Nenda kwa yaliyomo

Vitabu vya Samweli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ana akimtoa Samueli kwa Eli, mchoro wa Jan Victors, 1645.
Ernst Josephson, Daudi na Sauli, 1878.

Vitabu vya Samweli katika Biblia ya Kikristo ni viwili na vinaitwa kwa jina la Samweli, aliye wa mwisho (1050-1015 hivi K.K.) kati ya Waamuzi, tena nabii na mwanzilishi wa ufalme wa Israeli.

Mazingira ya vitabu hivyo[hariri | hariri chanzo]

Hapo mwanzo vitabu viwili vya Samweli vilikuwa kitabu kimoja, kikionyesha mfululizo wa historia ya Israeli kuanzia wakati wa Waamuzi mpaka karibu na mwisho wa utawala wa Mfalme Daudi.

Vitabu hivyo havimtaji mwandishi wake, ingawa kulikuwa na fununu kwamba baadhi ya habari zake ziliweza kutokana na ripoti zilizokuwa zimeandikwa na Samweli, Nathani, Gadi, Daudi na waandishi wa kitabu cha Yasheri (1 Sam 10:25; 2 Sam 1:18; 1 Nya 27:24; 29:29).

Habari za vitabu hivyo viwili zinachukua muda wa miaka themanini hadi mia moja.

Mafungu ya kwanza ya 1 Samweli yanaendelea kueleza habari za historia ya Israeli tangu wakati wa kitabu cha Waamuzi.

Wakati wa kuhani Eli, maisha ya Israeli upande wa siasa na wa dini yalifuata mfano wa wakati wa Waamuzi, watu walipomwasi Mungu na kuanguka chini ya utawala wa mataifa ya jirani (1 Sam 2:12, 32; 3:11-13; 4:10-11, 18; taz. Amu 2:13-15).

Lakini Samweli aliyekuwa mkuu katika Waamuzi wote, alipofaulu kuwahamasisha Waisraeli kuondoa miungu yao na kumrudia Bwana, Yeye kwa neema yake aliwaokoa watu wake kutoka kwa maadui zao waliokuwa wamewanyanyasa (1 Sam 7:3-6, 13, 15-17; taz. Amu 2:18; 3:9, 15).

Lakini Samweli hakuweza kuleta mabadiliko ya kudumu katika taifa, tena wanawe hawakufaa kumrithi, na watu walidai ianzishwe serikali ya kifalme, kama ilivyokuwa katika mataifa ya jirani yao (1 Sam 8:1-5). Baada ya kuimarishwa kwa ufalme sawasawa, uongozi siku zote ungekabidhiwa au kurithiwa kutoka kwa baba hadi mwanawe (1 Sam 8:19-22).

Basi, Sauli aliwekwa kuwa mfalme wa kwanza wa Israeli, lakini Samweli aliwaonya watu kwamba jambo hilo lisingeondoa matatizo ya taifa. Chini ya Waamuzi Waisraeli waliadhibiwa kwa ajili ya kuasi na kutokuamini kwao (1 Sam 12:9-11), na chini ya wafalme wangeadhibiwa kwa sababu hizohizo (1 Sam 12:13-15).

Wakati wa kwanza wa ufalme wa Israeli mambo mengi ya utawala yalifanana na ule wa Waamuzi, hasa kwa jinsi viongozi walivyopewa nguvu maalumu ya Roho wa Mungu, ili waweze kuwaokoa Waisraeli kutoka kwa watawala wa kigeni, na kutimiza kazi nyingine walizopewa (1 Sam 10:6; 11:6, 11; taz. Amu 3:10; 6:34; 11:29; 14:6, 19).

Sauli alipomwasi Mungu na kukataliwa, Roho wa Mungu alimtoka akaja juu ya Daudi (1 Sam 16:13-14). Kinyume cha Sauli, Daudi alijinyenyekeza mbele ya Mungu, naye alitamani kutimiza mapenzi yake (Zab 89:20; Mdo 13:22).

Kwa Daudi wakati mpya kabisa ulianza, na hatimaye Waisraeli waliimarika kitaifa na kufanikiwa, kama walivyokuwa wametamani kwa muda mrefu. Vitabu vya Samweli vinaeleza habari za utawala wa Daudi ambaye, katika nyakati zote zilizofuata, alihesabiwa kuwa mfalme bora wa Israeli, na mzazi mkuu wa Masiya aliyeahidiwa (2 Sam 7:12-16; Mt 22:42; Lk 1:32-33).

Samweli[hariri | hariri chanzo]

Ukuu wake ulidokezwa na uzazi wake wa ajabu, kwa kuwa mama yake alikuwa tasa akampata baada ya kusali na kuweka nadhiri (1Sam 1).

Hivyo baada ya miaka michache alihamia Shilo kwenye sanduku la agano kama mtumishi wa kuhani Eli.

1Sam 3 inasimulia wito wake: akiwa amelala karibu na sanduku hilo akaamshwa na Mungu mara tatu mpaka akafundishwa na Eli kumtambua na kumuitikia Mungu. Hapo akamtabiria Eli adhabu kali, na hivyo Israeli ikajua kuwa amefanywa nabii wa Bwana.

Samweli aliwaamua Waisraeli kwa kuwakomboa mikononi mwa Wafilisti (1Sam 7), lakini ni muhimu hasa kwa kuwaanzishia ufalme kwa kuwaweka wakfu kwanza Sauli halafu Daudi ambao maisha na mambo yao yanaelezwa katika kitabu chote.

Kwa kweli yeye na Mungu hawakupendezwa na jinsi Waisraeli wengi walivyotaka kuiga mtindo wa mataifa yote: Samweli aliwaangalisha kuhusu matatizo na unyonyaji wa wafalme, naye Mungu aliona katika ombi hilo uasi ambao Waisraeli wanamkataa asiwatawale tena, lakini akamuagiza Samweli awakubalie (1Sam 8).

Mfalme Sauli na mfalme Daudi[hariri | hariri chanzo]

1Sam 9:11-10:16 inasimulia Sauli alivyoteuliwa kuwa mfalme wa kwanza.

Akitawala karibu miaka ishirini (1030-1010 hivi K.K.), alifanya makosa na kulaumiwa na Samweli, hata akakataliwa kabisa na Mungu kwa kutomtii kikamilifu (1Sam 15).

Ingawa akaendelea kutawala kwa muda fulani, polepole alijitokeza kijana Daudi ambaye akaja kuanzisha ukoo wa kifalme wa milele.

1Sam 16-17 inaanza kutuletea mkusanyo wa hadithi juu ya Daudi ambazo zinampatia sifa aliyostahili, ingawa nyingine zinagongana: k.mf. kama aliingia katika utumishi wa Sauli kutokana na uhodari wake katika muziki au katika vita.

Uhodari huo wote ukaendelea kusifiwa ila Daudi aliutumia kwa utukufu wa Mungu: ndiye aliyeingiza ala mbalimbali katika ibada na kutunga zaburi kadhaa, na ndiye aliyeeneza utawala wa Israeli kuliko yeyote.

Kadiri alivyozidi kupendwa na Mungu na watu, Sauli alimchukia kwa kijicho na kutaka kumuua (1Sam 18:6-16).

Daudi alipolazimika kukimbia na kuunda kikosi chake akapata nafasi rahisi ya kumuua Sauli lakini alijizuia kwa kuheshimu krisma aliyopakwa awe mfalme (1Sam 24 na 26): hivyo ni mfano bora wa kujali wito wa Kimungu.

Baada ya kufanywa mfalme wa kabila lake (Yuda, yaani Kusini) na ya kupigana vita na mwana wa marehemu Sauli, Daudi akakubaliwa kuwa mfalme wa Israeli yote (yaani Kaskazini pia): pamoja na taarifa hiyo, 2Sam 5:1-12 inatuambia alivyoteka Yerusalemu uliokuwa bado mikononi mwa Wapagani akaifanya makao makuu ya kisiasa na ya kidini ya taifa lote la Mungu ili aunganishe Kaskazini na Kusini katika mji huo uliopo katikati.

Kuanzia hapo Yerusalemu ukawa mji mtakatifu wa dini tatu zinazomuabudu Mungu wa Abrahamu: Uyahudi, Ukristo na Uislamu.

2Sam 6 inasimulia sanduku la agano lilivyohamishiwa Yerusalemu kwa shangwe kubwa; hasa Daudi alicheza mbele ya Mungu kwa nguvu zake zote huku amevaa nguo ndogo ya kikuhani tu, bila ya kujijali kama mfalme.

Kwa unyenyekevu wake alimpendeza Mungu akapewa naye ahadi ya ajabu, yaani kwamba ufalme wake utadumu milele (2Sam 7). Utabiri huo wa nabii Nathani ukaja kuongoza tumaini la Waisraeli hasa walipodhulumiwa, k.mf. zamani za Yesu chini ya ukoloni wa Warumi, ambapo wote walimtazamia mwana wa Daudi mwenye kurudisha ufalme wa Israeli.

Pamoja na hayo, Daudi (aliyetawala miaka 1010-970 hivi K.K.) akabaki kielelezo cha mfalme wa Israeli, ambaye awe tofauti na wengine wote kwa kuwa hasa mtumishi mnyenyekevu wa Mungu.

Kisha kupewa ahadi hiyo alikwenda mbele ya Mungu na kusali vizuri kama kawaida yake hata nje ya ibada: sala yake ya sifa na shukrani imejaa mshangao kwa ukuu wa Mungu na fadhili zake na kumalizika kwa ombi nyenyekevu.

Ingawa hakukubaliwa kumjengea Mungu hekalu la ajabu alivyokusudia, amekuwa mwalimu wa sala kwa nyakati zote: hata leo liturujia inategemea sana zaburi zake.

Matendo mengine tofauti yaliyobadilisha sana maisha ya Daudi ni dhambi alizotenda kwa ajili ya mke wa Uria, yaani uzinifu, unafiki na uuaji wa askari huyo mwadilifu (2Sam 11).

Basi, Nathani akamuendea ili kumlaumu na kumtabiria adhabu mbalimbali, hasa kwamba upanga hautaondoka nyumbani mwake (2Sam 12:1-25).

Ikawa hivyo hasa kwa sababu ya Absalomu] mwanae ambaye alimuua kaka yake (2Sam 13:22-37) na baada ya kusamehewa akafanya njama hata akamfukuza Daudi toka Yerusalemu (2Sam 14:28-15:29) akazini na masuria wake mahali pa wazi (2Sam 16:20-23).

Hata hivyo Daudi akazidi kumpenda na alipoambiwa amekufa akamlilia kwa namna ambayo iliwashangaza na kuwachukiza waliompigania: yeye ambaye alijiombea na kupewa msamaha wa Mungu hakumchukia mwanae aliyehatarisha uhai wake (2Sam 18:19-20:8).

2Sam 24 pia inatuchorea sura yake ya kiroho: alipoadhibiwa na Mungu kwa tauni iliyoua Waisraeli wengi baada ya yeye kuhesabu askari wote alioweza kuwategemea vitani, basi kama mchungaji mwema aliomba adhabu imuangukie mwenyewe, lakini si kondoo zake wasio na kosa. Mfalme wa kumpendeza Mungu ni mchungaji wa watu wake; Yesu Kristo mwana wa Daudi anawajua kondoo zake mmojammoja kwa jina, naye amejitwisha adhabu ya makosa yao: ndiye mfalme na mchungaji bora (Yoh 10:11-18).

Habari za mwisho za Daudi zinapatikana katika 1Fal 1-2 tunaposikia juu ya njama ya mtoto mwingine: Adonia alitaka kutawala akajifanya mfalme huku Daudi mkongwe hana habari.

Lakini Nathani akaingilia kati ili mwandamizi wake awe Solomoni, ambaye alipozaliwa na mke wa Uria alimhakikishia Daudi msamaha wa Mungu.

Muhtasari wa 1 Samweli[hariri | hariri chanzo]

1:1-7:17 Israeli chini ya Eli na Samweli

8:1-12:25 Kuanzishwa kwa ufalme

13:1-15:35 Ushindi wa kwanza wa Sauli

16:1-19:24 Kuinuka kwa Daudi

20:1-31:13 Sauli amwudhi Daudi

Muhtasari wa 2 Samweli[hariri | hariri chanzo]

1:1-4:12 Vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kifo cha Sauli

5:1-10:19 Daudi aimarisha ufalme wake

11:1-20:26 Matatizo katika nyumba ya Daudi

21:1-24:25 Mambo mengine

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.