Babeli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Babuloni)
Sehemu ya geti la Ishtar huko Babeli.
Mnara wa Babeli ulichorwa mara nyingi na wasanii kama katika picha hii ya Pieter Brueghel Mzee.

Babeli ulikuwa mji wa kale katika Mesopotamia, muhimu kwa karne nyingi kama mji mkuu wa milki zilizotawala maeneo makubwa ya Mashariki ya Kati.

Inatajwa mara nyingi katika Biblia, hasa kwa jina la Babuloni.

Maghofu yake hupatikana karibu na mji wa kisasa wa Al Hillah (Irak) kando ya mto Frati km 90 kusini kwa Baghdad.

Historia

Orodha ya wafalme wake ilianza mnamo mwaka 2300 KK. Mfalme mashuhuri wa kwanza alikuwa Hammurabi.

Babeli ulikuwa mji mkuu wa milki mbili kubwa kabla na baada ya kipindi cha enzi ya Ashuru.

Kati ya miaka 1770 KK na 1670 KK na mara ya pili kati ya miaka 612 KK na 320 KK inaaminika ulikuwa mji mkubwa zaidi duniani.

Wakati wa Milki ya pili ya Babeli mfalme Nebukadreza II alitawala nchi zote kati ya Palestina (Kanaani au Israeli) hadi Ghuba ya Uajemi.

Bustani ya malkia Semiramis ilikuwa moja ya maajabu saba ya dunia.

Piramidi au zigurat kubwa za mji zilikuwa maarufu na mfano wao ni mnara wa Babeli unaotajwa katika kitabu cha Mwanzo 11:1-9 (katika Tanakh, yaani Biblia ya Kiebrania, na katika Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo).

Wakati ule jeshi la Babeli liliteka mji wa Yerusalemu mwaka 587 KK, lilibomoa hekalu la Suleimani na kuwapeleka Wayahudi hadi Mesopotamia kwa uhamisho wa Babeli.

Inaaminika ya kwamba sehemu kubwa za Biblia ya Kiebrania ziliandikwa uhamishoni kule Babeli.

Mwaka 539 KK Waajemi walivamia Dola la Babeli na kuliteka. Babeli uliendelea kuwa mji muhimu katika Dola la Uajemi.

Baada ya ushindi wa Aleksanda Mkuu juu ya mfalme Mwajemi Darius III, Babeli ulikuwa chini ya utawala wa Wagiriki. Aleksanda alikufa Babeli mwaka 323 KK katika jumba la kifalme la Nebukadreza.

Mwaka 275 KK Wagiriki walijenga mji mkuu mpya wakawalazimisha wakazi wa Babeli kuhamia huko Seleukia. Huo ulikuwa mwisho wa mji ule mkubwa.

Mataifa ya kale walikumbuka mji wa Babeli kwa muda mrefu.

Barua ya kwanza ya Petro na kitabu cha Ufunuo wa Yohane katika Agano Jipya (kilichoandikwa mnamo mwaka 90 BK) vinatumia jina la Babeli kama jina la fumbo kuashiria Roma.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Babeli kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.