Mizimu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mizimu inamaanisha hasa roho zilizoishi katika mwili kabla ya kuiaga dunia.

Katika baadhi ya dini na mila inaaminika kuwa mizimu inaweza kuwa na faida kwa watu walio hai duniani na ina uwezo wa kuwasiliana nao kwa kutumia njia mbalimbali kufuatana na mazingira au utamaduni.

Kuna tofauti kati ya mizimu; pengine ni roho za binadamu ambao hawakutimiza majukumu yao au walifanya kinyume wakati wapo duniani; pengine ni roho za watu walioshi kwa uadilifu.

Katika Kanisa Katoliki na baadhi ya madhehebu mengine, mizimu inaweza kuwa ya watakatifu.

Mizimu katika jadi za Afrika[hariri | hariri chanzo]

Watafiti mbalimbali walioangalia jamii za jadi katika Afrika walikuta imani katika mizimu. Imani hizo hazitokei Afrika tu, maana imani za kufanana zilitambuliwa pia katika dini za jadi katika mabara mengine kama vile Asia na Ulaya. Lakini kila jamii ina namna yake ya pekee ya kuwaza na kushughulikia imani hizo.

Kwa lugha ya Kiswahili, "mzimu" ni neno linalotaja pia mahali ambapo watu huwasiliana na roho za watu waliofariki dunia zamani.

Tena baadhi ya jamii za Kiafrika huamini kuna mizimu iliyoumbwa katika hali hiyo, yaani haikuwahi kuwa binadamu hapo kwanza.

Kwa hiyo, kuna imani ya mizimu ya aina mbalimbali: mizimu ambayo ni roho za watu waliokufa na mizimu ambayo haijawahi kuwa binadamu. Kwa kuwa mizimu ni roho, haina umbo maalumu, lakini ina uwezo wa kutokea katika maumbile tofautitofauti kama vile mtu, mnyama, mdudu, mimea, au vitu visivyo na uhai.

Kwa utamaduni wa Kiafrika, mizimu mizuri ni wahenga, yaani roho za watu ambao walipokuwa katika hali ya ubinadamu waliishi vizuri kulingana na tamaduni na matakwa ya jamii, walikuwa na sifa nzuri. Sasa ni mizimu mizuri ambayo hulenga kuilinda jamii au mtu mmojammoja dhidi ya matatizo. Hivyo, pale mtu anapokumbwa na matatizo wahenga humsaidia. Aidha, kufanikiwa au kutokufanikiwa kwa jamii katika masuala mbalimbali kunatokana na uhusiano wao na wahenga. Jamii inapaswa kufuata mila na desturi zake na kuepuka, kadiri iwezekanavyo, kuvunja miiko ya jamii kwa sababu kufanya hivyo kunawaudhi wahenga. Mtu anayefuata kanuni zote hulindwa, hupata mafanikio na kuishi kwa amani ilhali yule anayekiuka mila na desturi hupatwa na majanga makubwa au anaweza kuiingiza jamii nzima katika matatizo kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wahenga kujitoa katika ulinzi na hivyo kuyaachia mizimu mibaya nafasi ya kufanya mambo mabaya, au wahenga wenyewe kutoa adhabu kwa jamii au kwa mtu mmojammoja.

Aidha, inasadikiwa kuna mizimu mibaya, ambayo malengo yao ni kuidhuru jamii na wakati mwingine hujitokeza kama pepo ambao huwaingia na kuwadhuru watu; hao huitwa kwa majina tofautitofauti kama vile misoha, irumenang, na’ndenga na war’umu kwa Wabena, Wamasai, Wamakonde na Wachaga. Baada ya Uislamu na Ukristo kuenea barani Afrika kusini kwa Sahara yanatumika pia majina yanatokana na lugha ya Kiarabu kama mashetani au majini ambayo kwa asili yana maana tofauti. Hao mizimu mibaya huwa na kinyume cha sifa hizo hapo juu, yaani walipokuwa binadamu waliishi katika hali isiyotakiwa katika jamii au inayochukuliwa kuwa ni ya kutia aibu, halafu kufa katika hali inayochukuliwa kuwa ni ya laana, kama vile kujinyonga au kuzikwa bila kufuata mila na desturi za jamii. Kwa mfano, Wanyore wa Kenya huamini kuwa mwanamume au mwanamke anayefariki dunia kabla hajaoa au kuolewa atataka kuzuia wengine kuoa au kuolewa na kuzaa. Kwa hiyo, kabla ya miili ya wanaume na wanawake hao kuzikwa, inafanyiwa miviga ili kuzuia tatizo hilo lisienee kwa wengine. Aidha, inasadikiwa kuwa baadhi ya mizimu mibaya hutokana na watoto ambao walikufa kabla ya kuzaliwa: hao huidhuru jamii kwa sababu huwa na hasira na hutaka kulipa kisasi.

Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.