Kitabu cha Isaya

Kitabu cha Isaya ni kati ya vitabu vya kinabii vya Tanakh (Biblia ya Kiebrania) na vya Agano la Kale ambayo ndiyo sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo.
Utunzi na mada
[hariri | hariri chanzo]Nabii Isaya (kwa Kiyahudi יְשַׁעְיָהוּ, yaani "YHWH anaokoa"), kuhani wa Yerusalemu mwenye elimu nzuri, alizaliwa katika Ufalme wa Yuda (Israeli Kusini) mwaka 765 hivi KK, akatabiri kwa muda usiopungua miaka 40 akiingilia kati matukio yote ya siasa, ambayo yalikuwa ya kutisha kutokana na nguvu za Waashuru ambao waliangamiza ufalme wa Israeli (Kaskazini) na kukaribia kufuta hata ufalme wa Kusini.
Maandishi yake yanapendeza kuliko yote ya Kiyahudi, hasa upande wa ushairi. Lakini ukuu wa Isaya uko hasa upande wa imani.
Kuanzia wito wake alioupata hekaluni, alipong’amua kwamba Mwenyezi Mungu ni mtakatifu kabisa, yaani tofauti mno na yeyote na chochote (6), alitawaliwa na wazo la utukufu wa Mungu na la unyonge wa binadamu anayehitaji kutakaswa naye. Kwa msingi huo alidai wafalme na wananchi wote wa Yuda wamtegemee Mungu tu, si mataifa yenye nguvu, hata upande wa siasa na mbele ya hatari kubwa namna gani.
Lakini toka mwanzo aliambiwa hatasikilizwa, hivyo ikambidi atabiri adhabu. Kweli hali haikuwa shwari, ndiyo sababu wengi walishindwa kuamini na kutulia, wakaendelea kujifanyia mipango na kutafuta msaada kutoka kwa binadamu, hasa Farao wa Misri. Hapo Mungu alimuagiza Isaya atembee uchi mwaka mmoja unusu ili kudokeza kuwa Wamisri watafanywa watumwa wa Waashuru wasiweze kusaidia kitu (20:1-6).
Katika kutuliza watu alimtabiria mfalme Ahazi kwamba mwanamwali atamzaa mtoto wa kiume atakayethibitisha uwepo wa Mungu pamoja na watu wake, jina lake Emanueli litakavyomaanisha. (7:1-17) Kweli mke wa Ahazi alimzaa Hezekia atakayeendeleza ufalme wa ukoo wa Daudi, lakini Wakristo wanaona utabiri huo ulimlenga zaidi Yesu, mwana wa Bikira (walivyoelewa watafsiri wa kwanza wa Biblia katika Kigiriki) ambaye kweli ni Mungu pamoja nasi, na ni mwana wa Daudi ambaye atatawala milele kwa amani na haki (11:1-9).
Hivyo, pamoja na adhabu kwa utovu wao wa imani (22:1-14), Isaya aliwatabiria watu wa Yuda kuwa Mungu hataangamiza kabisa taifa lake, bali ataacha mabaki yake ambayo yataleta wokovu (10:20-23): katika mabaki hayo Bikira atamzaa Masiya ambaye ni Mungu pamoja nasi, mwana wa Daudi ambaye ataleta amani na haki duniani.
Nafasi ya mwisho kwa Isaya kutuliza watu ilikuwa mwaka 701 KK ambapo jeshi kubwa la Waashuru lilizingira Yerusalemu na kutamka maneno ya kumkufuru Mungu. Isaya aliwarudishia jibu la dharau, nao kweli wakakimbia haraka baada ya kupatwa na tauni.
Isaya ni maarufu pia kwa ubora wa mashairi yake yaliyofanya ujumbe wake upendeze na uguse zaidi. Kwa sababu hiyo wengi walipenda kuyakariri na kuyasoma na hata kuiga mtindo wake: ndiyo maana kitabu chake kiliongezewa maandishi mengine mengi mpaka miaka mingi baada ya mwenyewe kuuawa kwa kukatwa kwa msumeno wakati wa mfalme Manase.
