Ufunuo wa Yohane

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Yesu akimtokea Yohane.
Mchoro mdogo wa karne ya 9 uliopo katika ukurasa wa kwanza wa Kitabu cha Ufunuo, Biblia ya Basilika la Mt. Paulo, Roma, Italia.

Kitabu cha Ufunuo ni cha mwisho katika orodha ya vitabu 27 vinavyounda Agano Jipya katika Biblia ya Kikristo.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Mwandishi[hariri | hariri chanzo]

Kundi la mwisho la vitabu vya Agano Jipya linajulikana kwa jina la Yohane, kwa kuwa Injili ya nne, barua tatu na kitabu cha Ufunuo viliandikwa na mtume huyo na wanafunzi wake.

Agano Jipya

Akiwa kijana kuliko mitume wenzake, Yohane alijaliwa kuishi miaka mingi na kuandika hadi miaka 70 hivi baada ya Yesu kwenda mbinguni.

Miaka hiyo yote alizidi kutafakari na kuhubiri maneno na matendo ya Bwana akitambua mafumbo mengi yaliyofichika ndani yake. Pengine alirekebisharekebisha maandiko yake mpaka mwishoni, halafu akawaachia wanafunzi wake kuyakamilisha na kuyaeneza kati ya Wakristo wa mkoa wa Efeso ambapo aliongoza Kanisa miaka mingi.

Hatua muhimu ni ile iliyofuata kufungwa kwake katika kisiwa cha Patmo (leo nchini Ugiriki). Akiwa huko, Yesu Kristo alimtokea Yohane na kumpa ufunuo maalumu siku ya Bwana, yaani Jumapili (Ufu 1:9-11)

Ufunuo ni kitabu pekee cha kinabii katika Agano Jipya; kilikamilika mwaka 95 hivi B.K.; lengo lake ni kuwaimarisha katika tumaini Wakristo waliozidi kudhulumiwa na serikali ya Dola la Roma.

Mtindo wa uandishi[hariri | hariri chanzo]

Kitabu hiki kimejaa mafumbo kama kawaida ya mtindo wa kiapokaliptiko.

Mtindo huo ni mgumu kueleweka kwa sababu mwandishi hakuweza kutamka wazi watesi watakaoangamizwa na Mungu ni akina nani.

Tena alipenda kusisitiza anatoboa siri za Mungu alizojaliwa kuzijua kwa njia za ajabu (njozi, malaika n.k.).

Tunahitaji kutafsiri mifano mingi (vitu, viungo, rangi n.k.) na tarakimu (nne, saba, kumi na mbili, elfu n.k.).

Kwa ajili hiyo ni muhimu kujua maana zake katika Biblia (Ufunuo umejaa madondoo ya Agano la Kale: mistari 274 kwa 404!).

Mpangilio[hariri | hariri chanzo]

Mpangilio wake kwanza una barua saba kwa makanisa ya mkoa wa Efeso, halafu sura 4-22 zina unabii kuhusu mambo yajayo, yaani vita vikali zaidi na zaidi kati ya Yesu Kristo na shetani ambaye anatumia dini na serikali za Kipagani.

Ushindi utakuwa wa Kristo na Kanisa, ambao hatimaye wanachorwa kama bwanaarusi na bibiarusi katika utukufu wa Mungu. (Ufu 1;4-5; 12; 21-22).

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:

Tafsiri ya Kiswahili[hariri | hariri chanzo]

  • [1] Agano Jipya kwa lugha ya Kiswahili

Vya lugha nyingine[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya Agano Jipya bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ufunuo wa Yohane kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.