Mkoa wa Mara
Mkoa wa Mara | |
![]() |
|
Majiranukta: 1°33′S 34°1′E / 1.550°S 34.017°E | |
Nchi | Tanzania |
---|---|
Wilaya | 7 |
Mji mkuu | Musoma |
Serikali | |
- Mkuu wa Mkoa | |
Eneo | |
- Jumla | 30,150 km² |
- Kavu | 19,208 km² |
- Maji | 10,942 km² |
Idadi ya wakazi (2022) | |
- Wakazi kwa ujumla | 2,372,015 |
Tovuti: http://www.mara.go.tz/ |
Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania. Unapakana na Kenya upande wa mashariki, mikoa jirani ya Mwanza na Simiyu upande wa kusini, Arusha upande wa kusini-mashariki, hatimaye Ziwa Nyanza (au Viktoria) upande wa magharibi. Jina linatokana na lile la mto Mara. Eneo la mkoa ni la km2 30,150, lakini kwa asilimia 36 ni maji. Sehemu kubwa ya Hifadhi ya Wanyama ya Serengeti iko ndani ya Mkoa wa Mara. Idadi ya wakazi ilikuwa 2,372,015 wakati wa sensa ya mwaka 2022[1], kutoka 1,743,830 wa sensa ya mwaka 2012 [2], na 1,368,602 wa sensa ya 2002[3]. Musoma ndio makao makuu ya mkoa.
Kuna wilaya 9 zifuatazo katika mkoa wa Mara: Bunda Mjini, Bunda Vijijini, Serengeti, Tarime Vijijini, Tarime Mjini, Rorya, Butiama, Musoma mjini na Musoma vijijini.
Una postikodi namba 31000.
Makabila
Makabila ya Mara ni mengi kuliko mikoa yote ya Tanzania, kama vile Waluo, Wajita, Waruri, Wazanaki, Wakuria, Wakabwa, Wakiroba, Wasimbiti, Wangoreme, Wakwaya, Waikoma, Wanata, Waisenye, Waikizu, Wasizaki, Wasukuma, Wataturu na makabila madogo kama Wanandi, Wakisii au Wamaragori.
Kuna jumla ya makabila 30 yanayodai kujitegemea. Jamii zinazosahaulika huunganishwa katika kundi la Wasuba (Wategi, ambao pia huitwa Abhathegi maarufu kama Abhagirango, Waugu, Warieri, Wakine, Wasweta na Waganjo, Wagire, Wakiseru, Wakamageta na Waturi). Baadhi ya jamii hizo zilimezwa na mila, lugha na desturi za Waluo zikaitwa Suba-Luo.
Baadhi ya jamii kwa upande wa Kenya iliyotawaliwa na Waingereza katika kaunti za Migori na Homa Bay huitwa Wasuna, Wagwasi, Waungoe, Wakajulu na Wakadem. Hata hivyo habari hizi bado zinafanyiwa utafiti kuangalia muingiliano wa lugha na tofauti za kilahaja kati ya jamii moja na nyingine hasa zilizopo Tanzania. Itakumbukwa jamii nyingi ziliingia upande wa Kenya kabla ya nchi za Afrika Mashariki kupata uhuru. Zipo tafiti nyingi siku hizi ambazo zinajaribu kubainisha makundi ya jamii hizo lakini muingiliano bado haujapatiwa ufafanuzi makini.
Kimsingi Mkoa wa Mara una jamii hizo zipatazo 30 lakini lugha kuu ni saba tu na nyingine ni lahaja kutokana na makundi ya lugha hizi: Luo, Kuria, Sukuma, Suba, Shashi, Zanaki na Taturu. Yapo makundi ya Wanata, Waisenye na Wataturu, Wazanaki (kundi lake: Kabwa, Kirobha, Wasimbiti, Wairienyi, Waikizu, Wangoreme), Luo (Wakowak, Wakamoti), Wakuria (Nyebhasi, Nyamongo, Wanchari, Wasweta, Wakenye, Warenchoka, Watimbaru, Waregi, hadi 14/15), Sukuma, Nyantuzu na Shashi (Wajita, Wakwaya, Waruri, Wakerewe, Wakara). Jamii zote humezwa katika makundi saba ya lugha kuu lakini kila jamii inajitofautisha kwa lahaja yake.
Ni jamii za Kibantu peke yake zinazoweza kuwasiliana na kuelewana kukiwa na tofauti kidogo katika matamshi ya maneno.
Ukichunguza zaidi, wakazi wa asili wa Mkoa wa Mara ni makabila makuu mawili yenye uhusiano wa karibu sana, yaani Wakurya (na vikabila kadhaa: Wakurya ni jina ‘linalobeba’ mengi ya yale yanaoyoitwa 'makabila' mkoani Mara, ambayo tafsiri yake halisi ni 'vikabila'[4]) na Wajita (hawa nao wana vikabila kadhaa).
Pia, Wakurya-Waghusii si 'Bantu halisi' bali ni mchanganyiko kati ya Wabantu na Waniloti. Katika makabila ya Kibantu, yaliyoathiri damu ya Wakurya ni pamoja na:
- Wasukuma (kwa mfano, baadhi ya koo za Kizanaki, zilichanganya damu sana na Wasukuma)
- Wachaga (kwa mfano, Wakerobha au Wakiroba, walichanganya damu sana na wahamiaji toka Machame na Marangu kwa Wachaga - na hadi leo Machame na Marangu ni majina ya vitongoji huko kwa Wakiroba Mkoa wa Mara!)
- Wakikuyu (kwa mfano, baadhi ya Wakurya wa Kenya wana asili ya Wakikuyu au 'Abhaghekoyo'). Pia Wakikuyu wanachanga majina mengi na Wakurya - kama Nyambura, Murughi, Mwita, n.k. na hata lugha zinafanana kwa kiasi kikubwa. Pia, kama makabila, Wakurya-Waghusii, Wakikuyu, na Wameru wa Kenya wana uhusiano wa karibu na asili moja.
- Makabila mengine yanayohusiana nao ni Wagisu (Uganda) na Waluhya (Kenya). Kuna wakati ambapo makundi hayo yote yalikuwa kabila moja, lakini wakatengana kwa kuhamia sehemu za mbali, wakawa makabila tofauti tunayoyajua leo.
Waniloti waliochanganya damu na Wakurya ni pamoja na:
- Wamasai (baadhi ya koo za Wakurya wa leo zilitoka Umasai).
- Wajaluo (hasa kutokana na ujirani baada ya ujio wa Waniloti Mkoani Mara),
- Wakalenjin (hasa kutokana na uhamiaji na pia wote kuwa na mila za wafugaji).
Kwa hiyo, dhana ambayo imejengeka sana vichwani mwa watu kwamba Mara kuna makabila mengi, kwa kiasi kikubwa ni potofu. Ukiangalia kwa undani hata lugha na mila zilizopo, utaona kwamba hata hao kina yego/mbani (Wajita, Wakwaya, Wakara, Waruri, Wakerewe, n.k.) ni 'vikabila' tu vya kabila kubwa la Wajita.
Ukiachia Wajaluo (au 'Jakowiny Luo'), mkoani Mara pia kuna Wataturu na Wanandi. Wanandi ni moja kati ya 'vikabila' vya Wakalenjin. Hata hivyo, idadi ya watu wa makabila haya ni ndogo ukilinganisha na ile ya 'Wakurya-Waghusii' na Wajita (ikiwa na maana ya kabila kubwa linalojumuisha pia Wakwaya, na Waruri).
Pia Mara, Wakurya hawaishi tu Tarime, bali huishi wilaya zote 6 za Mkoa wa Mara: Tarime, Rorya (hao ni Wakurya wa North Mara), Musoma Vijjini, Musoma Mjini, Bunda, na Serengeti (hao ndio Wakurya wa South Mara). Abhaghusii (wanaoishi eneo la Nyanza, Kenya) ni sehemu ya Wakurya wa 'North Mara'.
Kwa hiyo, wanahistoria wanatakiwa kuliweka hili sawa. Wazungu walichorekodi ni majina ya vikabila (au koo kubwa).
Kwa wakereketwa wa historia, Wakiroba (kikabila cha Wakurya-Wakisii) na Wakwaya (kikabila cha Wajita) ndiyo wakazi asili ya inayoitwa leo hii Musoma mjini. Makundi hayo mawili, pamoja na kuwa makabila tofauti, yana uhusiano wa muda mrefu wa karibu sana. Hupendana, na hata vita walipigana kwa kushirikiana!
Pia Wakurya na Wajita, uhusiano wao wa karibu, na hata kushabihiana kwa lugha zao (makabila hayo makubwa mawili, hakuna anayeweza akamsengenya mwenzie, na asijue anasema nini), si jambo lililoanza juzi. Mababu walisimulia hao wote wamehamia Mara, wakitokea maeneo ambayo kwa sasa yako katika nchi zinazojulikana kama Misri na Libya (hata Wajaluo nao, walikuja toka huko). Wakati wa msafara, waligawanyika makundi matatu:
• Moja likapita mashariki mwa Ziwa Viktoria. Hili lilikuwa ndilo kundi kuu. Koo nyingi za Kikurya zilipita huko. Katika nyakati tofauti, zilitengana na Wagisu (Uganda), Waluhya, Wameru, Wakikuyu (Kenya).
• Moja likapita magharibi mwa Ziwa Viktoria. Koo nyingi za Wajita, pamoja na baadhi ya koo za Wakurya (kama Abhashanake) walipita huko.
• Moja likapita katikati ya Ziwa Viktoria. Hili kundi lilikuwa dogo zaidi. Lilijumuisha zaidi koo chache za Kijita, kama vile Wakerewe.
Hakuna historia ya vita kati ya Wakurya na Wajita, bali wameishi kwa kuelewana na kusaidiana. Hata hivyo, koo za Kikurya hupenda sana kupigana hadi leo hii.
Pia tukumbuke: Wabantu ni familia moja, na Waafrika ni ’kabila’ moja kubwa, na binadamu wote, bila kujali rangi, wametoka kwa Muumba mmoja na wana asili moja – ni watoto wa Adamu na Eva (Waarabu humwita Hawa), kwa wale wanaoamini dini; au ni watoto wa Mwafrika kwa wale wanaoamini sayansi.
Majimbo ya bunge
Wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015 mkoa huu ulikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo:
- Bunda Mjini : mbunge ni Esther Bulaya (Chadema)
- Bunda Vijijini : mbunge ni Boniface Mwita Getere (CCM)
- Butiama : mbunge ni Nimrod Mkono (CCM)
- Musoma Mjini : mbunge ni Vedastus Mathayo Manyinyi (CCM)
- Musoma Vijijini : mbunge ni Prof. Sospeter Muhongo (CCM)
- Mwibara : mbunge ni Kangi Lugola (CCM)
- Rorya : mbunge ni Lameck Airo (CCM)
- Serengeti : mbunge ni Mwalimu Marwa Ryoba (Chadema)
- Tarime Vijijini : mbunge ni John Heche (Chadema)
- Tarime Mjini : mbunge ni Ester Matiko (Chadema)
Tazama pia
Marejeo
- ↑ https://www.nbs.go.tz
- ↑ Sensa ya 2012, Mara Region
- ↑ "Mara Region Homepage for the 2002 Tanzania National Census". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2003-12-15. Iliwekwa mnamo 2003-12-15.
- ↑ Kwa hiyo unapotaja 'vikabila' vya Wakurya, kwa usahihi, utataja, pamoja na vinginevyo: Abhatimbaru (Watimbaru), Abhakira (Wakira), Abhanyamongo (Wanyamongo), Abhasubha (Wasuba), Abhakerobha (Wakiroba), Abhakabhwa (Wakabwa), Abhasimbete (Wasimbiti), Abhaikoma (Waikoma), Abhangoreme (Wangoreme), Abhaisenye (Waisenye), Abhanyabhasi (Wanyabasi), Abhaireghe (Wairege) n.k. bila kuwasahau Abhaghusii (Wakisii). Kihistoria, Wakurya (Abhakurya, Abhakorya) na Wakisii ('Waghusii' au 'Abhaghusii' tukitumia maneno sanifu katika lugha husika) ni kabila moja. Tofauti ndogo zilizopo katika lugha ni za kijiografia tu. Hata Abhashanake (Wazanaki), Abhaighisho (Waikizu), Abhanatta (Wanata), n.k. ni 'vikabila' tu vya Wakurya. Makundi yote hayo ni makundi ya 'Mura' (sawa na Morani kwa Wamasai) na 'Bhei' (kwa jinsia ya kike). Tamaduni zao ni zilezile - kutahiri wanawake kwa wanaume, kuchonga meno (hata Mwalimu jina lake la utani ni 'Mchonga'), kuwa na sera ya marika (kama Abhaghini, Abhanyambureti, n.k.) yanayozunguka vizazi hata vizazi na kujirudia, kuwa na 'Ekesero' kama kundi la watu waliotahiriwa wakati mmoja, ambao lilikuja kuwa msingi wa majina ya 'intakes' za JKT), n.k.
Viungo vya nje
- Tanzanian Government Directory Database (Kiingereza)
- Historia ya Mkoa wa Mara (Kiswahili)
![]() | |
---|---|
Arusha | Dar es Salaam | Dodoma | Geita | Iringa | Kagera | Katavi | Kigoma | Kilimanjaro | Lindi | Manyara | Mara | Mbeya | Morogoro | Mtwara | Mwanza | Njombe | Pemba Kaskazini | Pemba Kusini | Pwani | Rukwa | Ruvuma | Shinyanga | Simiyu | Singida | Songwe | Tabora | Tanga | Unguja Kaskazini | Unguja Kusini | Unguja Mjini Magharibi |
![]() |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mara bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Mkoa wa Mara kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Usiingize majina ya viongozi au maafisa wa sasa maana wanabadilika haraka mno. |