Kontena

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Wafanyakazi wanafunga kontena pamoja kwenye meli
Kontena kwenye bandari ya New Jersey
Kona za kontena

Kontena (kwa Kiing. container) ni sanduku kubwa la metali -hasa feleji- ambayo vipimo vyake vimesanifishwa kwa matumizi ya kimataifa. Kontena hutumiwa kutunza na kusafirisha bidhaa za kila aina kwa meli, lori au reli. Kontena ndogo husafirishwa pia kwa ndege.

Kontena zimepunguza sana kiwango cha kazi na gharama kinachohitajika kusafirisha mizigo. Zilianza kutokea mnamo 1956 huko Marekani kwa matumizi ya mizigo ya kijeshi zikaenea pia upande wa meli za kiraia.

Tofauti zilizotokea katika matumizi ya kontena[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya kupatikana kwa kontena meli kubwa ilijazwa mizigo yake kwa msaada wa wafanyakazi mamia waliobeba bidhaa gunia kwa gunia ndani ya meli na kuzipakiza katika chumba cha mizigo. Bidhaa ziliwekwa katika magunia au katika masanduku yaliyotengenezwa kwa ubao kwa kila aina ya shehena. Zilijazwa katika malori au mabehewa ya mizigo ya reli, kupelekwa bandarini na hapo kuondolewa katika lori au kwenye behewa na wafanyakazi waliojaza nyavu iliyovutwa na winchi kubwa hadi kwenye meli. Hapa nyavu ulifunguliwa na wafanyakazi walichukua yale magunia au masanduku na kuzipanga katika nafasi za kubeba mizigo. Wakati meli ilifika bandari nyingine kazi ilirudia: wafanyakazi wengi walihitajika kubeba bidhaa kutoka vyumba vya meli, kuzipanga katika nyavu zilibebwa kwa winchi hadi nje ya meli, halafu hapa kusambazwa na wafanyakazi juu ya malori au mabehewa ya usafiri; mara nyingi kwanza hadi ghala ya bandarini na baadaye baada ya kuzipakia tena kwenye usafiri wa nchi kavu hadi mahali palipotakiwa.

Kontena ilibadilisha mtindo huu. Sasa bidhaa zinaingizwa katika kontena kiwandani au kwenye ghala. Kontena inahamihswa juu ya lori au behewa ya treni inayoisafirisha hadi bandarini. Hapa kuna winchi kubwa inayochukua kontena yote na kuiwekea juu ya meli. Kwenye bandari ya kufika kontena yote inapelekwa bandarini, moja kwa moja juu ya lori. Sasa ni watu wachache tu wanaoshughulika mzigo huu, na kazi inaendelea haraka zaidi pia kwa gharama dogo kuliko zamani.

Usafinishaji[hariri | hariri chanzo]

Ilikuwa lazima kufikia mapatano juu ya ukubwa wa kontena na kuzisanifisha. Hii inawezesha ujenzi wa malori, mabehewa ya reli na meli zilizo tayari kubeba kontena bila kupotezs nafasi bure.

Kontena ya kimsingi ni kontena ya futi 20. Hii inamaanisha ya kwamba urefu wake ni futi 20 (~mita 6.058), upana futi 8 (mita 2.438) na kimo cha futi 8.5 (mita 2.591). Aina hii huitwa TEU (=(Twenty-foot Equivalent Unit) ni kama kipimo cha kutaja kiasi cha mizigo meli inaweza kubeba au kiasi kinachopokelwa katika mabandari

Kila kona ya kontena huwa na vyuma imara na nafasi ya kuzifungana pamoja ambayo ni muhimu kama meli inakuta mawimbi makubwa. Kontena ziko imara kiasi ya kwamba inawezekana kuzipanga moja juu ya nyingine hadi kimo cha kontena 7 zilizojaa.

Kuna pia kontena zenye urefu mara mbili yaani futi 40 pia kontena zilizo juu zaidi. Kwa matumizi kwenye ndege kuna vipimo sanifu vidogo zaidi.

Matumizi kwa usafiri mbalimbali[hariri | hariri chanzo]

Kontena inaruhusu kubeba mizigo kutoka mahali hadi mahali kwa kutumia usafiri mbalimbali bila kufungua mzigo tena. Kwa hiyo inawezekana kuchukua mzigo ndani ya kontena kiwandani kwa lori, kuihamisha kwa treni hadi bandarini, kuihamisha kwenye meli na kuisafirisha tena kwa lori na reli kwenye nchi inalyolengwa.

Siku hizi kuna malori mengi pia mabehewa ya reli ambayo yamejengwa kikamilifu kupokea kontena.

Nyumba iliyojengwa kwa kutumia kontena zilizoongezwa madirisha na milango

Matumizi mengine ya kontena[hariri | hariri chanzo]

Kuna pia kontena zilizoandaliwa kwa matumizi ya makazi ya watu kwa hiyo inawezekana kuunganisha makontena ya aina hii kupata jengo la kukaa watu au ya ofisi haraka sana.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu: