Nenda kwa yaliyomo

Hilali

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mwezi mpya)
Picha ya mwezi unaoonekana kwa darubini kwa umbo la hilali.
Hilali angani.
Hilali barabarani.

Hilali (kutoka Kiarabu هلال hilāl) ni neno la kutaja mwezi mpya au mwezi mchanga yaani mwezi jinsi unavyopatikana angani ukianza kuonekana tena baada ya hali ya kutoonekana inayotokea kila baada ya takriban siku 29. Hilali ina umbo la pinde nyembamba.

Jina hili linaangaliwa sana katika mazingira ya pwani ya Afrika ya Mashariki na pia kati ya wafuasi wa dini ya Uislamu maana katika kalenda ya Kiislamu kuonekana kwa hilali ni muhimu kwa hesabu ya mwezi mpya pamoja na sikukuu za dini hiyo. Kwa mfano, kufunga kwa mwezi wa Ramadhani kunaanza siku ambako hilali inaonekana baada ya mwezi wa nane Shaaban katika kalenda ya Kiislamu.

Historia ya ishara

[hariri | hariri chanzo]

Ishara ya hilali inajulikana kutoka tamaduni mbalimbali za kale ambako ilichorwa kama alama ya mwezi wenyewe, ya mwezi wa kalenda au pia kama ishara ya kidini kwa ajili ya mungu wa mwezi aliyeabudiwa katika tamaduni nyingi za kale.

Katika Uajemi ya Kale na Roma ya Kale alama ya hilali ilikuwa pia sehemu ya nembo la kifalme. Kwa njia hiYO iliingia pia katika sanaa ya Waislamu baada ya ushindi wao juu ya Waajemi na Waroma. Hivyo inaonekana pia katika Kuba ya Mwamba ambalo ni jengo la Kiislamu la kale zaidi lililosimama hadi leo. [1]

Katika utamaduni Wa Waislamu hilali ilianza kutumiwa tangu karne ya 18 BK kama sehemu ya bendera, nembo za kifalme na pia kama mapambo juu ya majengo. Tangu karne ya 19 ilikuwa nembo rasmi ya jeshi la Milki ya Kiosmani (Uturuki) na kutoka huko kuenea kama ishara ya Uislamu wenyewe.

Leo hii picha ya hilali inapatikana kama ishara kwenye bendera za nchi mbalimbali zenye Waislamu wengi.

Orodha ya bendera za kuonyesha Hilali

[hariri | hariri chanzo]
Nchi huru zinazotambuliwa kimataifa
Majimbo au madola ndani ya nchi huru zinazotambuliwa kimataifa
Nchi zinazojitegemea zisizotambuliwa kimataifa
Bendera za nchi za kihistoria
Bendera na nembo nyingine
  1. Makala HILAL ii. — IN ISLAMIC ART, uk. 381, katika Brill_-_The_Encyclopaedia_of_Islam_Vol_3, Leiden-London 1986; hapa inatazamiwa kama ishara ya ushindi juu ya Waajemi, si kama ishara ya Kiislamu bado