa kwa maisha ya utu uzima. Mafunzo hayo yaliambatana na kutahiriwa/kukeketwa. Mafunzo haya yanatolewa kulingana na kitivoː kwa mfano, kitivo cha jando ni mafunzo kwa vijana wa kiume na unyago ni kitivo cha mafunzo ya vijana wa kike. Yote yakiwa na lengo la kuwaandaa vijana kuingia maisha ya utu uzima.

Jando ni kitendo cha kuwapeleka vijana wa kiume sunnah kwa lengo la kuwatahiri na kuwapa mafunzo ya jadi kulingana na utamaduni wa kabila husika. Jando la asili la Wakaguru lilikuwa kama ifuatavyo:

Siku moja kabla ya siku ya kutahiriwa, vijana (waluko) walinyolewa nywele za kichwani (kugetigwa) kama ishara ya kuwaandaa wali na hapo ngoma za jadi zilipigwa usiku kucha (nghoma ya mugono) yaani mpaka siku ya tukio. Ngoma hizo ni kama vile mkwaju ngoma (chidugo), igubi, (kayamba), kabati, mdumange, silanga (shilanga) au nyinginezo. Ngoma hizo zilipigwa zote au baadhi kutegemeana na uamuzi au uchumi wa mwenye sherehe kwa sababu walioalikwa walikula na kunywa pombe bure kwa gharama za mwenye sherehe.

Siku ya tukio la kutahiri, alfajiri kila kitu kilikuwa kimeandaliwa na pembe ya mnyama (igunda) ilipigwa kuashiria shughuli imeiva. Tofauti na kipindi hiki ambapo jando linaweza kufanyika kwa kutahiri hata mtu mmoja tena mambo yakaenda kisasa (kutahiri hospitalini), zamani Wakaguru waliwatahiri vijana wakiwa wengi tena waliokwisha balehe na kwa kundi, labda itokee yupo mmoja tu katika familia au ukoo. Hivyo siku hiyo wali (watahiriwa) walikusanywa na kupeleka sehemu ya tukio palipoitwa kuchibalu.

Walikusanywa sehemu moja ili kumrahisishia ngariba (muhunga) kuweza kufanyia kazi yake sehemu moja.

Walipokuwa wanasindikizwa kuelekea sehemu ya tukio, walifungwa nguo lubega bila ya nguo zaidi huku wakisindikizwa na nyimbo ikiwemo "namutema na majelee, sombwe eyaaa namutema na majele".

Baada ya kufika kwenye tukio (kuchibalu) vijana waliingizwa kwenye chemba ya sehemu maalumu ya kutahiria tayari kwa kumsubiri ngariba ambaye alikuwa wa kijadi pia, si daktari wa kisasa wa hospitalini.

Wakati ngariba alipokaribia sehemu ya tukio, pembe ya mnyama ilipulizwa kwa nguvu kuashiria mtaalamu amefika, kwa wale waoga ulikuwa ndio wakati wa kujikojolea.

Muda huo nyimbo mbalimbali ziliimbwa na ngoma ya igubi kupigwa ikiwa na wake kwa waume.

Ngariba alipoingia alikuwa hana salamu na mtu, na mara moja aliingia walikokuwako wali ili shughuli Luanda. Hapo wanawake hawakuruhusiwa kuingia kuona, ila wanaume tu, tena hata wanaume ambao hawajatahiriwa (walajoni) hawakuruhusiwa kuingia na kuona tukio. Kama iligundulika kuna mwanamume hajatahiriwa na anashuhudia tukio, hakutolewa nje bali alikamatwa kwa nguvu na kutahiriwa hata kama wazazi au walezi wake hawakupanga iwe hivyo. Aidha ilikuwa ruksa kwa mtu huyo kuingia na kutaka kutahiriwa kwa hiari (kigumila).

Wakati wa kutahiriwa vijana walipangwa katika mstari ili aanze mmoja na afuate mwingine, na kwa mila za Kikaguru kama kuna mtu na mdogo wake ilitakiwa aanze kutahiriwa mkubwa (Chilongola), ndipo afuate mdogo.Na kama kulikuwa na watoto wa mtu na dada yake ilitakiwa watangulie kutahiriwa wa dada (wa babamunu), ndipo wafuate wa kaka (iwana). Na hii ilikuwa hivyo kwa sababu dada ndiye anayeendeleza ukoo (ukungugo). [3]

Shughuli ilianza kwa kijana mmojammoja kukamatwa na mzee au kijana mwenye nguvu, hapo mtahiriwa alitolewa nguo iliyokuwa imefungwa lubega na kubaki kama alipozaliwa na kukalishwa chini na operesheni kuanza. Wakati huo ngoma za jadi huko nje ziliendelea kupigwa ili sauti za wanaotahiriwa, hasa wanaolia kwa maumivu, zisisikike, mfano wa wimbo ni "chailaila chelele ichibadya chailaila chelele".

