Kalenda ya mwezi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kalenda ya Mwezi ni kalenda inayohesabu miezi kufuatana na mwendo wa Mwezi kwenye anga. Mwezi una muda wa siku 29,5 kutoka mwezi mpya hadi mwezi mpya. Faida yake ni ya kwamba mwezi unaonekana na watu wote. Hali hii inasaidia kuelewana haraka kati ya watu juu ya tarehe fulani katika mazingira ambako hakuna mitambo wala maandishi. Mwaka wa miezi hii 12 una siku 354.

Kwa sababu hiyo kalenda za kale katika mataifa na tamaduni mbalimbali mara nyingi zilikuwa hasa kalenda za kufuata mwezi.

Kalenda ya mwezi ina mwaka wa siku 354 ambao ni fupi kuliko mwaka wa jua mwenye siku 365 1/4. Kutokana na hiyo kalenda haiwezi kutabiri majira yanayoenda sambamba na mwendo wa jua. Hii ilileta ugumu katika makadirio ya mambo yote yanayohusu mpangilio ya kilimo kinachofuata majira ya joto na baridi au ukame na mvua. Hali hizi zote zinategemea hali ya jua na kukadiriwa katika mwaka wa jua. Ugumu huu uligusa pia mambo ya utawala na serikali kwa sababu uwezo wa wakulima kulipa kodi inategemea mavuno. Kalenda ambayo haisaidii kupanga wakati wa mavuno hivyo kupatikana kwa mapato ya serikali ina faida kidogo tu.

Kutokana na sababu hizo kalenda za mwezi zilirekebihswa mara nyingi kwa njia ya kuingiza siku za nyongeza ili muda wa mwaka ilingane na mwaka wa jua.

Kalenda ya Kiyahudi ni mfano hadi leo jinsi mwaka wa mwezi unasahihishwa kwa kuingiza miezi ya nyongeza. Katika utaratibu wa kipindi cha miaka 19 kuna miaka 12 ya kawaida na miaka saba yenye mwezi wa nyongeza inayobadilishana ili kulinganisha kalenda ya mwezi na mwendo wa jua hivyo mwezi wa mavuno inabaki katika majira yake.

Kalenda ya mwezi tupu ambayo ni muhimu hadi leo ni kalenda ya kiislamu. Tarehe zake zinabadilika kila mwaka katika kalenda ya Gregori ambayo ni Kalenda ya kimataifa inayofuata jua. Kwa mfano Ramadhani iko mwaka 2006 BK wakati wa Novemba; kila mwaka inasogea mbele itafika miezi ya Agosti, Mei, Januari na kadhalika hadi kurudi tena Novemba katika mwendo wa miaka wapitao 33.

Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kalenda ya mwezi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.