Ufalme
Ufalme ni mfumo wa utawala ambapo mfalme, malkia au mtu mwingine aliyerithi cheo chake ni mkuu wa dola. Vyeo vingine vya mkuu katika ufalme ni pamoja na kaisari, shah, tenno, sultani, amiri au mtemi. Kwa kawaida mfalme amerithi cheo chake kutoka kwa baba yake au mama yake, kwa hiyo alizaliwa kama mfalme mteule na ataendelea kuwa na cheo hicho hadi kifo chake. Lakini kama mfalme aliyetangulia hakuwa na mrithi inawezekana ya kwamba mfalme mpya amechaguliwa. Mfano wa dola lenye mfumo wa ufalme ambapo mkuu anachaguliwa mara kwa mara ni Vatikani ambapo Papa ni mkuu wa dola.
Neno ufalme hutumiwa pia kwa kutaja nchi inayotawaliwa na mfalme au malkia, kwa mfano Ufalme wa Maungano, Ufalme wa Eswatini na kadhalika.
Kiwango cha madaraka cha mfalme huwa na tofauti kubwa. Leo hii wafalme wengi wako chini ya katiba ya nchi na mara nyingi wana madaraka machache; nafasi yao ni ya heshima na desturi. Lakini kuna falme kadhaa ambaPo mfalme bado ana madaraka makubwa, habanwi na katiba wala bunge wala serikali kama vile Omani au Saudia.
Tofauti ya ufalme na jamhuri
[hariri | hariri chanzo]Kinyume cha ufalme ni jamhuri inayoongozwa na mkuu, mara nyingi kwa cheo cha rais au katika nchi kadhaa na kamati ya watu wanaochaguliwa na kwa kawaida kwa kipindi fulani. Mara nyingi rais wa nchi huchaguliwa kwa kipindi cha miaka 4-6 na katika nchi nyingi kuna uwezekano Wa kwamba anarudi tena kwa kipindi kingine. Kuna jamhuri ambapo vongozi wanalenga kuhakikisha ya kwamba mtoto wao anaendelea na cheo cha mkuu wakiacha kutawala, lakini hii kwa kawaida si utaratibu wa kisheria katika jamhuri; mfano wa kisasa ni Korea Kaskazini ambayo ni jamhuri inayotawaliwa na familia Kim katika kizazi cha pili ilhali mtoto wa kiongozi Kim Jong Il anateuliwa kumfuata baba.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Sababu za kuanzishwa kwa ufalme
[hariri | hariri chanzo]Ufalme ni muundo wa kale sana lakini haukuwa mfumo wa kwanza wa serikali. Wataalamu huona ya kwamba chanzo chake ni azimio la kabila au kundi dogo la watu kumruhusu mtoto wa kiongozi mwenye nguvu na uwezo kuendelea na shughuli za baba. Kuna mifano watu walioishi na viongozi wa muda tu waliamua kuwa na mfalme wakati wa vita wakiona uongozi wenye nguvu ni wa lazima. Kulitokea pia ya kwamba kiongozi aliyeteuliwa kwa kipindi cha matatizo au vita alionekana kuwa na uwezo akaendelea hadi kifo na kumpatia mtoto wake nafasi ya mrithi wakati alipokuwa bado na nguvu.
Historia ya Biblia kama mfano wa kuanzishwa kwa ufalme
[hariri | hariri chanzo]Biblia inasimulia jinsi gani watu wa Israeli ya Kale walioongozwa kila mahali na wazee lakini kama walipata matatizo makubwa viongozi walijitokeza walioitwa "Waamuzi" na kuwa na majukumu ya kijeshi pamoja na ya kisheria. Kitabu cha Waamuzi 8#22 kinaonyesha pia jinsi gani suala la ufalme lilivyokuwa na ugumu; mwamuzi Gideon alipoombwa na watu kuwa mfalme alikataa na kudokeza ya kwamba Mungu pekee anastahili kuwa na cheo hicho. Baadaye Sauli alijitokeza kama kiongozi dhidi ya tishio la Waamoni; alipowashinda vitani watu walimfanya Sauli mfalme wao wa kwanza. Mataifa mengi walipata ufalme kwa njia zilizofanana na Israeli ya Kale yaani wakati wa vita ambapo wengi walikubali haja ya kiongozi mwenye nguvu.
Kupinduliwa kwa wafalme au kubanwa kwa madaraka yao
[hariri | hariri chanzo]Mfano mashuhuri wa kinyume ni historia ya Athens au Roma ya Kale ambazo zilitawaliwa zamani na wafalme lakini viongozi wa miji hiyo walifukuza wafalme baada ya kuona tabia za kidikteta pamoja na kupuuzia haki za watu wakaanzisha jamhuri zilizoteuliwa na viongozi waliochaguliwa kwa muda tu. Lakini Roma ya Kale ilirudia mfumo wa ufalme tangu Kaisari Augusto ingawa kwa jina iliendelea kama jamhuri hadi mwisho.
Mara nyingi wafalme waliunganisha nafasi za mkuu wa serikali na kiongozi wa jeshi na jaji mkuu. Mataifa mbalimbali walimjua mfalme pia katika nafasi ya kidini kama kuhani mkuu au kama mkuu anayeshika nafasi ya Mungu duniani.
Mamlaka kubwa ya wafalme ilisababisha mara nyingi jitihada za kubana madaraka yao. Mfano mashuhuri ni Uingereza ambapo wafalme walipaswa kushauriana na bunge ya wakubwa na wawakilishi wa miji kabla ya kukusanya kodi kwa ajili ya vita au kwa shughuli maalumu. Jambo kama hilo halikutokea katika Uingereza pekee lakini katika nchi hiyo bunge lilikuwa taasisi ya kudumu isiyofutwa tena na hivyo kuwa chanzo cha muundo wa ufalme wa kikatiba ambako mamlaka ya mfalme iko chini ya sheria fulani.
Tangu uhuru wa Uholanzi, Marekani na baadaye mapinduzi ya Kifaransa nafasi ya ufalme ilianza kupungua katika Ulaya na kutoka hapo pia katika sehemu nyingine za dunia. Hasa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia falme muhimu kama Ujerumani, Austria-Hungaria, Urusi na Milki ya Osmani zilibadilisha mfumo wa utawala zikawa jamhuri.
Ukoloni na ufalme
[hariri | hariri chanzo]Ukoloni wa karne ya 19 ulisababisha kupotea kwa falme nyingi dunani. Mwanzoni wakoloni walitumia mara nyingi wafalme na watemi waliokuwepo kama mawakala wa utawala wao ndani ya koloni. Lakini kadiri walivyounganisha falme mbalimali za kale ndani ya maeneo mapya makubwa yaliyoendelea kuwa mataifa mapya walidhoofisha pia nafasi ya ufalme wa kieneo.
Nchi za Afrika zilipopata uhuru mara nyingi zilijitangaza kuwa jamhuri na kwa njia hiyo falme za kale za Afrika zilifutwa au kupoteza madaraka ya kiutawala na kubaki kwa jina tu kama taasisi za kiutamaduni.
Ufalme leo
[hariri | hariri chanzo]Kuna nchi 44 duniani zilizoendela na mfumo wa ufalme hadi karne ya 21. (Linganisha jedwali). Ufalme wa kale ni Japani ambapo kuna wafalme tangu zaidi ya miaka 2000. Pia Ufalme wa Muungano, ambao wafalme wanaendelea karibu mfululizo tangu miaka 1,000 hivi, naDenmark tangu miaka 1,200 hivi.
Nchi |
Aina ya ufalme |
Cheo |
Jina |
Maelezo | |
---|---|---|---|---|---|
Japan | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | Tenno | Naruhito | Tenno hana madaraka ya kisiasa. Tangu 1945 ni mwakilishi wa taifa pekee. Japani ni ufalme wa kale duniani tangu zaidi ya miaka 2500. Cheo cha tenno chamaanisha „mtawala wa kimbingu“ | |
Antigua na Barbuda[1] | Ufalme wa kikatiba - chini ya usimamizi wa bunge | malkia | Elizabeth II wa Uingereza | — | |
Australia[1] | — | ||||
Bahamas[1] | — | ||||
Bahrain | Ufalme wa kikatiba | Mfalme | Hamad ibn Isa Al Khalifa | Hadi 2002 Emirati, baadaye ufalme; tangu mageuzi ya kisiasa imekuwa ufalme wa kikatiba | |
Barbados[1] | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge- | Malkia | Elizabeth II wa Uingereza | — | |
Ubelgiji | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | Mfalme | Albert II | — | |
Belize[1] | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | malkia | Elizabeth II wa Uingereza | — | |
Bhutan | Ufalme wa kikatiba | Mfalme | Jigme Khesar Namgyel Wangchuck | Tangu 1907 hadi 18 Julai 2008 ufalme bila masharti, baadaye ufalme wa kikatiba | |
Denmark | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | malkia | Margrethe II | Mfalme / malkia wa Denmark ni pia mkuu wa nchi ya Greenland na ya Visiwa vya Faroe | |
Grenada[1] | Elizabeth II wa Uingereza | — | |||
Jamaika[1] | — | ||||
Jordan | Ufalme wa kikatiba | Mfalme | Abdullah II | nchi ilianzishwa 1921 na Ufalme wa Maungano | |
Kambodia | Norodom Sihamoni | hadi 1955 na tangu 1993 ufalme | |||
Kanada[1] | Ufalme wa kikatiba | malkia | Elizabeth II wa Uingereza | — | |
Eswatini | Ufalme bila masharti. Harakati ya kidemokrasia iko njiani | Mfalme | Mswati III | — | |
Ufalme wa Nchi za Chini (Uholanzi) | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | Malkia | Beatrix I | Ufalme unajumlisha Uholanzi katika Ulaya na Aruba, Curaçao na Sint Maarten katika Amerika ya Kati | |
Lesotho | Ufalme wa Kikatiba | Mfalme | Letsie III | Mfalme aliitwa hadi 1965 „Mtemi Mkuu“. Mfalme hana madaraka ya kiserikali wala hatungi sheria | |
Malaysia | Mizan Zainal Abidin | Ufalme wa uchaguzi - Malaysia ina majimbo 13 na kati ya hizo usultani 9; mfalme huchaguliwa kila baada ya miaka 5 masultani 9 kati yao kwa njia ya kubadilishana nafasi; cheo cha mfalme ni Yang di-Pertuan Agong „mtawala mkuu“ | |||
Moroko | Ufalme wa kikatiba | Mohammed VI | |||
New Zealand[1] | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | malkia | Elizabeth II wa Uingereza | — | |
Norwei | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | Mfalme | Harald V | Ufalme wa kujitegema tangu 1905 | |
Papua Guinea Mpya[1] | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | malkia | Elizabeth II wa Uingereza | — | |
Visiwa vya Solomon[1] | — | ||||
Uarabuni wa Saudia | Ufalme bila masharti | Mfalme | Salman | Ufalme wa Kiislamu uliounganishwa 1931 | |
Uswidi | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | Carl XVI Gustaf | — | ||
Hispania | Felipe V | Ufalme hadi 1931; tena tangu 1947 bila mfalme chini ya dikteta Franco na tangu 1975 chini ya mfalme | |||
St. Kitts na Nevis[1] | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | malkia | Elizabeth II wa Uingereza | — | |
St. Lucia[1] | — | ||||
Saint Vincent na Grenadini[1] | — | ||||
Uthai | Ufalme wa kikatiba | Mfalme | Bhumibol Adulyadej (Rama IX) | — | |
Tonga | George Tupou V | — | |||
Tuvalu[1] | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | malkia | Elizabeth II wa Uingereza | — | |
Ufalme wa Maungano | Malkia wa Uingereza ni pia mkuu wa nchi wa „maeneo chini ya taji la Uingereza“ ambayo ni Guernsey, Jersey, Isle of Man halafu kwa maeneo ya ng’ambo ya Ufalme wa Maungano kama vile: Anguilla, Bermuda, Visiwa vya Virgin vya Uingereza, Eneo la Uingereza katika Bahari Hindi, Visiwa vya Cayman, Visiwa vya Falkland, Gibraltar, Montserrat, Visiwa vya Pitcairn, Saint Helena, Visiwa vya South Georgia na South Sandwich na Visiwa vya Turks-na Caicos. | ||||
Utemi | |||||
Luxemburg | Ufalme wa Kikatiba – chini ya mamlaka ya bunge | Mtemi Mkubwa | Henri I | — | |
Andorra | Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge | Watawala wa pamoja | Askofu Joan Enric Vives i Sicília na Rais Emmanuel Macron | Andorra ina watawala wawili wenye madaraka na heshima ya pamoja ambayo ni askofu wa Urgel (Hispania) na Rais wa Ufaransa | |
Liechtenstein | Ufalme wa kikatiba | Mtemi | Hans Adam II | ||
Monaco | Albert II | — | |||
Usultani na Emirati | |||||
Brunei | Ufalme bila masharti | Sultani | Hassanal Bolkiah | — | |
Oman | Haitham bin Tariq Al Said | — | |||
Katar | Ufalme bila masharti | Emir | Tamim bin Hamad | — | |
Kuwait | Ufalme wa kikatiba | Sabah al-Ahmad al-Sabah | Hadi 1991 ufalme bila masharti, tangu 1996 ina bunge | ||
Falme za Kiarabu | Shirikisho-Ufalme wa kikatiba | Rais | Chalifa bin Zayid Al Nahyan | Ufalme wa uchaguzi: kuna emirati 7; kila emir anaweza kuchaguliwa kuwa rais wa shirikisho lakini hadi sasa amechaguliwa kila safari Emir wa Abu Dhabi ambayo ni sehemu kubwa na tajiri | |
Eneo la Vatikani | |||||
Vatikani | Ufalme bila masharti | Papa | Fransisko | Ufalme bila masharti wa mwisho katika Ulaya; Papa huchaguliwa na mkutano wa makardinali |