Hifadhi ya Kitulo
Hifadhi ya Kitulo ni hifadhi ya taifa la Tanzania iliyopo katika mikoa ya Mbeya na Njombe.
Awali ilijulikana kama Elton Plateau baada ya mvumbuzi Fredrick Elton kupita eneo hili mnamo mwaka 1870.
Mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) lilichukua eneo hili kwa ajili ya ukulima wa ngano na ufugaji wa kondoo.
Baadaye likageuzwa kuwa shamba la ng'ombe ambalo lipo hadi leo. Kutokana na umuhimu wa eneo hili wadau mbalimbali wa mazingira walipendekeza eneo hili litangazwe kuwa hifadhi ya taifa ili kulinda umaridadi wa maua na mimea adimu inayopatikana ndani ya eneo hili.
Mwaka 2005, Kitulo ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa ikijumuisha sehemu ya eneo la shamba la mifugo, Msitu wa Livingstone na bonde la Numbi kiasi cha kilometa za mraba 412.9 ndani ya mwinuko wa mita 2100 na 3000 juu ya UB.
Hifadhi hii inasifika kwa kuwa na maua aina mbalimbali na zaidi ya aina 30 hupatikana Kitulo pekee na maeneo kusini mwa Tanzania.
Pia ndilo eneo pekee Tanzania ambapo ndege aina ya Tandawili machaka (Denhams Bustard) wana makazi. Wapo aina mbalimbali ya ndege kama vile Mpasua mbegu mweusi (Kipengere seed eater) na wengineo.
Jamii mpya ya nyani (Lophocebus Kipunji) waligunduliwa mwaka 2003 Kitulo. Hifadhi hii ina uwanda wa tambarare, mabonde, vilima na maporomoko ya maji. Ndani ya msitu, kuna miti aina ya cidar yenye urefu wa zaidi ya mita 50 na inakadiriwa kuwa mirefu kuliko yote duniani.
Kitulo inafikika kwa gari kutoka Chimala, eneo lenye maajabu ya kijiolojia, kilometa 78 mashariki kwa mji wa Mbeya. Pia unaweza kufika ukitokea Zambia kupitia Tunduma au Malawi kupitia Karonga kwa barabara.
Reli ya TAZARA hupita karibu na hifadhi ya Kitulo.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Orodha ya milima ya Tanzania
- Mbuga za Taifa la Tanzania
- Orodha ya milima ya mkoa wa Mbeya
- Orodha ya milima ya mkoa wa Njombe
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]Majarida ya hifadhi za Taifa Tanzania
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- TANAPA
- Utalii wa Tanzania Ilihifadhiwa 13 Januari 2010 kwenye Wayback Machine.
- Safiri Tanzania
- Maliasili za Tanzania
Makala hii kuhusu maeneo ya Tanzania bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Hifadhi ya Kitulo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno. |