Isaya wa Pili
[hariri | hariri chanzo]Katika kitabu chake unapatikana pia unabii wa wafuasi wake wa mbali wasiojulikana kwa jina, waliofanya kazi katika miaka 550-500 hivi K.K.
Ni kwamba, ingawa Ezekieli alifanya kazi nzuri, waliokuwa kwenye Uhamisho wa Babeli au Babuloni waliendelea kuzoea na kufurahia mazingira mapya yenye ustawi wa kiuchumi wakazidi kupotewa na hamu na tumaini la kurudi Yerusalemu.
Ndiyo sababu Mungu aliwatumia nabii mwingine mkubwa: hatujui jina lake, lakini tunamuita Isaya II kwa kuwa alifuata mapokeo ya Isaya na kulingana naye kwa ufasaha wa mashairi aliyoyatumia kutolea ujumbe wake; hivyo maandiko yake yamepangwa katika kitabu cha Isaya (40-55).
Sehemu hiyo inaitwa pia kitabu cha faraja ya Israeli kwa sababu ililenga kuwatia moyo Wayahudi wenzake huko Babeli kwamba Mungu atawarudisha kwao akitumia kama chombo chake mfalme Mpagani, kwa kuwa yeye anatawala watu wote pamoja na mioyo yao (Is 40:1-11). Hivyo akawafanya watamani kurudi badala ya kukwama katika kujitafutia maendeleo ya kidunia.
Kwa uchangamfu wa hali ya juu Isaya II alitabiri ukombozi na mwanzo mpya wa taifa kama ajabu kubwa kuliko lile la mababu wao kutoka Misri chini ya Musa. Alilifananisha na uumbaji mpya utakaowezekana kwa sababu Mungu wa Israeli si mmoja kati ya wengi, walivyodhani kwa muda mrefu, bali kweli ni peke yake, hakuna mwingine: ndiyo sababu anaweza yote. Imani hiyo ilizidi kutia mizizi kati ya Wayahudi na kuwaimarisha dhidi ya kishawishi cha kuabudu wengine.
Pamoja na hayo, katika sura hizo mna mashairi manne bora kuhusu mtumishi mteswa wa Bwana ambayo ndiyo utabiri bora juu ya Yesu na juu ya wokovu atakaoleta kwa kuteseka mwenyewe ili kufidia dhambi za wote (42:1-4; 49:1-6; 50:4-9; 52:13-53:12). Hatimaye Isaya II ndiye aliyeandaa dini ya Kiyahudi kupokea mataifa yote.
Isaya wa Tatu
[hariri | hariri chanzo]Isaya 56-66 ni sura za baadaye tena (Isaya III, mwaka 500 hivi K.K.) ambazo zinawakaribisha watu wa mataifa yote kujiunga na Israeli katika kumuabudu Mungu pekee. Kiini chake ni Isa 61:1-3.
Ufafanuzi
[hariri | hariri chanzo]Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Bandstra, Barry L. (2008). Reading the Old Testament: an introduction to the Hebrew Bible. Cengage Learning. ISBN 978-0495391050.
- Barker, Margaret (2003). "Isaiah". Katika Dunn, James D. G.; Rogerson, John William (whr.). Eerdmans Commentary on the Bible. Eerdmans. ISBN 9780802837110.
- Becker, Uwe (2020). "The Book of Isaiah: Its Composition History". Katika Lena-Sofia Tiemeyer, Lena-Sofia (mhr.). The Oxford Handbook of Isaiah. Oxford University Press. ISBN 978-0-19-066924-9.
- Blenkinsopp, Joseph (2002). Isaiah 40–55: A new translation with introduction and commentary. Doubleday. ISBN 0-385-49717-2.
