Wawanji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Wawanji ni kabila kutoka wilaya ya Makete, katika milima ya Kipengere ya Mkoa wa Njombe, sehemu ya kusini ya nchi Tanzania.

Mwaka 2003 idadi ya Wawanji ilikadiriwa kuwa 28,000[1]. Lugha yao ni Kiwanji.

Wawanji ni majirani kabisa wa kabila la Wakinga. Wawanji na Wakinga wamepakanishwa na hifadhi ya Kitulo. Asilimia kubwa ya Wawanji wapo sehemu za Ikuwo na Matamba, maarufu kama bonde la Uwanji.

Historia ya Wawanji[hariri | hariri chanzo]

Inasemekana Wawanji walitokea Dodoma katika kabila la Wagogo; uthibitisho wa hilo ni kwamba majina mengi ya koo za Kigogo na Kiwanji zinafanana. Tofauti ipo katika matamshi ambayo yaliathiriwa na lafudhi ya mahali walipofika wazee wa zamani walipotoka Ugogo kwenda kusini. Kwa mfano, Wagogo wana Msemwa ila Wawanji wana Nsemwa, Wagogo wana Mgogo ila Wawanji wana Ngogo, Wagogo wana Mkinda ila Wawanji wana Nkinda. Hii inaonyesha jinsi gani asili ya watu hao ilivyo moja, ila imebadilika kutokana na uhamaji ambao ni moja ya tabia ya viumbe hai. Kwa maana hiyo, ukitaka kuita majina ya koo za Kiwanji mengi yanaanza na N'.

Mahusiano ya Wawanji na makabila mengine[hariri | hariri chanzo]

Uchunguzi uliofanyika kwa kipindi kirefu umebaini kuwa Wawanji ni watu wakarimu sana na kupokea wageni wa aina yoyote bila ubaguzi. Uthibitisho wa hili ni pale wanapoonekana kuishi vyema na makabila yaliyowazunguka kama Wakinga, Wabena, Wanyakyusa, Wasafwa na wengine; pia wanaweza kuoana na makabila yote Tanzania bila kipingamizi.

Pia ukarimu huu ulionekana miaka mingi iliyopita, kwani mababu waliotokea Ugogo waliishi vyema na makibila jirani, kiasi cha kusahau lugha yao ya Kigogo na kuunda lugha mpya ya Kiwanji yenye misamiati ambukizi toka makabila jirani.

Mwisho makabila jirani huamini kuwa huwezi kufika nyumbani kwa Mwanji ukaondoka bila chakula na pia kama ukienda na chakula chako basi, mtakila wote na wewe utakula chakula chao.

Mazao maarufu yanayostawishwa katika bonde hili ni kama: mahindi, ngano, maharagwe, njegere, viazi mviringo, na kwa kiasi kidogo mtama na ulezi. Lakini pia kuna pareto kama zao la biashara.

Dini na ushirikina[hariri | hariri chanzo]

Idadi kubwa ya Wawanji ni Wakristo, wanamwamini Yesu Kristo. Pia Waislamu wapo, lakini si kwa idadi kubwa: kila watu 10 Mwislamu ni mmoja au hakuna kabisa. Hii inajidhihirisha wazi kutokana na kuwepo kwa makanisa mengi kuliko misikiti, mfano mji wa Matamba una msikiti mmoja ambao unafanana na nyumba ya mtu ya kuishi eneo la Mahanji, lakini makanisa ni mengi mno, yapo kila kitongoji.

Pia Wawanji wanasadikika kuwa washirikina toka enzi; ushirikina wao ni wa pekee, unatofautiana na makabila yote Tanzania, na unajulikana kama Wanyambuda. Ushirikina huo umesambaa na unakua na kuenea kwa kasi zaidi miaka ya 2010. Zamani walikuwa ni wazee lakini miaka hii mpaka vijana wanaomaliza elimu za sekondari wanapewa aina hii ya ushirikina. Kazi yao kubwa ni kula watu, yaani wanaamini kuwa wanaweza wakakuua kiuchawi na ukaendelea kuishi hata zaidi ya wiki, huku wakiwa tayari wameshakula vitu vya ndani kama ulimi, utumbo na ini. Hivyo mgonjwa anaweza akalazwa hospitali, kumbe ameshaliwa viungo vyake vya ndani.

Wana sayansi ya ajabu ambayo huwezi kuona hata walipotolea hiyo nyama ila kuna wazee wataalamu ndio hutambua hilo mapema na wanawajua mpaka waliohusika. Uchawi huo huenezwa kutoka familia moja kwenda nyingine kwa njia ya pombe kwenye vilabu vya kienyeji. Hata kama ulikuwa mtu mwema, kama ni mnywaji wa pombe za kienyeji unakuwa kwenye hatari ya kupata huo uchawi.

Lakini hawa Wanyambuda hawawezi kumuua mgeni au mtu wasiyemjua, ila wanachokifanya ni kila mshirika ambaye yupo kwenye hicho kikundi cha Unyambuda anatoa sadaka ya mtu ampendaye kutoka katika familia yake: anaweza kumtoa mtoto wake mpendwa, au mama yake, au mke wake, au hata mjomba na shangazi ili mradi ana undugu naye. Kikundi kinapendekeza mtu ambaye ni mpendwa kwako, ikitokea unashindwa kutoa sadaka, basi kikundi kinapendekeza kukuua mwenyewe, na lazima uawe tu.

Hii hali imepelekea kuhama kwa vijana pindi tu wanapomaliza elimu zao za sekondari, kwani kijana aliYesoma na anaYeonekana ni msaada mkubwa kwa familia yake, huyo ndiye kipaumbele kikubwa kutolewa sadaka na wazazi wake au ndugu zake. Hii imepelekea vijana wengi kuhamia mjini na waliofanikiwa kimaisha wanashindwa kutoa msaada nyumbani kwao au hata kuwajengea wazazi wao nyumba nzuri, wakihofiwa kuuawa na mzazi au mtoto mwenyewe. Kwa jina lingine wanaitwa Freemasons wa Uwanji.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Vwanji. A language of Tanzania.
Flag of Tanzania.svg Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wawanji kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.