Wakwaya
Wakwaya ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi kwa wingi katika wilaya za Musoma mjini na Musoma vijijini, katika Mkoa wa Mara, pwani kabisa mwa Ziwa Viktoria. Mwaka 1987 walikadiriwa kuwa 102,000 hivi[1].
Lugha yao ni Kikwaya, mojawapo ya lugha za Kibantu katika jamii ya lugha za Kiniger-Kongo. Inaendana hasa na Kijita, Kiruri, Kiregi, Kikabwa, Kisimbiti, Kikara, Kikerewe, Kizinza, Kihangaza pamoja na Kiha, hivyo watu wa lugha hizo huelewana.
Eneo wanaloishi huitwa Bukwaya; linapatikana katika mwelekeo wa 1°30' hadi 1°40'S na 33°40 hadi 33°50'E, likijumuisha kata mbalimbali kama vile Etaro, Nyegina, Nyakatende, Ifulifu, Mkirira, Buhare pamoja na Bisumwa. Pia Wakwaya na Wakiroba ndio makabila halisi la Musoma mjini. Hata jina lenyewe la Musoma limetokana na neno la Kikwaya Omusoma ambalo linamaanisha eneo la nchi kavu lililoingia majini. Kutokana na Wazungu kushindwa kutamka neno hilo wakati wa ukoloni waliita Musoma ambalo linatumika hadi leo.
Asili ya jina la Wakwaya limetokana na aina ya ndege aitwaye tai au mwewe ambaye kwa Kikwaya huitwa mukwaya; ndege huyu inasadikika alimsaidia mtoto wakati alipokuwa na njaa ambapo alimdondoshea chakula na kumuokoa maisha yake.
Wakwaya wametokana na Wakwiregi ambalo pia ni kabila la mkoani Mara. Kabila hili haliongelewi sana kutokana na kuwa na idadi ndogo ya watu, pia kumezwa na kabila la Wajita ambalo kwa kiasi fulani huendana nao sana kwani watu wa jamii hizo mbili hawawezi kusengenyana. Pia kabila hili huendana kwa karibu na Waruri ambao hupatikana jirani sana na eneo la Bukwaya. Tena kabila hili huendana na Wakerewe na hata mila na desturi za jamii hizo huendana sana.
Shughuli za kiuchumi za jamii hii ya Kikwaya ni ufugaji, uvuvi pamoja na kilimo. Ingawa idadi ndogo ya watu hujipatia kipato kutokana na uchimbaji mdogomdogo wa madini aina ya dhahabu ambayo hupatikana katika kijiji cha Kigera Etuma katika machimbo ya Ekungu.
Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wakwaya kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |