Nenda kwa yaliyomo

Mfalme

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Wafalme)
Aina za serikali duniani
aina za Jamhuri: buluu, kijani, njano na machungwa;
Ufalme:
nyekundu Ufalme wa kikatiba ambapo mfalme ana madaraka madogo tu ya kisiasa
zambarau:Ufalme wa kikatiba ambapo mfalme ana madaraka makubwa
dhambarau nyeusi: mfalme ana madaraka yote asibanwe na katiba
Mengine: Utawala wa chama kimoja au kamati ya kijeshi

Mfalme ni mtawala wa kiume juu ya nchi katika utaratibu wa ufalme. Kwa kawaida amerithi cheo chake kutoka kwa mzazi wake aliyekuwa mfalme pia. Lakini kuna pia wafalme waliochaguliwa au kuteuliwa kwa namna nyingine, hasa kama mfalme aliyetangulia alikufa bila kuacha mrithi.

Utawala wa kifalme ulikuwa wa kawaida katika nchi nyingi za dunia kwa muda mrefu.

Mwanamke anayeshika nafasi ya mfalme huitwa "malkia".

Kama cheo kinaendelea katika ukoo mmoja kutoka mababa kwa watoto wao familia hiyo huitwa nasaba.

Madaraka ya mfalme

Madaraka ya wafalme yalitofautiana kati ya nchi na nchi na kati ya kipindi na kipindi cha historia. Mifano ni:

  • Mfalme wa kikatiba imekuwa hali ya kawaida katika karne ya 19 na 20 pale ambapo utaratibu wa kifalme umeendelea. Mfalme hatekelezi tena shughuli za serikali. Serikali inachaguliwa na bunge kwa msingi wa kura za raia wote jinsi ilivyopangwa katika katiba ya nchi. Nafasi ya mfalme inafanana na ile ya rais katika jamhuri. Kuna tofauti kama mfalme ana athira katika siasa au kama cheo chake ni cha heshima tu na hana uwezo wa kuingilia kati kazi za bunge na serikali. Mifano yake ni wafalme wa Skandinavia au pia utaratibu wa Uingereza na nchi nyingine za Jumuiya ya Madola zisizo jamhuri. Nafasi ya mfalme iko hasa kama vikundi ndani ya bunge havikubaliani kuhusu serikali mpya na hakuna upande wenye kura nyingi kabisa. Lakini wafalme wa nchi kama Moroko na Yordani wana athira kubwa zaidi.
  • Mfalme mwenye mamlaka yote bila kufungwa na katiba alikuwa wa kawaida zamani lakini leo hii wamebaki wachache sana. Falme za aina ni Saudia, Omani, Qatar, Eswatini na Brunei.
  • Mfalme wa sehemu ya taifa tu: mifano yake ni Kabaka wa Buganda huko Uganda au Asantehene wa Ashanti katika Ghana. Wafalme hao wa jadi bado wanaheshimiwa na kuwa na athira kwa sababu wanatambuliwa na watu wao hata ndani ya jamhuri kubwa zaidi kuliko eneo la kabila au kundi lao.

Wafalme na watawala wengine

Katika Kiswahili hakuna utaratibu sanifu mtawala gani anastahili kuitwa "mfalme". Kwa kawaida anasimamia eneo au nchi ya kujitegemea lakini wengine huweka pia masharti kuhusu ukubwa wa eneo lake.

Kwa maeneo fulani kuna vipindi katika historia ambapo si rahisi kutofautisha kati ya wafalme na watawala wadogo wengine kama watemi, machifu n.k.. Mara nyingi watawala wa Waswahili ambao hawakuwa na mamlaka nje ya eneo dogo la mji wao walijiita Sultani na Wareno waliwaita "reyes" (wafalme). Hali hii ililingana na mifano mingine kama kati ya Wagiriki wa Kale ambapo vilevile watawala wadogo juu ya miji walitumia cheo cha "mfalme".

Tazama pia