Isaya II

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Isaya II ni jina lililobuniwa na wataalamu wa Biblia ili kumtaja mwandishi wa Isa 40-55.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Katika kitabu cha Isaya, pamoja na habari za Nabii Isaya, unapatikana pia unabii wa wafuasi wake wasiojulikana, waliofanya kazi katika miaka 550-500 hivi K.K., na hasa ule wa Isaya II.

Ni kwamba, ingawa Nabii Ezekieli alifanya kazi nzuri, waliokuwa uhamishoni Babuloni waliendelea kuzoea na kufurahia mazingira mapya yenye ustawi wa kiuchumi wakazidi kupotewa na hamu na tumaini la kurudi Yerusalemu.

Ndiyo sababu Mungu aliwatumia nabii mwingine mkubwa: hatujui jina lake, lakini tunamuita Isaya II kwa kuwa alifuata mapokeo ya Isaya na kulingana naye kwa ufasaha wa mashairi aliyoyatumia kutolea ujumbe wake; hivyo maandiko yake yamepangwa katika kitabu cha Isaya (40-55).

Sehemu hiyo inaitwa pia kitabu cha faraja ya Israeli kwa sababu ililenga kuwatia moyo Wayahudi huko Babeli kwamba Mungu atawarudisha kwao akitumia kama chombo chake mfalme Mpagani, kwa kuwa yeye anatawala watu wote pamoja na mioyo yao (Is 40:1-11). Hivyo akawafanya watamani kurudi badala ya kukwama katika kujitafutia maendeleo ya kidunia.

Kwa uchangamfu wa hali ya juu Isaya II alitabiri ukombozi na mwanzo mpya wa taifa kama ajabu kubwa kuliko lile la mababu wao kutoka Misri chini ya Musa. Alilifananisha na uumbaji mpya utakaowezekana kwa sababu Mungu wa Israeli si mmoja kati ya wengi, walivyodhani kwa muda mrefu, bali kweli ni peke yake, hakuna mwingine: ndiyo sababu anaweza yote. Imani hiyo ilizidi kutia mizizi kati ya Wayahudi na kuwaimarisha dhidi ya kishawishi cha kuabudu wengine.

Pamoja na hayo, katika sura hizo mna mashairi manne bora kuhusu mtumishi mteswa wa Bwana ambayo ndiyo utabiri bora juu ya Yesu na juu ya wokovu atakaoleta kwa kuteseka mwenyewe ili kufidia dhambi za wote (42:1-4; 49:1-6; 50:4-9; 52:13-53:12). Hatimaye Isaya II ndiye aliyeandaa dini ya Kiyahudi kupokea mataifa yote.

Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Isaya II kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.