Mkoa wa Tanga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Tanga

Majiranukta kwenye ramani: 5°18′15″S 38°19′3″E / 5.30417°S 38.3175°E / -5.30417; 38.3175

Mkoa wa Tanga
Mahali pa Mkoa wa Tanga katika Tanzania
Mahali pa Mkoa wa Tanga katika Tanzania
Majiranukta: 5°0′S 38°15′E / 5°S 38.25°E / -5; 38.25
Nchi Tanzania
Wilaya 6
Mji mkuu Tanga
Serikali
 - Mkuu wa Mkoa Martin Shigela
Eneo
 - Mkoa 27,348 km²
Idadi ya wakazi (2012)
 - 2,045,205
Tovuti: http://www.tanga.go.tz/
Milima ya Usambara Magharibi.

Mkoa wa Tanga ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania na uko Kaskazini Mashariki mwa nchi, ukipakana na Kenya upande wa Kaskazini, Bahari Hindi upande wa mashariki na mikoa ya Morogoro, Manyara na Kilimanjaro wenye Postikodi namba 21000. Mpaka upande wa kusini unafuata mto Mligaji kuutenganisha na mkoa wa Pwani.

Makao makuu yako Tanga mjini.

Eneo la mkoa[hariri | hariri chanzo]

Tanga ni kati ya mikoa midogo ya Tanzania ikiwa na msongamano mkubwa wa wakazi ndani ya eneo lake. Msongamano ni mkubwa hasa wilaya ya Lushoto kwenye ardhi yenye rutuba nzuri.

Mkoa una eneo la km² 27,348 ambalo linaunganisha sehemu za pwani pamoja na milima ya ndani kama Usambara.

Eneo linalofaa kwa kilimo ni km² 17,000.

Kuna wilaya 10 ambazo ni Handeni Vijijini, Handeni Mjini, Kilindi, Korogwe Vijijini, Korogwe Mjini, Lushoto, Mkinga, Muheza, Pangani na Tanga Mjini.

Hali ya hewa[hariri | hariri chanzo]

Kwa jumla hali ya hewa ni joto lenye unyevu. Handeni kuna joto kavu zaidi. Milima ya Usambara hakuna joto sana.

Miezi ya Desemba - Machi halijoto huko Tanga inafikia sentigredi 30-32 mchana na 26-29 usiku. Wakati wa Mei hadi Oktoba halijota inapoa: ni sentigredi 23-28 mchana na 20-24 usiku. Unyevu iko juu kati ya asilimia 100 na asilimia 65.

Maeneo mengi ya mkoa hupokea angalau milimita 750 za mvua kwa mwaka au zaidi. Pwani ni zaidi: takriban milimita 1,100 hadi 1,400 ikipungua sehemu za ndani isipokuwa milima ya Usambara ambako mvua inaweza kuzidi milimita 2000 kwa mwaka.

Wakazi[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 2012 wakazi waliohesabiwa katika sensa walikuwa 2,045,205[1].

Makabila makubwa mkoani Tanga ni Wasambaa, Wazigua, Wabondei na Wadigo. Mengine ni Wapare, Wataita, Wambugu, Wasegeju na Wanago.

Pia kuna Waarabu wengiwengi wenye asili ya Oman.

Wasambaa ndio kabila kubwa lililoko katika milima ya Usambara, Muheza, Korogwe na Lushoto. Kwa jumla ndio asilimia 40 ya wakazi wote wa mkoa.

Wazigua ni kabila kubwa huko Handeni na sehemu za Korogwe na Pangani. Wabondei wako hasa Muheza na sehemu za Pangani. Wadigo ndio wengi Tanga yenyewe na sehemu za pwani.

Elimu[hariri | hariri chanzo]

Katika mkoa huu elimu inahitaji kuboreshwa zaidi, hasa maeneo ya vijijini, maana watu wengi wa mkoa huu hufanya shughuli zao za kimila; hali hiyo huwafanya kushindwa kuendelea na shughuli za kimaendeleo katika taifa la Tanzania.

Wilaya ya Handeni kuna machimbo ya madini, ila kuhusu elimu ipo nyuma sana kwani mpaka sasa hakuna shule ya sekondari inayotoa huduma ya kidato cha tano na sita. Kama haitoshi shule za watu binafsi hakuna hata moja.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Mkulima akionyesha pilipili mtama kutoka kwenye shamba lake, Magoroto - Tanga.

Wakazi wengi hutegemea kilimo cha riziki pamoja na ufugaji na uvuvi.

Mazao ya chakula hasa ni mahindi, muhogo, ndizi, maharagwe na mpunga.

Tanga ilikuwa na viwanda vingi kiasi katika miaka ya 1960 na 1970 lakini karibu vyote vimekwama kutokana na siasa ya Ujamaa na uchumi wake ulioiga mfumo wa nchi za kisoshalisti. Viwanda vichache vilivyobaki havizalishi mali kulingana na uwezo wao. Kilichobaki hasa ni kiwanda cha saruji Tanga.

Utalii umeanza kupanuka kidogo, hasa katika eneo la Pangani, Mapango ya Amboni na kituo cha Makumbusho Urithi Tanga.

Majimbo ya bunge[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015 mkoa huu ulikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo:

Wakuu wa wilaya tangu waaapishwe tarehe 29 Juni 2016[hariri | hariri chanzo]

1.     Tanga            -           Thobias Mwilapwa.

2.     Muheza         -           Mhandisi Mwanaisha Rajab Tumbo.

3.     Mkinga          -           Yona Lucas Maki.

4.     Pangani         -           Zainab Abdallah Issa.

5.     Handeni       -           Godwin Crydon Gondwe.

6.     Korogwe       -           Robert Gabriel.

7.     Kilindi                      -           Sauda Salum Mtondoo.

8.     Lushoto        -           Januari Sigareti Lugangika.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Population Distribution by Administrative Units, United Republic of Tanzania, 2013. National Bureau of Statistics, Ministry of Finance, Dar es Salaam and Office of Chief Government Statistician, President’s Office, Zanzibar (March 2013). Jalada kutoka ya awali juu ya 2013-05-02. Iliwekwa mnamo 2017-08-22.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]