Uajemi ya Kale

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Uajemi ya Kale ni kipindi katika historia ya Uajemi kilichotokea kabla ya kuingia cha Uislamu nchini na hasa kipindi cha milki kubwa.

Nasaba mbalimbali za watawala ziliunda madola makubwa yaliyounganisha nyanda za juu za Uajemi pamoja na nchi za jirani. Athira ya Uajemi ilikuwa kubwa nyakati zile ikiwa nchi muhimu zaidi katika Asia ya Magharibi kwa karne nyingi.

Chanzo cha historia[hariri | hariri chanzo]

Kuna dalili za kuwepo kwa watu katika eneo la Uajemi kuanzia zama za mawe. Akiolojia iligundundua vifaa vya Homo neanderthalensis na baadaye ya Homo sapiens.

Kijiji cha kwanza ambako watu walilima kilithibitishwa kuwa cha zamani za mnamo 7200 KK.

Dola la kwanza linalojulikana katika eneo la Uajemi ilikuwa milki ya Elam katika tambarare ya Khuzestan jirani na Mesopotamia. Wakazi walitumia lugha ya karibu na Kisumeri kwenye mto Frati.

Mnamo mwaka 3000 KK tawi moja la wahamiaji Waarya liliingia kutoka kaskazini na kukalia nyanda za juu za nchi; tawi lingine likaingia Uhindi. Neno "Arya" ni asili ya jina "Iran" jinsi watu wa Uajemi wanaita nchi yao.

Wamedi[hariri | hariri chanzo]

Kati ya makabila hayo walikuweko Wamedi walioanzisha milki ya Umedi na kutawala theluthi ya magharibi ya Uajemi ya leo. Walipaswa kukubali ubwana wa milki ya Ashuru katika Mesopotamia. Mnamo mwaka 700 KK makabila ya Wamedi yaliunganishwa mara ya kwanza katika shirikisho wakafaulu kujiweka huru kutoka utawala wa Ashuru wakajenga mji mkuu wao huko Ekbatana.

Chini ya mfalme Cyaxares Wamedi waliunga mkono mfalme Nabopolassar wa Babeli wakashambulia pamoja milki ya Ashuru na kuiharibu.

Waakhameni[hariri | hariri chanzo]

Kati ya makabila yaliyokuwa chini ya Wamedi walikuweko Waajemi waliojiita wenyewe Waparsi. Mnamo mwaka 700 KK kiongozi wa moja kati ya koo za Waajemi alikuwa mfalme wao lakini bado chini ya ubwana wa Umedi.

Mwaka 553 KK mfalme wa 5 katika nasaba ya Akhameni Koreshi II aliasi dhidi ya babu yake Astyages mfalme wa Umedi akafaulu kumpindua. Hapo Koreshi alijiita "mfalme wa Wamedi na Waajemi" akaendelea kufanya vita dhidi ya majirani wake akatwaa milki za Lydia, Babeli, Baktria na Sogdia na hivyo kuunda milki kubwa iliyowahi kujulikana duniani hadi wakati ule.

Mwanawe Koreshi, Kambisi II alivamia Misri mwaka 525 KK na kuongeza nchi hii katika milki ya Waakhameni.

Mfalme aliyefuata, Dario I alizidi kupanua eneo hadi kujumlisha Asia Magharibi yote, milima ya Kaukazi, Asia ya Kati pamoja na Afghanistan, sehemu kubwa za Pakistani ya leo, Afrika ya Kaskazini pamoja na Misri, Libia, pwani ya Sudani, Eritrea, sehemu za Balkani. Aliingia pia Ugiriki kwa shabaha ya kuadhibu Athens iliyowahi kusaidia miji ya Wagiriki katika Asia Ndogo iliyoasi dhidi ya milki ya Uajemi. Lakini kwenye mapigano ya Marathon mwaka 490 KK Waajemi wakashindwa wakarudi Asia.

