Lori

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Lori ya kubeba kontena ikiwa na mkono wa winchi ya kupakiza mzigo wake
Lori lenye ukubwa wa katikati yenye sehemu ya mizigo iliyofungwa
Daimler-Lastwagen, 1896

Lori (kutoka Kiingereza lorry) ni motokaa kubwa ya kubeba mizigo ya kila aina. Kutokana na ukubwa wake lori mara nyingi husukumwa na injini ya diseli.

Muundo wa lori[hariri | hariri chanzo]

Kuna aina mbalimbali. Kwa kawaida huwa na fremu imara, magurudumu yanayosukumwa na injini kupitia giaboksi. Mbele kuna chumba cha dereva chenye kiti chake na vifaa vya kutawala lori kama vile usukani, kichapuzi na breki. kwa kawaida kuna pia viti kwa ajili ya abiria au wasaidizi 1 - 2. Malori makubwa huwa pia na kitanda cha dereva nyuma ya viti.

Nyuma ya chumba cha dereva kuna sehemu ya mizigo na umbo lake linategemea aina ya mizigo. Malori ya kubeba kontena au vipande vikubwa huwa na sehemu bapa tu; kama ni ya kubeba vipande vingi vidogo au masi kama mchanga na mawe kuna nususanduku inayoweza kupandishwa kusudi la kutelezesha yaliyomo yake. Kama ni bidhaa zisizotakiwa kupigwa na jua au mvua kuna sehemu ya mzigo inayofungwa ama kwa kitambaa au sehemu yote ya mizogo ni kama sanduku au chumba cha chuma chenye milango nyuma.

Malori ya pekee yako kwa ajili ya kazi maalumu. Kama kazi ni kubeba vyakula vinavyohitaji kutunzwa baridi au hata katika hali ya mgando sehemu ya mizigo ni kama friji yenye mashine ya kupoza halihewa kushuka chini.

Malori makubwa huwa mara nyingi na sehemu mbili ambayo ni mbele lori lenye chumba, injini na giaboksi pekee halafu nafasi ya kufunga sehemu pa pili ambayo ni trela kubwa ya mizigo juu yake.

Ukubwa[hariri | hariri chanzo]

Malori madogo sikubwa kuliko motokaa kubwa. Katika nchi nyingi laiseni ya udereva ya kawaida inamruhusu mwenye laiseni kuendesha malori madogo hadi uzito wa tani 3.5.

Malori ya katikati hufikia uzito chini ya tani 10. Juu ya tani 10 ni malori mazito na hapa dereva anahitaji mafunzo maalumu.

Malori ya kubeba mizigo mingi kwa mahali pa mbali mara nyingi huwa pia na trela. Malori huwa na magurudumu manne au zaidi kama ni mazito.

Muundo wa lori kubwa ya sehemu mbili yenye magurudumu 18 huwa na sehemu zifuatazo:
1. Lori ya mbele
2. trela kubwa ya pekee (inaweza kutengwa)
3. Sehemu ya injini
4. Chumba
5. Sehemu ya kitanda cha dereva (malori makubwa pekee)
6. paa ya juu
7. tangi ya fueli
8. Sahani ya kiunganishi cha trela
9. nafasi ya mzigo
10. mguu wa trela wa kuisimamisha wakati wa kutengwa na lori