Nabii Ezekieli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nabii Ezekieli alivyochorwa na Michelangelo katika Cappella Sistina, Vatikani.

Nabii Ezekieli (kwa Kiebrania יְחֶזְקֵאל, Y'ḥez'qel) ni mmojawapo kati ya manabii muhimu zaidi wa Israeli katika Agano la Kale. Alifanya kazi miaka 592-570 hivi K.K., kadiri ya ushahidi wa kitabu chake.

Habari zake tunazipata katika kitabu hicho tu, anapotajwa kwa jina mara tatu, kumbe kwa kawaida Mungu anamuita “binadamu”.

Mwana wa kuhani Buzì, wakati wa Uhamisho wa Babeli, alijaliwa njozi iliyomuonyesha utukufu wa Mwenyezi Mungu na, kisha kufanywa mlinzi wa Waisraeli, alilaumu uasi wa taifa hilo teule, alitabiri maangamizi ya karibuni ya mji mtakatifu, Yerusalemu, na uhamisho wa wakazi wake. Akiwa kati yao, alidumisha tumaini lao, akitabiri kwamba mifupa yao iliyokauka kabisa itafufuliwa kuwa na uhai mpya[1].

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu, hasa tarehe 23 Julai[2][3].

Mazingira yake[hariri | hariri chanzo]

Polepole Wayahudi waliohamishiwa Babeli waliweza kujitafutia kazi (kwanza kilimo, halafu biashara), wakafaulu sana, hata wengine wakawa watumishi wa serikali.

Lakini upande wa dini walikuwa hatarini, kwa sababu imani ya Mwisraeli inategemea taifa, nchi na hekalu ambavyo vyote vilikuwa vimeharibika.

Kwa ajili yao Mungu akatuma tena manabii, hasa Ezekieli ambaye anaonekana kuwa alihamishwa tangu mwaka 598 KK. Kabla hajahamishwa aliweza kumfahamu Yeremia, na kweli aliathiriwa na ujumbe wake ambao aliuunga mkono na kuuendeleza.

Kazi yake[hariri | hariri chanzo]

Alifanya unabii wake hukohuko uhamishoni, ingawa ujumbe wake uliwalenga waliobaki Yuda pia. Kwanza aliwatolea maneno ya hukumu ili watubu kabla hawajaangamia, lakini baadaye akawapa maneno ya faraja wasikate tamaa. Katika kuwahakikishia kuwa wataanza upya nchini kwao aliwapa maelekezo yote kwa ajili hiyo. Kwa namna ya pekee, akiwa kuhani, kama vile Yeremia, katika kitabu chake alishughulika sana na hekalu na mambo ya ibada.

Upande mwingine alianzisha mtindo mpya wa unabii ambao unaitwa wa Kiapokaliptiko (kilele chake ni Ufunuo wa Yohane) na ambao hauhusu tena matukio madogomadogo ya siasa, bali kwa njozi za ajabuajabu unaonyesha maana ya historia yote mpaka mwisho. Njozi 4 anazozisimulia kinaganaga na zisizosahaulika (utukufu wa Mungu kuhama hekalu, utukufu huo kurudi hekaluni, hekalu kutokwa na maji yenye uwezo wa kuponya hata Bahari ya Kifo, hatimaye mifupa mikavu kusimama na kuishi tena) zinachukua nafasi kubwa katika kitabu chake na kwa mafumbo yake yanavutia ubunifu wetu ujitahidi kuelewa yaliyofichika katika mifano, tarakimu, rangi n.k.

Dini ya Kiyahudi mpaka leo inategemea sana kazi aliyoifanya Ezekieli ya kukazia utekelezaji wa Torati hata pasipo uhuru wa kisiasa. Muhimu kwake ni kwamba Wayahudi popote walipo wamtukuze Mungu kwa kufuata sheria yake. Tena alitabiri kuwa Mungu tu atawawezesha kufanya hivyo kwa kugeuza mioyo yao migumu kama mawe yadunde kama ile ya nyama, au vizuri zaidi kwa kuwatia moyo mpya na roho mpya wazishike amri zake (11:17-20; 36:26). Mungu atawaokoa kabla hawajatubu ili jina lake litukuzwe katika watu wake: wokovu anaouleta hautegemei matendo mema ya binadamu, bali muungano wa Mungu na wale walioitwa kwa jina lake (16:58-63). Hakuna kitabu kinachosisitiza utukufu wa Mungu kuliko hicho.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Marejeo ya Kiislamu[hariri | hariri chanzo]

  • Ibn Kutayba, K. al-Ma'arif ed. S. Ukasha, 51
  • Tabari, History of the Prophets and Kings, 2, 53–54
  • Tabari, Tafsir, V, 266 (old ed. ii, 365)
  • Masudi, Murudj, i, 103ff.
  • K. al-Badwa l-tarikh, iii, 4/5 and 98/100, Ezechiel
  • Abdullah Yusuf Ali, Holy Qur'an: Translation and Commentary, Note. 2473 (cf. index: Ezekiel)

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Nabii Ezekieli kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.