Mfalme aliyefuata, Xerxes I alirudi Ugiriki miaka 10 baadaye kwa jeshi kubwa na jahazi za kijeshi. Alijenga daraja la jahazi juu ya mlangobahari wa Bosporus akashinda Wagiriki kwenye mapigano ya Thermopili tarehe 11 Agosti 480 KK ambako askari 300 kutoka Sparta chini ya mfalme Leonidas walifaulu kuwazuia Waajemi kwa siku kadhaa hadi sehemu kubwa ya Wagiriki wakaweza kujiokoa. Waajemi waliendelea hadi Athens iliyoachwa na wakazi wote lakini kwenye mapigano ya baharini ya Salamis jeshi lote la bahari la Kiajemi lilizamishwa na Wagiriki. Mwaka ulikofuata, 479 KK, Wagiriki walifaulu kushinda jeshi la Waajemi kwenye mapigano ya Plataia. Katika miaka iliyofuata Wagiriki walifaulu kuwalazimisha Waajemi kuondoka katika pwani ya Ionia yenye miji mingi ya Kigiriki.

Chini ya wafalme wa Kiakhameni waliofuata milki kubwa ilipaswa kushindana na majiribio ya sehemu mbalimbali za milki yao zilizojaribu kuasi na kupata uhuru. Bonde la mto Indus liliondoka katika milki.

Mfalme Xerxes III alifaulu kurudisha Misri katika milki mwaka 343 KK na kukandamiza uasi wote.

Dario III alikuwa mfalme wa mwisho wa nasaba hii (336 KK - 330 KK). Mnamo 334 KK Aleksanda Mkuu mfalme wa Makedonia ya Kale alishambulia milki ya Uajemi. Katika mapigano ya Issos (333 KK) alishinda jeshi la mfalme Dario mara ya kwanza akaendelea kwa kuvamia Misri na kuiteka mwaka 332 KK. Mwaka 331 KK alielekea tena Mesopotamia alipokutana na Dario na jeshi lake kwenye mapigano ya Gaugamela na kumshinda tarehe 1 Oktoba 331 KK. Akaendelea na kuingia Babeli bila mapigano alipojitangaza kuwa "mfalme wa Asia". Katika Januari 330 KK alifika kwenye mji mkuu Persepolis akaendelea kumfuata Dario hadi Baktria. Huko mfalme wa Uajemi aliuawa na gavana wake; Aleksanda alimwua gavana huyo akarudi na maiti ya mfalme Persepolis alipomzika kwa heshima yote na kujitangaza mtawala mpya wa Uajemi. Huo ulikuwa mwisho wa nasaba ya Waakhameni.

Nasaba ya Seleukos[hariri | hariri chanzo]

Waparthi 250 KK - 226[hariri | hariri chanzo]

Wasasani 226 - 651[hariri | hariri chanzo]

Angalia makala: Milki ya Wasasani

Wasasani walikuwa nasaba ya mwisho ya Uajemi kabla ya uvamizi wa Waarabu katika karne ya 7 BK.

Walipindua Waparthi waliowatazama kama wageni kutoka kaskazini wakalenga kurudisha ukubwa wa Uajemi wa Kale chini ya Waakhemi. Walifufua Uzoroasta kama dini rasmi ya milki yao, na kwa vipindi kadhaa walitesa Wakristo walioanza kuenea katika milki yao. Walipigana vita vingi dhidi ya Dola la Roma na baada ya mgawanyiko wa dola hilo, dhidi ya Ufalme wa Bizanti. Wakati huohuo walipaswa kupigana na mashambulio ya makabila kutoka Asia ya Kati.

Vita hizi nyingi zilichosha nguvu ya milki, na baada ya vita ya miaka 30 dhidi Roma, Wasasani walikosa nguvu kujitetea dhidi ya uvamizi wa Waislamu kutoka jangwa la Uarabuni.

Walijenga utamaduni mkubwa ulioshawishi pia majirani yake na hata Waarabu waliovamia na kutawala maeneo yao kama sehemu ya ukhalifa wao.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Uajemi ya Kale kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.