Kitabu cha Hosea

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Hosea na mke wake Gomeri katika Bible Historiale, 1372.

Kitabu cha Hosea ni kimojawapo kati ya vitabu vya Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania), na hivyo pia vya Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo.

Kwa kuwa kina sura 14 tu, kimepangwa tangu zamani za kale kati ya vitabu 12 vya Manabii Wadogo.

Hata hivyo umuhimu wake katika maendeleo ya Ufunuo wa Mungu kwa Israeli ni mkubwa, kwa jinsi kilivyoathiri vitabu vilivyofuata hadi Kitabu cha Ufunuo.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo hayo.

Muda wa unabii wa Hosea[hariri | hariri chanzo]

Nabii Hosea alitokea Ufalme wa Israeli (Kaskazini) ambapo alifanya kazi ya unabii kuanzia miaka ya mwisho ya utawala wa Yeroboamu II (786 - 746 KK) hadi karibu na maangamizi ya mwaka 722 KK ambayo aliyatabiri kutokana na uasi wa kidini wa Waisraeli wenzake.

Wakati huohuo walifanya kazi pia Amosi upande wa Kaskazini, halafu Isaya katika Ufalme wa Kusini (Yuda).

Mada kuu[hariri | hariri chanzo]

Hosea alitangaza hasa upendo wa Mungu kwa taifa lake. Adhabu zenyewe zilizotabiriwa zinaelezwa kuwa zimetokana na upendo huo wenye wivu ambao unalenga kuwarudisha Waisraeli katika upendo mwaminifu wa kiuchumba.

Hosea alikuwa wa kwanza kumfananisha Mwenyezi Mungu na mume mwaminifu wa mwanamke malaya.

Maisha ya nabii mwenyewe yalikuwa na tabu ya namna hiyo ili yawe kwa wote kielelezo che uhusiano kati ya Mungu na watu wake.

Alidai Waisraeli wawe waaminifu kwa Mungu pekee, pamoja na kusisitiza kuwa dini haiwezi kuishia katika ibada zisizohuishwa na upendo, la sivyo wataangamia.

Muhtasari[hariri | hariri chanzo]

Mwanzoni mwa kitabu, Hosea aliagizwa na Mungu amuoe kahaba atakayemzalia wanaharamu anayewakilisha taifa la Israeli lililoabudu miungu mingine pia kama asili ya ustawi wake na kutegemea mbinu za kisiasa ili kujidumisha salama.

Kwa kuwa hawakumtegemea Mungu wao, Hosea aliwatabiria Waisraeli watapelekwa uhamishoni huko Ashuru.

Kama vile mke wa Hosea alivyoweza kujirekebisha, hivyo hata Israeli ikitubu itaokoka na kufaidika na baraka za Mungu.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]


Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.

Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kitabu cha Hosea kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.