- Blenkinsopp, Joseph (2003). Isaiah 56–66: A new translation with introduction and commentary. Doubleday. ISBN 0-385-50174-9.
- Boadt, Lawrence (1984). Reading the Old Testament:An Introduction. Paulist Press. ISBN 9780809126316.
- Brettler, Marc Zvi (2010). How to read the Bible. Jewish Publication Society. ISBN 978-0-8276-0775-0.
- Brueggemann, Walter (2003). An introduction to the Old Testament: the canon and Christian imagination. Westminster John Knox. ISBN 978-0-664-22412-7.
- Cate, Robert L. (1990a). "Isaiah". Katika Mills, Watson E.; Bullard, Roger Aubrey (whr.). Mercer Dictionary of the Bible. Mercer University Press. ISBN 9780865543737.
- Cate, Robert L. (1990b). "Isaiah, book of". Katika Mills, Watson E.; Bullard, Roger Aubrey (whr.). Mercer Dictionary of the Bible. Mercer University Press. ISBN 9780865543737.
- Childs, Brevard S. (2001). Isaiah. Westminster John Knox Press. ISBN 9780664221430.
- Clifford, Richard (1992). "Isaiah, Book of: Second Isaiah". Katika Freedman, David Noel (mhr.). The Anchor Bible Dictionary. Juz. la 3. Doubleday. uk. 473. ISBN 0385193610.
- Cohn-Sherbok, Dan (1996). The Hebrew Bible. Cassell. ISBN 0-304-33702-1.* Coogan, Michael D. (2009). A Brief Introduction to the Old Testament. Oxford University Press.
- Gnuse, Robert Karl (1997). No Other Gods: Emergent Monotheism in Israel. Continuum. ISBN 9781850756576.* Goldingay, John (2001). Isaiah. Hendrickson Publishers. ISBN 0-85364-734-8.
- Goldingay, John (2005). The message of Isaiah 40–55: a literary-theological commentary. Continuum International Publishing Group. ISBN 9780567030382.
- Hannah, Darrell D. (2005). "Isaiah Within Judaism of the Second Temple Period". Katika Moyise, Steve; Menken, Maarten J.J. (whr.). Isaiah in the New Testament: The New Testament and the Scriptures of Israel. Continuum. ISBN 9780802837110.
- Lemche, Niels Peter (2008). The Old Testament between theology and history: a critical survey. Westminster John Knox Press. ISBN 9780664232450.
- Petersen, David L. (2002). The Prophetic Literature: An Introduction. Westminster John Knox Press. ISBN 9780664254537.
- Sawyer, John F.A. (1996). The Fifth Gospel: Isaiah in the History of Christianity. Cambridge University Press. ISBN 9780521565967.
- Soggin, J. Alberto (1989). Introduction to the Old Testament: From Its Origins to the Closing of the Alexandrian Canon. Westminster John Knox Press. ISBN 0-664-21331-6.
- Stromberg, Jake (2011). An Introduction to the Study of Isaiah. Continuum International Publishing Group. ISBN 9780567363305.
- Sweeney, Marvin A. (1996). Isaiah 1–39: With an Introduction to Prophetic Literature. Eerdmans. ISBN 9780802841001.
- Sweeney, Marvin A. (1998). "The Latter Prophets". Katika McKenzie, Steven L.; Graham, Matt Patrick (whr.). The Hebrew Bible Today: An Introduction to Critical Issues. Westminster John Knox Press. ISBN 9780664256524.
- Whybray, R. N. (2004). The Second Isaiah. T&T Clarke. ISBN 9780567084248.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]
Tafsiri
- Book of Isaiah – Hebrew, side by side with English
- Book of Isaiah (English translation [with Rashi's commentary] at Chabad.org)
- Bible Gateway
Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki
Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.
| Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kitabu cha Isaya kama historia yake au athari wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
