Mwezi (wakati)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mwezi ni mojawapo wa vipindi kumi na mbili vya mwaka. Muda wa mwezi unategemea aina ya kalenda inayotumika.

Mwezi kama kipimo cha wakati[hariri | hariri chanzo]

Awamu za mwezi kuanzia mwezi mwandamo kupitia hilali, robo ya kwanza, nusu mwezi, robo ya tatu, mwezi mpevu hadi mwezi mwandamo tena.

Uso wa mwezi jinsi unavyoonekana duniani hubadilikabadilika. Mwezi mpevu unaonekana kama duara kamili la kung'aa lakini baada ya kuonekana hivi umbo lapungua kila siku hadi kutoonekana kabisa na hali hii huitwa mwezi mwandamo. Baadaye mwezi unaonekana tena kama hilali nyembamba na kuongezeka hadi kuwa duara tena. Muda wa mabadiliko yote kupita mara 1 ni siku 29 1/4.

Muda wa mabadiliko kati ya mwezi mwandamo hadi kupotea na kuwa mwezi mwandamo tena ni kati ya siku 28 - 29. Kipindi hiki kinakumbukwa kirahisi, kinatazamiwa na watu wote wakati uleule kwa hiyo pamoja na kipindi cha siku kilikuwa kati ya vipimo vya kwanza vya wakati kwa binadamu.

Inawezekana kwamba juma la siku saba lilianza kwa kuzingatia robo 4 za mwezi wa siku 28.

Awamu za mwezi zilikuwa vipindi vya kuhesabu wakati tangu mwanzo wa kalenda. Hadi leo kuna kalenda ya mwezi ndiyo kalenda ya Kiislamu inayopanga wakati kutokana na hali halisi ya awamu za mwezi.

Kalenda ya mwezi[hariri | hariri chanzo]

Katika kalenda ya mwezi ni sawa na kipindi kutoka awamu ya mwezi mpya angani hadi mwezi mpya unaofuata ni 29.53 siku. Mwezi mpya unaanza sawa na kuonekana kwa mwezi mpya jinsi ilivyo katika kalenda ya Kiislamu.

Kalenda ya jua[hariri | hariri chanzo]

Kwa kalenda ya jua muda wa mwezi unakaribia tu muda kati ya awamu za mwezi. Katika kalenda ya Gregori miezi ina kati ya siku 28 hadi 31. Lakini vipindi hivi havina uhusiano tena na hali halisi ya awamu za mwezi wa angani mwenyewe. "Mwezi" ni lugha tu haimaanishi gimba la angani tena.

Majina ya miezi[hariri | hariri chanzo]

Kwa Kiswahili nchini Tanzania miezi inatofautishwa kwa namba; mwezi wa kwanza, wa pili, wa tatu ... hadi mwezi wa kumi na mbili.

Pamoja na njia hiyo, kuna majina ya Kilatini iliyofika kwenye Kiswahili kupitia lugha za wakoloni, yaani Kijerumani na Kiingereza. Ndiyo yanayotumika zaidi nchini Kenya.

Majina ya miezi yenye asili ya Kilatini[hariri | hariri chanzo]

(majina ya Kilatini katika mabano)

 1. Januari (Ianuarius), siku 31
 2. Februari (Februarius), siku 28*
 3. Machi (Martius), siku 31
 4. Aprili (Aprilis), siku 30
 5. Mei (Maius), siku 31
 6. Juni (Iunius), siku 30
 7. Julai (Iulius), siku 31,
 8. Agosti (Augustus), siku 31
 9. Septemba (September), siku 30
 10. Oktoba (October), siku 31
 11. Novemba (November), siku 30
 12. Desemba (December), siku 31
 • Februari huongezeka siku moja kufikia 29 katika miaka mirefu kufuatana na utaratibu wa kalenda ya Gregori.

Majina ya Kiarabu ya miezi (Kalenda ya Kiislamu)[hariri | hariri chanzo]

 1. Muharram محرّم
 2. Safar صفر
 3. Rabi`-ul-Awwal (Rabi' I) ربيع الأول
 4. Rabi`-ul-Akhir (Rabi' II) ربيع الآخر أو ربيع الثاني
 5. Jumaada-ul-Awwal (Jumaada I) جمادى الأول
 6. Jumaada-ul-Akhir (Jumaada II) (Jumaada II) جمادى الآخر أو جمادى الثاني
 7. Rajab رجب
 8. Shaaaban شعبان
 9. Ramadan رمضان
 10. Shawwal شوّال
 11. Dhul Qaadah ذو القعدة
 12. Dhul Hijjah ذو الحجة

Miezi hii haina wakati maalumu katika kalenda ya jua yenye miezi Januari - Desemba, bali inabadilika kila mwaka.