Operesheni kwa kila mmoja ilifanyika kama dakika tatu kwa kutumia kisu kidogo kilichoitwa "lumo" na ilifanyika kwa uchungu mkali kwani zamani Wakaguru walitahiriwa bila ganzi za kutuliza maumivu. Hii ilipima ukomavu kwani ikitokea ukatahiriwa bila ganzi na usilie ulionekana ni mwanamume mkomavu. Japo desturi hiyo ilipotea na kuanza kutumia sindano za ganzi kabla ya kutahiri ili kupunguza maumivu ya tohara.

Ni dhahiri kwamba zamani, kabla ya kuibuka kwa magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi, kwa kushiriki vifaa vyenye ncha kali kama kisu, tohara ilifanyika kwa kutumia kisu kimoja au vichache kutahiri kundi kubwa. Hivyo walichanga kisu.

Baada ya shughuli ya tohara kuisha wali wanyamulusi) walikalishwa pembeni kwa kuvalishwa nguo lubega, na hapo hakuna aliyempa mwenzake pole wala hongera. Mara moja walipewa singa (mpunza) zilizotengeneza kwa vitambaa au nyuzi za wanyama, hasa ng`ombe, kwa ajili ya kufukuzia nzi wasitue kwenye majeraha.

Baada ya hapo walijitokeza vijana waliokwisha tahiriwa zamani na kuonesha sehemu zao za uume kwa waliotahiriwa siku hiyo ili kutoa wasiwasi kwamba ipo siku watapona na watakuwa kama wao.

Baada ya tukio kumalizika ngariba aliondoka kurudi kwake au kuendelea na ratiba yake, na kila kikundi kilikaa kwa masaa kadhaa na kurudishwa kambini (kikumbi) na kuanza maisha ya jandoni. Na kama wote walikuwa wa hapohapo (hachibalu) maelekezo ya kuanza maisha ya jandoni yalitolewa likiwemo la kukaa vizuri kwa kupanua miguu saa zote ili kuepuka kuumia kwa sehemu za jeraha zisigusane na sehemu nyingine za mwili, hasa mapaja.

Waliorudishwa kambini kwao walitembezwa polepole huku nyimbo zikiimbwa njiani hadi kwenye kambi yao moja kwa moja na hawakuruhusiwa kurudi tena nyumbani (ukaya). Ikumbukwe kuwa makazi ya jando yalijengwa mbali kidogo na makazi ya watu. hasa porini. ili mafunzo yote yanayotolewa huko, zikiwemo baadhi ya nyimbo na mizimu (figono), yasisikike kwa vijana ambao hawajatahiriwa na wanawake, ijapokuwa kwa kanda nyingine za Ukaguru baadhi ya wanawake walizijua.

Wakati wanyamulusi wamesharudishwa kambini siku hiyo na kuanza maisha ya jandoni huku nyumbani ngoma zilipigwa usiku kucha hadi siku iliyofuata watu walikula na kunywa pombe sana.

Kesho yake au zaidi ya siku hiyo mwenye shughuli alisitisha ngoma na kuwaamuru watu kurudi makwao vikiwemo vile vikundi vya ngoma na kutoa shukurani kwa ushiriki wao.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Lugha yao haina "r" ila "l"; vilevile haina "z" ina "f"
  2. Wakagulu
  3. Mzee mmoja kutoka kijiji cha Kibedya, mwl. David Chidaka, anasema: "mtoto wa dada ndiye anayeendeleza ukoo katika jamii zinazofuata ukoo wa mama (matrilineal societies), hivyo ni lazima aanze yeye kutahiriwa ndo wafuate watoto wa kaka".

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Bauer, Andreas, Street of Carvans
  • Beidelman, Thomas O, The Cool Knife
  • Beidelman, Thomas O, The Kagura
Flag of Tanzania.svg Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wakaguru kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.