Rasi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rasi ndogo

Rasi (pia:peninsula lat. nusukisiwa) ni sehemu ya nchi inayoelekea katika maji ya bahari au ziwa na kuzungukwa na maji pande tatu. Ni kama kisiwa kinachounganishwa na bara upande mmoja tu.

Rasi inaeza kuwa ndogo au kubwa. Mifano ya rasi kubwa ni nchi za Italia na Korea au Bara Hindi.

Rasi kubwa barani Afrika ni Pembe la Afrika.

Rasi ndogo zaidi mara nyingi zina umaarufu fulani kwa sababu zilikuwa alama muhimu ya kutambua njia ya baharini zamani za usafiri kwa jahazi (meli za tanga). Mifano mashuhuri ni Rasi ya Tumaini Jema na Rasi Agulhas kwenye ncha ya kusini ya Afrika, Rasi Delgado iliyokuwa alama ya mpaka kati ya utawala wa Wareno na Wajerumani katika Afrika ya Mashariki na hivyo hadi leo mwisho wa mpaka kati ya Msumbiji na Tanzania.

Rasi hizi ndogo ziliweza kuhofiwa na wanabaharia za jahazi kwa sababu mara nyingi mikondo ya maji ndani ya bahari iliathirikia kwa ghafla na rasi hizi na jahazi zilizosafiri karibu na pwani ziliweza kusukumwa ghafla kuelekea nchi penye miamba.