Nenda kwa yaliyomo

Kumbukumbu la Sheria

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mose akipokea Torati (juu) na kuwasomea Waisraeli (chini).
Mose akitazama toka mbali nchi ya ahadi, Kum 34:1-5 (mchoro wa Tissot).

Kumbukumbu la Sheria (pia: Kumbukumbu la Torati) ni kitabu cha tano katika Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na cha Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Majina[hariri | hariri chanzo]

Kwa asili kimeandikwa katika lugha ya Kiebrania, na katika lugha hiyo kinaitwa דְּבָרִים, Devarim, maana yake “Maneno”, ambalo ni nomino ya kwanza katika kitabu hicho.

Maelezo yaliyomo ni kama marudio ya sheria iliyotolewa katika Mlima Sinai, kwa hiyo kitabu kimeitwa Kumbukumbu la Torati. Jina hilo linatokana na maneno ya Kigiriki 'deuteros' (maana yake 'ya pili'), na 'nomos' (maana yake 'sheria') yaliyounganika na kuwa Δευτερονόμιον, Deuteronomion. Ndivyo kilivyoitwa na waliotafsiri Biblia ya Kiebrania mara ya kwanza katika lugha ya Kiyunani, miaka 200 hivi K.K. (tafsiri yao inaitwa Septuaginta).

Kwa kweli kitabu hiki kinapitia upya matukio ya wokovu ya wakati wa Musa kikifaidika na ujumbe wa manabii, hasa Hosea. Kwa msingi huo, kitabu hiki kinasisitiza sana uaminifu kwa sheria za Agano la Kale na pia tuzo na adhabu zitakazotolewa kufuatana na matendo ya Waisraeli, lakini pia upendo wa Mungu unaodai kurudishiwa.

Wengine wanakiita Kitabu cha Tano cha Mose (au Musa) kwa vile mapokeo yalimdhania kuwa mwandishi wa kitabu hicho. Siku hizi kitabu hicho kinafikiriwa kuwa kiliandikwa kama miaka 600 baada ya Musa, ingawa kina namna ya hotuba alizoweza kuwatolea Waisraeli kabla hajafa.

Vitabu hivyo vitano pamoja kwa jina la Kigiriki vinaitwa Pentateuko.

Yaliyomo[hariri | hariri chanzo]

Kitabu cha Kumbukumbu la Sheria kina sura thelathini na nne, ambazo karibu zote zinasimulia hotuba za Mose kwa Waisraeli. Mahali ni tambarare ya Moabu na wakati ni mwezi wa 11 katika mwaka wa mwisho wa matembezi ya Wanaisraeli.

  • Hotuba ya kwanza (sura 1 hadi 4) yarudia matokeo muhimu ya safari ya jangwani ya watu wa Israeli. Inaeleza jinsi ilivyo muhimu kumtii Mungu. Kuna maonyo dhidi ya uasi.
  • Hotuba ya pili (sura 5 hadi 26) ni sehemu kuu ya kitabu. Humo kuna marudio ya Amri Kumi, sheria kwa ajili ya maisha katika nchi ya ahadi na sura ya 20 ina sheria kuhusu vita.
  • Hotuba ya tatu (sura 27 hadi 30) inajadili yale yatakayofuata kama watu hupuuza maagizo ya Mungu au kuyatekeleza. Mwishoni ahadi kati ya Mungu na Wanaisraeli inarudiwa na Yoshua ateuliwa kuwa kiongozi mpya baada ya Musa.

Ni sura nne za mwisho tu zinazohusu mambo ya kihistoria: Yoshua kuteuliwa mwandamizi wa Mose kama kiongozi wa taifa (Kumb 31:1-8 inasimulia jinsi Musa alivyomuachia Yoshua uongozi wa Waisraeli wote kwa kumwekea mikono = Hes 27:12-23), Mose kuimba wimbo wake wa mwisho (sura 32), baraka ya Mose kwa makabila 12 ya Israeli (sura 33), na mwishoni habari za kifo chake Mose (sura 34).

Musa alifikia mpakani mwa nchi takatifu asikubaliwe kuiingia kama adhabu ya makosa yake, ila alionyeshwa yote kutoka mlimani (Kumb 32:48-52) halafu akafariki (Kumb 34). Kazi aliyopangiwa iliishia huko, mwingine akampokea na kuendeleza ukombozi wa Kimungu. Binadamu wote ni vyombo tu vinavyotumika kwa muda fulani, halafu vinaweza kuachwa. Kumbe Mungu ndiye mtendaji mwenyewe ambaye hasinzii wala halali, bali anazidi kuwashughulikia watu wake. Kwa imani hiyo mtu anatakiwa kuwa daima tayari kuwaachia wengine nafasi yake.

Katika maneno yake yote ya kukumbukwa ni hasa yale ya 6:4-9 ambayo Mwisraeli yeyote anayakariri kila siku katika sala na kuyashika pengine neno kwa neno.

Maneno mengine muhimu sana yapo 26:5-10: ni kama kanuni ya imani ambayo Mwisraeli alikuwa anaiungama mbele ya Mungu wakati wa kumtolea malimbuko ya ardhi. Hivyo alikuwa akikiri amepewa yote na Bwana, halafu akaweza kuyafurahia mavuno.

Mazingira[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kupokea sheria katika Mlima Sinai, Waisraeli walikuwa jangwani kwa muda wa karibu miaka 40, wakitangatanga kati ya Sinai na Kanaani.

Katika muda huo watu wote waliokuwa na umri wa miaka 20 na zaidi wakati wa kuondoka Mlima Sinai walikufa, na kizazi kipya kilikuwa kimepata umri wa kutosha.

Kwa hiyo Musa alirudia kueleza sheria kwa watu wa kizazi hicho, kabla hawajavuka Yordani na kuingia Kanaani.

Maelezo hayo yalitolewa katika majuma mawili ya mwisho wa maisha ya Musa, Waisraeli walipokaa katika nchi tambarare ya Moabu, wakifanya maandalizi ya mwisho ya kuingia Kanaani (Hes 22:1; 35:1; Kum 1:1-5).

Kurekebisha sheria na kuthibitisha agano[hariri | hariri chanzo]

Kitabu cha Kumbukumbu si marudio tu ya maagizo na amri zilizotolewa hapo awali, bali kina maelezo mengi ya ziada. Kinataja upya amri za sheria, lakini kinatia mkazo zaidi katika maneno mengine.

Sheria zilizoandikwa katika vitabu vya Kutoka, Walawi na Hesabu zilitoa amri kama madai ya moja kwa moja tu, lakini kitabu cha Kumbukumbu, kwa sababu hakikutaka kutoa mafundisho juu ya vitabu vile tu, kinaongeza kueleza kwamba uhusiano wa Waisraeli na Mungu wao lazima uwe zaidi kuliko sheria na madai ya haki tu. Uwe uhusiano wa kiroho wenye upendo na baraka.

Hali ya kitabu hiki ni ya mfano wa mhubiri kuliko wa mtoaji wa sheria, na wasomaji wake au wasikilizaji wake ni watu kwa jumla, kuliko makuhani na waamuzi tu (Kum 8:5-6; 10:12-13).

Kitabu kinasisitiza kwamba, watu watimize amri za Mungu ili kumjua na kumpenda Mungu wao zaidi, si kwa sababu tu wamedaiwa kuzitimiza katika maagano (Kum 6:3, 5-9; 7:7-8,11).

Agano ni msingi wa kitabu, lakini uhusiano baina ya Mungu na watu wake katika agano hilo ulitakiwa uwe wa upendo. Upendo mkuu wa Mungu kwa watu wake usababishe upendo wa kumtii Yeye (Kum 5:6-7; 6:1-3).

Kwa neema yake Mungu alichagua Israeli kuwa taifa lake akawaahidi kuwapa nchi ya Kanaani iwe nchi yao hasa (Kum 7:6-7; 8:1; 9:4-5).

Kama watu walitaka kufurahia baraka za agano hilo katika ushirika wa upendo na Mungu, walipaswa kujua sheria yake na kuitimiza. Kizazi kilichotangulia kiliapa kuwa na uaminifu katika agano kwa Mungu huko Sinai (Kut 24:7-8), lakini walikosa vibaya sana. Wakati huo kizazi kipya kilipokuwa tayari kuingia Kanaani, agano lilithibitishwa. Musa alirudia maneno yote ya sheria, na watu waliahidi upya kuitii (Kum 26:17-18).

Hati za agano hapo kale[hariri | hariri chanzo]

Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kina mambo mengi yanayofanana na hati za maagano jinsi yalivyofanyika katika nchi za maeneo yale hapo kale, ambapo bwana mkubwa au mfalme fulani alifanya mapatano na watu waliokuwa chini yake au waliomtegemea. Maagano kama hayo hayakutokana na majadiliano ya makundi mawili yaliyokuwa sawa, bali yalikuwa kadiri yaliyoandaliwa na yule mkuu, yakitangaza mamlaka yake juu ya watu na kupanga kanuni za maisha yaliyowapasa. Watu hawakuwa na njia yo yote ila kukubali masharti ya mkuu au ya mfalme wao.

Kwa kawaida hati ya agano ilianza kwa utangulizi wa historia ambapo mkuu alijieleza akiorodhesha mambo yote aliyowafanyia watu wake. Kisha ikafuata orodha ya masharti ya maagano yaliyowekwa juu ya watu. Kwanza, watu walionywa kuwa waaminifu na watiifu kwa mkuu wao, na baadaye walionywa wasianzishe fitina yo yote kwa kufanya mapatano na mfalme mwingine. Baada ya masharti yale ya msingi, amri na sheria zake zilielezwa kinaganaga zilizohusika na matakwa ya sehemu ile.

Kwa kawaida katika hati hizo mashahidi walitajwa. Pia zilieleza faida ambazo zitatokana na utiifu wa watu na adhabu ambazo zitatokana na uasi. Kisha hati ilifungiwa na kutunzwa kwa usalama katika patakatifu pa watu waliohusika, ili iweze kusomwa wakati wowote, na hapo iweze kupata nyongeza zake kama zikitakiwa.

Mara nyingine hati ilimalizika kwa kujumlishwa muhtasari wa maagizo na masharti maalumu, au kwa ahadi kwamba maagano hayo yaendelee kwa muda wote ambao watu wataendelea kuwa waaminifu na watiifu kwa masharti yake.

Kuhusu agano baina ya Mungu na Israeli alama nyingi za namna hiyo zinaonekana katika maandiko ya sheria zilizoandikwa katika vitabu vya Kutoka, Kumbukumbu la Torati na katika kitabu cha Yoshua. Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kimeandikwa kwa mtindo ulioelezwa hapo juu.

Licha ya mpangilio wa kitabu kwa jumla kufanana na hati za maagano kama zilivyoandikwa katika nchi zile wakati ule, hata mambo mengi yanayoshughulikiwa katika maagano hayo yanaonekana sehemu mbalimbali katika kitabu hicho.

Muhtasari[hariri | hariri chanzo]

1:1-4:43 Utangulizi wa historia

4:44-11:32 Maagizo ya msingi kuhusu agano

12:1-26:19 Amri zote zatajwa kinaganaga

27:1-30:20 Masharti ya agano

31:1-34:12 Siku za mwisho za Musa

Vitabu vinavyofuata Kumbukumbu la Sheria[hariri | hariri chanzo]

Vitabu vinavyofuata katika Biblia ya Kiebrania (Yoshua, Waamuzi, Samweli na Wafalme) vinataka kuthibitisha kwamba kweli ikawa kama hiki kinavyosema: Waisraeli walipofuata agano (wakati wa Yoshua) waliteka nchi ya ahadi na kuifurahia, lakini walipozidi kuasi (wakati wa Waamuzi, Samweli na Wafalme) walikuja kunyang’anywa nchi ile yote, kwanza sehemu nzuri zaidi (kaskazini), halafu ile hafifu zaidi (kusini). Hapo Waisraeli wote wakajikuta tena utumwani katika nchi ya kigeni kama kabla ya Musa, wakikosa hata sanduku la agano, lililopotea wakati wa maangamizi ya Yerusalemu na hekalu lake, baada ya wao kufikia hatua ya kula watoto wao kutokana na njaa.

Vitabu hivyo vilikamilishwa wakati wa kukaa uhamishoni Babeli, vikiwa jibu la swali kuu lililowakwaza huko: je, Mungu wetu ameshindwa? Waandishi walichagua matukio mbalimbali ya historia baada ya Yoshua ili kuthibitisha kuwa aliyeshindwa ni Israeli, si Mungu. Historia hiyo inaonyesha mfululizo wa maasi hata baada ya Mungu kutuma waamuzi na manabii wake ili kuwaonya Waisraeli na kuwaelekeza upya.

Lengo la waandishi halikuwa kutunza kumbukumbu za mambo yote kwa usahihi na ukamilifu, bali kuelekeza njia ya kupata wokovu hata baada ya Israeli kuonekana imekoma moja kwa moja. Kama vile Biblia nzima, vitabu hivyo vinalenga wokovu wetu, vikihakikisha kuwa Mungu anaweza kuleta mwanzo mpya hata hali ikiwa mbaya namna gani. Ndiyo sababu habari ya mwisho kabisa ni ya kuleta tumaini: kwamba mfalme Yekonia alitolewa gerezani (alipokaa miaka 37) na kufanywa mgeni wa kudumu mezani pa mfalme wa Babeli.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Vitabu vya ufafanuzi[hariri | hariri chanzo]

  • Craigie, Peter C (1976). The Book of Deuteronomy. Eerdmans.
  • Miller, Patrick D (1990). Deuteronomy. Cambridge University Press.
  • Phillips, Anthony (1973). Deuteronomy. Westminster John Knox Press.

Vingine[hariri | hariri chanzo]

  • Block, Daniel I (2005). "Deuteronomy". Katika Kevin J. Vanhoozer (mhr.). Dictionary for Theological Interpretation of the Bible. Baker Academic.
  • Bultman, Christoph (2001). "Deuteronomy". Katika John Barton, John Muddiman (mhr.). Oxford Bible Commentary. Oxford University Press.
  • Christensen, Duane L (1991). "Deuteronomy". Katika Watson E. Mills, Roger Aubrey Bullard (mhr.). Mercer Dictionary of the Bible. Mercer University Press.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.