Gibraltar
Gibraltar ni eneo la ng'ambo la Uingereza ambalo linaundwa na rasi ndogo katika bahari ya Mediteranea kwenye ncha ya kusini ya rasi ya Iberia katika Ulaya ya Kusini. Imepakana na Hispania.
Umuhimu wa Gibraltar
[hariri | hariri chanzo]Gibraltar imekuwa mahali muhimu tangu karne nyingi kwa sababu rasi hii iko kwenye Mlango wa Gibraltar ambako kuna km 14 za maji tu kati ya Afrika na Ulaya. Mwenye kutawala Gibraltar aliweza kutawala mwendo wa jahazi na meli kati ya Atlantiki na Mediteranea wakati wa vita. Hii ni sababu ya kwamba Uingereza ilitwaa rasi hii na kuitetea tangu mwaka 1704.
Jina la Gibraltar
[hariri | hariri chanzo]Jina la Gibraltar limetokana na uvamizi wa Waarabu wakati wa upanuzi wa Uislamu. Mwaka 711 jemadari Tariq ibn-Ziyad aliongoza jeshi lake kushambulia Hispania. Rasi inayoitwa leo "Gibraltar" ilipewa jina la "jabal at-Tariq" (mlima wa Tariq) lililotamkwa baadaye "Gibraltar". Kabla ya kuja kwa Waarabu mataifa ya kale yaliita mlango huu "Nguzo za Herakles" wakitaja milima midogo ya Gibraltar na Ceuta kwa jina hili.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Gibraltar ilikuwa sehemu ya Hispania kati ya 1501 na 1704. Mwaka 1704 wakati wa vita kati ya Hispania na Uingereza ilitwaliwa na Waingereza na Waholanzi. Mwaka 1713 Hispania ilikubali kwa nafasi ya amani ya Utrecht kuwa rasi itakuwa chini ya mamlaka ya Uingereza.
Hispania imedai mara nyingi kurudishiwa eneo hilo ikishtaki Uingereza kuwa na koloni la mwisho katika Ulaya. Lakini wakazi wenyewe walipigia kura mwaka 2002 hoja ya kubaki upande wa Uingereza badala ya Hispania na zaidi ya 98% wakakubali.
Mengine
[hariri | hariri chanzo]Wakazi wa Gibraltar ni takriban 32,000 walio wengi huwasiliana kwa Kilyanito, lahaja ya Kihispania, lakini wote wajua Kiingereza.
Upande wa dini, 72.1% ni Wakatoliki, 7.7% Waanglikana, 3.8% Wakristo wa madhehebu mengine, 3.6% Waislamu, 2.4% Wayahudi, 2.0% Mabanyani, n.k.
Mwamba wa Gibraltar wenye kimo cha mita 426 ni mahali pa pekee Ulaya penye nyani huru.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Government of Gibraltar
- The Unofficial Homepage
- Gibraltar Broadcasting Corporation (with radio streaming)
- Virtual Tour of Gibraltar Ilihifadhiwa 11 Machi 2007 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Gibraltar kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |