Waorthodoksi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Makanisa ya Kiorthodoksi)
Rukia: urambazaji, tafuta
Maeneo ya Waorthodoksi katika Ulaya na Mashariki ya Kati

Waorthodoksi ni Wakristo wanaofuata mapokeo ya Mitume wa Yesu jinsi yalivyostawi kihistoria katika Ukristo wa Mashariki upande wa mashariki wa Dola la Roma iliyoitwa pia Bizanti na nje ya mipaka yake. Leo hii ni nchi za Ulaya ya Mashariki pamoja na nchi za Mashariki ya Kati ulipoenea baadaye dini ya Uislamu.

Jina hilo lina asili ya Kigiriki likitokana na maneno όρθος ("orthos", yaani "nyofu", "sahihi") na δόξα ("doksa", yaani "rai", "fundisho") yaani "wenye fundisho sahihi".

Jina hilo lilitungwa ili kutofautisha Wakristo waliofuata mafundisho rasmi ya imani yaliyotolewa na Mitaguso ya kiekumene dhidi ya mikondo mingine ya wakati ule.

Kwa namna ya pekee jina hilo lilitumika upande wa mashariki, hivi kwamba lilipotokea farakano la mwaka 1054, likabaki kama jina maalumu la makanisa yenye ushirika na Patriarki wa Konstantinopoli (leo Istanbul katika Uturuki).

Makanisa ya kujitegemea ya Kiorthodoksi ni kama yafuatayo:

 • Patriarki wa Konstantinopoli
 • Patriarki wa Aleksandria
 • Patriarki wa Antiokia
 • Patriarki wa Yerusalemu
 • Patriarki wa Moskwa na Urusi
 • Patriarki wa Peć na Serbia
 • Patriarki wa Romania
 • Patriarki wa Bulgaria
 • Patriarki wa Georgia
 • Kanisa la Kiorthodoksi la Kipro
 • Kanisa la Kiorthodoksi la Ugiriki
 • Kanisa la Kiorthodoksi la Poland
 • Kanisa la Kiorthodoksi la Albania
 • Kanisa la Kiorthodoksi la Uceki na Slovakia


Hivi karibuni hata makanisa mengine ya mashariki yamechagua kujiita hivyo, ingawa yanaendelea kutofautiana kuhusu maazimio kadhaa ya mitaguso mikuu iliyokubaliwa na Wakristo walio wengi. Leo hii wanatofautisha kwa kutumia majina

 • "Waorthodoksi" kwa makanisa yaliyotokana na kanisa rasmi la Bizanti (Roma Mashariki) (ing.: Eastern Orthodox)
 • "Waorthodoksi wa Mashariki" kwa makanisa yaliyojitenga na kanisa hili la Bizanti (ing. Oriental Orthodox)

Hata hivyo pande mbili zinafanana katika liturgia na staili za ibada zao pia katika sheria kuhusu maaskofu (wasiooa), makasisi (wanaoweza kuoa) na umonaki.