Mfalme Sauli
.
Mfalme Sauli (1079 KK hivi hadi 1010 KK) anajulikana na Biblia na Kurani kama mfalme wa kwanza wa Israeli (labda kuanzia 1049 KK hadi kifo chake, yaani kwa muda wa miaka 42).
Baba yake alikuwa Kish wa kabila la Benyamini.
Sauli (kwa Kiebrania שָׁאוּל, Šāʼûl, "aliyeombwa"; kwa Kigiriki Σαούλ, Saoul; kwa Kiarabu طالوت, Ṭālūt), alipakwa mafuta na Samweli awe mfalme, lakini akaja kukataliwa kwa kukosa utiifu kwa Mungu na kwa kutokubali kukosolewa na nabii wake.
Habari zake katika Vitabu vya Samweli
[hariri | hariri chanzo]Vitabu viwili vya Biblia ya Kikristo vinaitwa kwa jina la mtu huyo, ambaye kwa njia yake taifa la Israeli lilianza kuwa na umoja zaidi na hatimaye kuwa ufalme. Badala ya kila kabila kujitegemea, yote 12 yalikubaliana yawe na kiongozi mmoja wa kudumu ambaye cheo chake kirithiwe na mwanae. Kwa umoja huo waliweza kushinda maadui wao wengi.
Vitabu hivyo vimekusanya kumbukumbu zote kuhusu mwanzo wa ufalme (1070-970 hivi K.K.), yaani kuhusu Samweli mwenyewe na wanaume wawili aliowapaka mafuta watawale Israeli kwa niaba ya Mungu: kwanza Sauli, halafu Daudi. Kumbukumbu hizo zilizokusanywa zilikuwa nyingi na tofauti, hivyo tunakuta humo tata nyingi kuliko katika vitabu vingine vyote vya Biblia. Hasa mna hoja za kukubali mfumo wa ufalme na hoja za kuukataa.
Samweli aliwaamua Waisraeli kwa kuwakomboa mikononi mwa Wafilisti (1Sam 7), lakini ni muhimu hasa kwa kuwaanzishia ufalme kwa kuwaweka wakfu kwanza Sauli halafu Daudi. Kadiri ya 1Sam 8, yeye na Mungu hawakupendezwa na jinsi Waisraeli wengi walivyotaka kuiga mtindo wa mataifa yote: Samweli aliwaangalisha kuhusu matatizo na unyonyaji wa wafalme, naye Mungu aliona katika ombi hilo uasi ambao Waisraeli wanamkataa asiwatawale tena, lakini akamuagiza Samweli awakubalie.
Ukweli ni kwamba mfalme aliwekwa wakfu kwa Mungu kama mwakilishi wake akitakiwa kutimiza matakwa yake, hasa kwa kusikiliza anamuambia nini kwa kinywa cha manabii wake. Ndiyo sababu Samweli alizidi kumuelekeza Sauli, na hatimaye akamkataa kwa ukaidi wake. Mabishano kati ya Samweli na Sauli ni mwanzo wa mabishano yote kati ya manabii na wafalme ambao hawakutaka kumtii Mungu, na hatimaye wakadhulumu na kuua manabii wake.
Mamlaka ya neno la Mungu lililoletwa na nabii ilitakiwa kuwa juu ya mamlaka ya serikali na nguvu ya kijeshi alivyokuwa navyo mfalme. Lakini mara nyingi wafalme, kwa kujivunia cheo chao, walishindwa kumnyenyekea nabii wa Mungu, wakaona afadhali kufuata manabii wengine wengi waliosema uongo ama kwa kudanganywa na matarajio yao ama kwa kujipendekeza kwa mfalme na kwa taifa lote.
1Sam 9:11-10:16 inasimulia Sauli alivyoteuliwa kuwa mfalme wa kwanza. Akitawala karibu miaka ishirini, alifanya makosa na kulaumiwa na Samweli, hata akakataliwa kabisa na Mungu kwa kutomtii kikamilifu (1Sam 15). Ingawa akaendelea kutawala kwa muda fulani, polepole alijitokeza kijana Daudi ambaye akaja kuanzisha ukoo wa kifalme wa milele.
1Sam 16-17 inaanza kutuletea mkusanyo wa hadithi juu ya Daudi ambazo zinampatia sifa aliyostahili, ingawa nyingine zinagongana: k.mf. kama aliingia katika utumishi wa Sauli kutokana na uhodari wake katika muziki au katika vita. Uhodari huo wote ukaendelea kusifiwa ila Daudi aliutumia kwa utukufu wa Mungu: ndiye aliyeingiza ala mbalimbali katika ibada na kutunga zaburi kadhaa, na ndiye aliyeeneza utawala wa Israeli kuliko yeyote.
Kadiri alivyozidi kupendwa na Mungu na watu, Sauli alimchukia kwa kijicho na kutaka kumuua (1Sam 18:6-16). Daudi alipolazimika kukimbia na kuunda kikosi chake akapata nafasi rahisi ya kumuua Sauli lakini alijizuia kwa kuheshimu krisma aliyopakwa awe mfalme (1Sam 24 na 26): hivyo ni mfano bora wa kujali wito wa Kimungu.
Hatimaye Sauli alijiua vitani kwenye mlima Gilboa, alipoona ameshindwa kama alivyotabiriwa kwa adhabu ya Mungu.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Wellhausen, Julius, Der Text der Bücher Samuelis
- Budde, Die Bücher Richter und Samuel, 1890, pp. 167–276
- Driver, S. R., Notes on the Hebrew Text of the Books of Samuel, 1890
- Cheyne, T. K., Aids to the Devout Study of Criticism, 1892, pp. 1–126
- Smith, H. P., Old Testament History, 1903, ch. vii.
- Cheyne, T. K., and Black, (eds.) Encyclopedia Biblica
- SAMUEL AND SAUL: A NEGATIVE SYMBIOSIS by Rabbi Moshe Reiss
- Hudson, J. Francis, 'Rabshakeh' [Lion Publishing 1992] is a fictionalisation of Saul's tragedy.
- Green, A., 'King Saul, The True History of the First Messiah' [Lutterworth Press 2007]
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mfalme Sauli kama habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |