Upagani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Upagani ni jina la kutaja imani za kidini amabazo ama zinaabudu miungu mingi au ni dini za jadi.

Neno hili linatumiwa hasa na watu katika mapokeo ya kikristo kutaja imani nyingine lakini siku hizi, hasa katika nchi kadhaa za Ulaya, kuna pia vikundi vya watu ambao wanajiita hivi wenyewe.

Asili ya jina[hariri | hariri chanzo]

Asili ya neno ni lugha ya kilatini ambako "pagus" ni eneo la mashambani, mbali na miji mikubwa, na "paganus" ni mtu anayeishi huko vijijini au mashambani.

Chaguo la neno hili kwa ajili ya dini kinatunza historia ya kwamba huko mwanzoni katika zamani za Roma ya Kale Ukristo ulikuwa dini ya watu wa miji lakini imani za kale za Waroma ziliendelea kwa muda mrefu vijijini.

Istilahi[hariri | hariri chanzo]

Hata kama neno "mpagani, upagani" linatoka katika mapokeo ya kikristo si lugha ya Biblia.

Maandiko ya Biblia ya Kiebrania kwa kawaida yanatumia neno "goi / goyyim" (גוי / גוים ) kwa kutaja watu wasio Wayahudi. Goi inamaanisha "taifa" na mara chache inaweza kutumiwa pia kwa taifa ya Israeli.[1]. Lakini uwingi wake "goyyim" (mataifa) inamaanisha watu wasio Wayahudi ambao pia wana imani tofauti.

Katika Agano Jipya lugha hii imetafsiriwa kwa Kigiriki na pale tunaposoma "mataifa" [2] kwa Kiswahili lugha asilia Kigiriki inatumia "ethni ἔθνη"

Wapagani wapya[hariri | hariri chanzo]

Tangu karne ya 19 kumekuwa na watu katika Ulaya waliotafuta njia mbadala za kidini nje ya Ukristo; wengine wao walijaribu kufufusha imani za jadi za Ulaya na hapa wengine wametumia jina la "upagani" kwa imani hizi. Hao ambao wamekadiriwa kuwa makumi elfu katika nchi mbalimbali za Ulaya wanaitwa "neo pagans" au wapagani wapya.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. kwa kawaida Biblia ya Kiebrania inatumia neno "am" kwa ajili ya Wayahudi wenyewe; "Am" ni kama "taifa" lakini zaidi kwa maana ya ukoo ilhali "goy" ni taifa zaidi kwa maana ya kieneo na kisiasa.
  2. kama vile Luka 21, 24: Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa