Nenda kwa yaliyomo

Breki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Breka ya sahani ya motokaa; sahani ni sehemu ya habi ya gurudumu na tairi inafungwa hapa. Sehemu nyekundu ina viatu vya breki ndani yake vinavyoshika sahani kama dereva anakanyaga pedali
Breki ya baisikeli yenye uwezo mdogo; kiatu cha breki husukumwa kwa nguvu ya wenzo wa mkono kutoka juu moja kwa moja kwenye tairi; breki aina hii inaweza kulegea haraka na hasa wakati wa mvua kiatu kinaweza kuteleza juu ya tairi

Breki ni kifaa kinachopunguza kasi ya injini au kuisimamisha. Neno latumiwa hasa kwa breki kwenye vyombo vya usafiri vyenye magurudumu kama treni, baisikeli, pikipiki au motokaa.

Breki mara nyingi hukaza gurudumu na kuchelewesha mwendo wake lakini kuna aina nyingine pia. Kazi hii inatekelezwa kwa kukaza sehemu iliyounganishwa na gurudumu kwa kiatu cha breki. Msuguano kati ya sehemu ya gurudumu na kiatu cha breki hubadilisha nguvu ya mwendo kuwa joto.

Breki za sahani na chungu[hariri | hariri chanzo]

Kwenye magari kuna hasa aina mbili za breki ni zile za sahani na zile za chungu. Chungu sawa na sahani inaunganishwa imara na sehemu ya gurudumu.

Ndani ya chungu kuna viatu vya breki vinavyosukumwa dhidi ya ukuta wa chungu na kusababisha msuguano unaochelewesha mwendo wa chungu na gurudumu.

Vivyo hivyo kwenye breki ya sahani viatu vya breki viko pande zote mbili nje ya sahani iliyounganishwa na gurudumu vikisukumwa dhidi ya sahani.

Kila aina ina faida na hasara yake. Siku hizi breki za sahani zatumiwa zaidi hasa kwenye magurudumu ya mbele. Aina hii inapitisha joto na kupoa haraka zaidi. Lakini breki za chungu ni afadhali kwa kushika gari ikisimama kwenye mtelemko. Kwa hiyo siku hizi mara nyingi magari huwa na breki za sahani mbele na chungu nyuma. Malori makubwa hutumia zaidi breki za chungu kwa sababu haitaji nguvu nyingi kama sahani na hii ni muhimu kwa magari mazito.

Muundo wa breki[hariri | hariri chanzo]

Breki inahitaji muundo ambako tendo la dereva anayetaka kusimama inafikishwa kwenye viatu vya breki yaani mahali pa kushika gurudumu. Dereva anakanyaga pedali na nguvu ya mguu wake unafikishwa kwa njia mbili:

  • kwenye magari ya zamani pedali ilivuta waya iliyovuta wenzo la viatu vya breki. Breki za aina hii hazitumiwi tena siku hizi isipokuwa kwa ajili ya breki ya mkono inayotumiwa wakati gari linasimama.
  • magari mengi huwa na breki haidroli. Hapa pedali inasukuma silinda inayopitisha shindikizo kwa nguzo ya mafuta ndani ya bomba ya breki. Mwishowe shindikizo inasukuma silinda ya gurudumu inayokaza viatu vya breki. Katika aina hii ya breki mara nyingi pampu inaongeza nguvu ya breki.
  • Magari makubwa kama mabasi na malori mazito huwa na breki ya upepo ambako shindikizo inapitishwa kwa njia ya hewa ndani ya bomba.