Nenda kwa yaliyomo

Biblia ya Kiebrania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nakala ya Biblia ya Kiebrania ya karne ya 11 pamoja na maelezo ya Targum kando

Biblia ya Kiebrania ni namna mojawapo ya kutaja vitabu vitakatifu vya Uyahudi vinavyoitwa na Wayahudi wenyewe "Tanakh". Ndivyo vinavyounda pia sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo na kuitwa na Wakristo "Agano la Kale" (vikiwa pamoja na Deuterokanoni au vikiwa peke yake).

Vitabu hivyo, vilivyoandikwa kwa Kiebrania na sehemu ndogo kwa Kiaramu, vinaheshimiwa pia na Wakristo wakiamini ya kwamba ufunuo wa vitabu hivyo ulikuwa hatua ya kwanza iliyokamilishwa baadaye na hatua ya pili au "Agano Jipya" kwa ujio wa Yesu Kristo.

Kuna madhehebu na wataalamu wanaopendelea kuviita vitabu hivyo kwa jina la Biblia ya Kiebrania ili wasisitize usawa wa vitabu vilivyofunuliwa au wasionekane wanavikosea heshima vitabu ambavyo kwa Wayahudi si jambo la "kale".

Hivyo kichwa cha Kilatini "Biblia Hebraica" limekuwa jina la kawaida kwa matoleo ya kitaalamu ya maandiko haya.

Hata hivyo majina "Agano la Kale" na "Agano Jipya" yanapatikana katika Biblia yenyewe (taz. hasa Eb 8).

Tofauti kati ya Biblia ya Kiebrania na Agano la Kale

Wakristo wengi huwa na vitabu vingine 7 katika matoleo ya Agano la Kale nje ya idadi ya vitabu vya Kiebrania.

Sababu ni kwamba Wakristo wa kwanza walizoea tafsiri ya Kigiriki ya Biblia ya Kiebrania iliyokuwa kawaida kati ya Wayahudi wakati wa Yesu, ambao wengi wao walikuwa wakiishi nje ya Israeli.

Tafsiri hiyo inayojulikana kama Septuaginta imejumlisha maandiko kadhaa ambayo kuanzia miaka 85-100 BK Wayahudi waliamua kuyakataa katika ibada zao.

Lakini Wakristo waliotegemea lugha ya Kigiriki kama lugha ya mawasiliano ya kimataifa waliendelea kutumia vitabu vya Septuaginta kwa jumla.

Hata katika hilo kuna tofauti ndogo kati ya Kanisa Katoliki ambalo limekubali vitabu saba zisizo sehemu ya orodha ya Kiebrania na Makanisa ya Kiorthodoksi ambayo pengine yamevikataa, pengine yamevikubali, pengine yanatumia vitabu vingine vichache vya nyongeza kama vile kitabu cha 3 na cha 4 cha Wamakabayo.

Tofauti hizi zilitokana na nakala mbalimbali zilizopatikana kwa sababu zamani vitabu havikuchapishwa bali vilinakiliwa kwa mkono pekee.

Ila tu vitabu vyote vya Biblia ya Kiebrania hukubaliwa na Wakristo wa kila aina.

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Biblia ya Kiebrania kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.