Mbeya (mji)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Jiji la Mbeya
Mlima wa Loleza juu ya mji wa Mbeya
Mlima wa Loleza juu ya mji wa Mbeya
Jiji la Mbeya is located in Tanzania
Jiji la Mbeya
Jiji la Mbeya
Mahali pa mji wa Mbeya katika Tanzania
Anwani ya kijiografia: 8°53′24″S 33°25′48″E / 8.89°S 33.43°E / -8.89; 33.43
Nchi Tanzania
Mkoa Mbeya
Wilaya Mbeya Mjini
Idadi ya wakazi
 - 300,000

Mji wa Mbeya ni mji mkubwa kusini-magharibi ya Tanzania. Mbeya ni kitovu cha Nyanda za Juu za Kusini ambazo ni eneo la uzalishaji wa mazao mengi. Ni makao makuu ya mkoa na wilaya.

Jiografia[hariri | hariri chanzo]

Mji umeenea katika bonde kati ya safu za milima ya Mbeya na milima ya Uporoto. Mlima mkubwa unaoonekana kutoka mjini ni Mlima wa Mbeya (Mbeya Peak) wenye urefu wa m 2818. Eneo la mji ni kati ya m 1600 kitovuni na m 1900 au zaidi juu ya UB kwenye mitelemko ya mlima Loleza.

Hali ya hewa haina joto kali kutokana na kimo. Wakati wa Juni-Julai halijoto wakati wa usiku inaweza kushuka chini hadi 0 °C mlimani hata chini zaidi. Mvua zinaanza mwezi wa Novemba hivyo ni wakati wa kupanda. Kwa kawaida mvua zinasimama tena Januari - Februari na kunyesha kwa wingi Machi - Aprili.

Uti wa mgongo wa mji ni barabara kuu ya TANZAM inayounganisha sehemu za nje kati ya Uyole na Mbalizi. Kitovu kipya cha mji kinahamishwa kwenda kata ya Foresti iliyoko kando ya barabara kuu.

Station Road huko Mbeya sehemu ya kale ya mjini

Historia[hariri | hariri chanzo]

Jina la Mbeya limetokana na neno la kisafwa "Ibheya" ambayo maana yake ni chumvi kwani miaka mingi wafanyabiashara walikuwa wanafika mahali hapo kubadilishana mazao yao kwa chumvi. Mlima mkubwa ulio karibu ulijulikana kwa jina la "Mbeya"[1] wakati wa ukoloni wa Kijerumani, na mji ulipokea baadaye jina kutokana na mlima huu.

Mji wa kisasa wa Mbeya ulianzishwa na wakoloni Waingereza mnamo mwaka 1927. Wakati ule dhahabu ilianza kupatikana katika mlimani karibu na Mbeya hadi Chunya.

Historia inavyoonekana katika jiografia ya Mbeya[hariri | hariri chanzo]

Mji ulianzishwa katika sehemu zinazoitwa bado Uhindini, Uzunguni na Majengo. Mji ulipangwa kufuatana na kawaida ya miji wa kikoloni ya Afrika ya Mashariki kuwa na sehemu tatu:

  • Uzunguni ni sehemu ya nyumba za Wazungu na karibu na ofisi za serikali (District Officer, polisi, mahakama)
  • Uhindini ni mtaa wa biashara uliokuwa hasa mkononi mwa wafanyabiashara wenye asili ya Uhindi na
  • Majengo kama sehemu kwa wafanyakazi Waafrika na familia zao.

Makanisa ya kale kama ishara ya historia[hariri | hariri chanzo]

Mahali pa makanisa ya kale panaonyesha ugawaji huu wa kihistoria:

  • Kanisa Anglikana iliyokuwa dhehebu rasmi la Uingereza lipo chini ya Uzunguni na karibu na ofisi za kiserikali (zinazoelekea siku hizi kuhamishwa kwenda Foresti) kama Mkuu wa Mkoa na mahakama. Knisa hili ni jengo dogo kwa sababu lilipangwa kwa kundi dogo la maafisa na wafanyabiashara pamoja na wakulima Waingereza wa Mbeya.
  • Kanisa la Moravian la mjini ambalo ni dhehebu la Kikristo asilia la Mbeya liko Majengo iliyokuwa sehemu kwa Waafrika. Kati ya Waingereza hawakuwepo Wamoravian.
  • Kanisa Kuu Katoliki lilihudumia Wazungu wachache hasa Waeire kati ya wakoloni pamoja na Wahindi kutoka Goa na pia Waafrika kwa hiyo iko kati ya Uzunguni na Uhindini karibu na Majengo.

Mji uliendelea kupanuka pande zote. Barabara kuu ya TANZAM inaunganisha sehemu za nje kati ya Uyole na Mbalizi.

Siku hizi sehemu kubwa ya wakazi ni wakristo, hasa wafuasi wa Kanisa la Katoliki, Kanisa la Moravian na Kanisa la Kiluteri. Makundi makubwa mjini ni Wasafwa wenyeji na Wanyakyusa waliohamia hapa kutoka Rungwe. Wanyakyusa ndio waliotangulia kuleta Uluteri mjini.

Kuna pia msikiti kubwa na hekalu la Wahindu.

Mawasiliano[hariri | hariri chanzo]

Kituo cha reli ya TAZARA Mbeya
Treni ya TAZARA kwenye kituo Mbeya

Mbeya ni njiapanda ya njia mbalimbali muhimu: Barabara kuu ya lami kutoka Daressalaam (850 km) hugawanya hapa kwenda MalawiMsumbiji kupitia Tukuyu/Rungwe, na kwenda ZambiaAfrika Kusini kupitia Tunduma/Mbozi. Vilevile njia ya reli ya TAZARA hupita Mbeya kuelekea Zambia. Kuna ghala kubwa kwa ajili ya mizigo ya Malawi inayofikishwa kwa reli kutoka Daresalaam bandarini ikihamishwa kwa malori kwenda Malawi hapa Mbeya.

Mbeya imekuwa na uwanja wa ndege mdogo usiokuwa na huduma ya kawaida kwa muda mrefu. Lakini kuna mipango ya kujenga uwanja mpya huko Songwe zipatao km 40 kufuata njia ya kwenda Zambia.

Wakazi[hariri | hariri chanzo]

Mbeya ni kati ya miji kumi mikubwa ya Tanzania. Idadi ya wakazi imekadiriwa kuwa wapatao 280.000 katika mw. 2005. Wengine mnamo 300.000 wanaishi katika mazingira karibu na Mbeya mjini.

Kiasili Mbeya ilikuwa eneo la Wasafwa. Siku hizi sehemu kubwa ya wakazi wanaweza kuwa mchanganyiko wa Wasafwa pamoja na makabila ya Wanyakyusa kutoka wilaya za Rungwe na Kyela, Wanyiha kutoka Mbozi, Wandali kutoka Ileje na Wakinga kutoka Makete.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Uchumi wa Mbeya mjini umetegemea kilimo cha mazingira yake na biashara. Viwanda mbalimbali vilianzishwa lakini havikufaulu sana. Kuna viwanda kwa mfano Zana za Kilimo, Highland Soap, Mbeya Textiles. Mbeya Ceramics iliporomoka kitambo.

Tangu miaka ya 1990 kitovu cha mji kinahamishwa kutoka eneo la zamani kwenda karibu na barabara kuu ya Daresalaam – Zambia.

Elimu[hariri | hariri chanzo]

Pamoja na shule za sekondari kuna taasisi kadhaa za elimu ya juu kama vile:

  • Chuo Kikuu Teofilo Kisanji ambacho ni chuo kikuu changa cha Kanisa la Moravian Tanzania kinachotoa kozi za ualimu na theolojia tangu mwaka 2005. Kilitanguliwa na chuo cha Motheco.
  • Mbeya Technical College
  • Chuo cha Kilimo Uyole (Agricultural Research Institute -ARI- Uyole) ambacho ni taasisi ya uchunguzi wa kisayansi pamoja na chuo.


Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Wajerumani waliandika "Mbeja" wakitamka "j" kama "y", linganisha Kamusi ya Koloni za Kijerumani, makala "Usafua"

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Flag of Tanzania.svg Kata za Wilaya ya Mbeya Mjini - Tanzania Flag of Tanzania.svg

Foresti • Ghana • Iduda • Iganjo • Iganzo • Igawilo • Ilemi • Ilomba • Isanga • Isyesye • Itagano • Itende • Itezi • Itiji • Iwambi • Iyela • Iyunga • Iziwa • Kalobe • Maanga • Mabatini • Maendeleo • Majengo • Mbalizi Road • Mwakibete • Mwansekwa • Mwansanga • Nonde • Nsalaga • Nsoho • Nzovwe • Ruanda (Mbeya) • Sinde • Sisimba • Tembela • Uyole