Nenda kwa yaliyomo

Uyahudi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Dini ya Kiyahudi)
"Magen David" au nyota ya Daudi ni ishara ya Uyahudi
Menora au tawafa ya mikono saba pamoja na yarmulke au kofia ya Kiyahudi ni pia ishara za imani

Uyahudi ni mojawapo kati ya dini za kale za binadamu, lakini jina hilo lilienea baada ya makabila mengi ya Israeli kutoweka, hata wakabaki karibu watu wa kabila la Yuda tu.

Uyahudi (Yuda) ni pia jina la kihistoria la sehemu ya kusini ya nchi ya Palestina au Israel.

Kwa jumla kuna namna mbili za kuangalia Uyahudi: ama kama dini au kama taifa. Namna zote mbili huchanganyikana na kutumiwa pamoja mara kwa mara.

Kuna Wayahudi wanaojitazama raia wa nchi fulani na Uyahudi wao ni katika imani tu. Kuna Wayahudi wengine wanaosema hawafuati dini ya Kiyahudi wala hawaamini lakini wanajisikia kuwa Wayahudi kwa sababu ya ukoo na pia desturi za utamaduni wao.

Wafuasi wa dini hiyo huitwa "Wayahudi" hata wasipokuwa na asili ya taifa hilo.

Hata wakati ambapo idadi yao ilikuwa ndogo duniani, imani yao ilikuwa na athira kubwa. Wataalamu wengine huuita "dini mama" ya Ukristo na Uislamu.

Siku hizi wako karibu milioni 15 duniani kote, hasa nchini Israel na Marekani.

Imani

Imani yake ni kwamba Mungu ni mmoja tu na wa milele; anajua na kuweza yote; ndiye aliyeumba mbingu na dunia akamteua Ibrahimu kuwa baba wa taifa la Mungu.

Kuna namna mbalimbali katika imani ya Kiyahudi kama madhehebu.

Mara nyingi kanuni 13 za mwalimu Myahudi Maimonides aliyeishi katika karne ya 12 hukubaliwa na Wayahudi wengi[1].

  1. Mungu alikubali kila kita anaendelea kuangalia uumbaji wake.
  2. Mungu ni mmoja tu, hana kasoro wala kosa.
  3. Mungu hana mwili, hafanani na kitu chochote duniani.
  4. Mungu alikuwepo daima, ataendelea kuwepo milele.
  5. Sala zifanywe kwa Mungu pekee.
  6. Mafundisho ya manabii wa Kiyahudi ni ya kweli.
  7. Musa alikuwa nabii mkuu kwa nyakati zote, hakuna atakayemshinda.
  8. Mungu alimpa Musa Torati wa kimaandishi na Torati wa kimdomo.
  9. Torati haitabadilishwa wala hapatakuwa na Torati nyingine.
  10. Mungu anajua dhana na mawazo wa kila mtu.
  11. Mungu atawatuza wenye haki na kuwaadhibu waovu.
  12. Masiya atakuja.
  13. Wafu watafufuka.

Tanakh

Msingi wa Imani ya Kiyahudi ni maandiko matakatifu ya Biblia ya Kiebrania au Tanakh. Maandiko hayo hukubaliwa pia na Wakristo katika Agano la Kale ambalo ni sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo.

Ndani ya maandiko hayo mara nyingi vitabu vya Torati huheshimiwa sana kama neno la Mungu mwenyewe lililotolewa kwa Musa.

Halafu vitabu vya manabii vinavyotazamiwa kama maneno yaliyotamkwa na manabii kwa agizo la Mungu.

Ngazi ya tatu ni maandiko mengine (ketuvim) yanayoaminiwa ni maandiko ya kibinadamu yaliyoongozwa na Roho wa Mungu.

Talmudi

Mbali ya Biblia, huheshimiwa pia maandiko ya Talmudi ambayo ni maelezo ya Biblia kuhusu maswali ya imani, historia na mapokeo ya Kiyahudi.

Ni wazi kwa Wayahudi kwamba Talmudi ni maneno ya kibinadamu.

Mitzvot - Amri

Kuna matendo fulani ambayo ni muhimu katika imani hiyo. Yanaitwa mitzvot au amri ya Mungu kwa Wayahudi.

Kuna amri 613 zinazojulikana kutoka Torati.

Sehemu ya amri hizo hazitekelezwi leo kwa sababu zinahusu hekalu la Yerusalemu lililoharibiwa mwaka 70 BK.

Amri kumi zina nafasi ya pekee kati ya amri zote.

Pamoja na amri hizo za Torati kuna maelezo mapana katika Talmudi. Hata madai ya Talmudi mara nyingi zatajwa kama "mizvot". Ila tu ni tabia ya Uyahudi ya kwamba wataalamu hutofautiana juu ya maelezo haya mara kwa mara.

Tanbihi

  1. What Do Jews Believe?, tovuti ya Jewfaq.org, iliangaliwa Novemba 2022
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.