Andorra

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Andorra
Ramani ya Andorra

Utemi wa Andorra (Kikatalani: Principat d'Andorra, Kifaransa: Principauté d'Andorre) ni nchi ndogo katika Ulaya ya kusini magharibi.

Katiba yake ni ya utemi lakini kuna watemi wawili, nao wako nje ya nchi. Mmoja ni rais wa Ufaransa na mwingine ni askofu wa Urgell katika Hispania.

Andorra ni nchi mwanachama ya Baraza la Ulaya lakini si ya Umoja wa Ulaya. Hivyo si sehemu ya eneo la kodi za pamoja la Ulaya. Hali hii inavuta watalii kwa sababu bidhaa nyingi zinapatikana bila kodi kwa bei nafuu kuliko Hispania au Ufaransa; kodi ya ongezeko la thamani (VAT) iko kwenye 4% pekee.

Andorra inatumia pesa ya Euro bila kushiriki katika mkataba wa Euro.

Siku hizi imekuwa nchi tajiri kutokana na utalii.

Jiografia[hariri | hariri chanzo]

Eneo la Andorra ni bonde katika milima ya Pirenei kati ya Hispania na Ufaransa. Mahali pake mlimani palisababisha imeendelea kama nchi ya pekee kwa sababu zamani hapakuwa na njia wala mawasiliano.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Asili ya Andorra kama nchi ya pekee ni katika karne ya 12 na katika mahali pake mlimani na mpakani kati ya Ufaransa na Hispania. Bonde la Andorra lilikuwa chini ya mtemi wa Urgell. Wakati ule hapakuwa bado na himaya moja kwa Hispania nzima. Kama historia ingeendelea kama kawaida, leo hii Andorra ingekuwa tu sehemu ya wilaya ndani ya Hispania. Lakini katika karne ya 11 palitokea ugomvi kati ya mtemi wa Urgell na jirani yake. Majirani walipatana ya kwamba watatawala bonde kwa pamoja.

Baadaye eneo la jirani liliingizwa katika ufalme wa Ufaransa na haki za kuwa mtemi mshiriki zilirithiwa na mfalme wa Ufaransa. Haki za mtemi wa Urgell zilirithiwa na askofu wa Urgell. Katika mwendo wa historia wafalme wa Ufaransa walipotea, hivyo rais wa jamhuri ya Ufaransa alirithi haki za utawala kama mtemi wa kushirikiana. Cheo cha askofu wa Urgell kimeendelea hadi wakati huu.

Miaka yote ya nyuma Andorra ilikuwa bonde maskini tu bila barabara nzuri, hivyo wala Hispania wala Ufaransa ziliona umuhimu wa kujitahidi ili kupata utawala kamili juu yake.

Katika hali hii Andorra imefika katika karne ya 21, ila tu mawasiliano ya kisasa yameondoa upweke na utalii umetajirisha nchi na wakazi wake.

Tarehe 14 Machi 1993 Andorra ilipata katiba iliyoifanya kuwa nchi huru ya kujitegemea kabisa. Nafasi ya watemi wa pamoja ni ya heshima tu, na utawala halisi umo mikononi mwa serikali inayochaguliwa na bunge.

Tangu 1993 Andorra ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Watu[hariri | hariri chanzo]

Idadi ya wakazi ni 85,000, ambao kati yao 2/3 si wananchi. Lugha rasmi ni Kikatalunya. 90.1% ya wakazi ni Wakatoliki.

Picha[hariri | hariri chanzo]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Andorra kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.