Koloni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Koloni ni eneo lililo chini ya nchi nyingine ambayo ni mbali.

Neno latumiwa kwa kutaja

  • makazi mapya ya watu kutoka eneo moja katika eneo jingine
  • eneo linalotawaliwa na nchi ya mbali hasa kwa kusudi la kufaidi na malighafi yaliyopo au kwa shabaha ya kuwa na kituo cha kijeshi au cha biashara.

Asili ya neno[hariri | hariri chanzo]

Asili ya neno koloni ni kilatini "colonia" kutokana na kitenzi "colere" (kulima, pia kuabudu). Colonia ilikuwa makazi ya Waroma wa Kale nje ya eneo lao la awali. Chanzo chake kilikuwa mji mpya uliokaliwa na wanajeshi wastaafu waliopewa ardhi ya shamba kama pensheni yao. Koloni za aina hii zilinazishwa hasa mpakani wa maeneo mapya yaliyotwaliwa karibuni na kungizwa katika Dola la Roma. Walowezi walipewa mashamba yao kwa masharti ya kuwa tayari kutetea mipaka kama vita inatokea.

-Tazama: Koloni nyakati za kale-

Aina za koloni[hariri | hariri chanzo]

Koloni zilienea hasa tangu upanuzi wa nchi za Ulaya tangu karne ya 15.

Koloni zilianzishwa kwa njia mbalimbali:

  • Vituo vya biashara viliundwa kwenye pwani za Afrika na Asia. Vingine viliimarishwa kuwa koloni kamili. Mfano wake ni Afrika Kusini ambako Waholanzi walipeleka walowezi kwa kusidi la kulima vyakula kwa mahitaji ya jahazi zilizosafiri kati ya Ulaya na Asia ya Kusini.
  • Koloni zilianzishwa kwa kusudi la kulima mazao au kupata malighafi yasiyopatikana walikotoka wakoloni. Mfano wake ni Peru ambako Hispania ilijipatia fedha. Mfano mwingine ni visiwa vya Karibi vilivyogeuzwa kuwa mashamba ya miwa kwa mahitaji ya sukari ya Ulaya.
  • Koloni kadhaa zilianzishwa kwa shabaha za kijeshi ili kuwa na kituo cha kijeshi au bandari. Mfano wake ni Gibraltar.
  • Koloni ziliundwa kwa shabaha ya kupeleka walowezi huko. Mfano wake ni koloni za Uingereza katika Amerika Kaskazini zilizokuwa baadaya nchi ya Marekani. Nyingine ziliundwa kwa kusudi la kuwapeleka wafuasi wa madhehebu ya kidini yasiyopendwa Uingereza penyewe au kwa shabaha ya kuwapeleka huko watu maskini waliokosa ardhi ya mashamba kwao. Australia ilianzishwa kama koloni ya wafungwa wa magereza waliopelekwa mbali ili kuwaondoa nyumbani.
Uenezaji wa Ukoloni wa kisasa tangu karne ya 15 hadi 20 -Subiri mabadiliko ya ramani !

Ukoloni[hariri | hariri chanzo]

Hasa mwisho wa karne ya 19 nchi za Ulaya zilitwaa maeneo na kuyafanya koloni kwa hofu ya kwamba nchi nyingine itayachukua. Kuwa na koloni ilikuwa kama dalili ya kuwa nchi yenye maana inayoheshimiwa. Mwisho wa karne ya 19 takriban 80% za maeneo yote duniani yalitawaliwa kama koloni ya namna moja au nyingine. Kipindi hiki cha ukoloni kiliporomoka baada ya vita kuu ya pili ya dunia.

Nchi lindwa na koloni[hariri | hariri chanzo]

Hali ya nchi chini ya utawala wa kikoloni zilitofautiana.

Kwa upande moja palikuwa na koloni zilizotawaliwa moja kwa moja na watawala wa nje. Kwa upande mwingine palikuwa na nchi na maeneo ambako watawala wenyeji waliendelea kuwa na madaraka lakini walipaswa kushauriana na wawakilishi wa nchi kubwa. Nchi hizi zilitazamiwa mara nyingi kama “nchi lindwa” chini ya ulinzi wa Uingereza, Ufaransa na kadhalika.

Kuna mifano ambako hali ya kuwa nchi lindwa ilidumu muda mfupi tu kabla ya kumezwa kabisa na kuwa sehemu ya koloni kamili. Mfano wake mmoja ni usultani wa Witu iliyoingizwa katika koloni ya Kenya bila kujali mawazo wa mtawala wa kienyeji au watu wake.

Lakini kuna pia mifano ambako mikataba asilia na wenyeji iliheshimiwa na mwisho wa ukoloni maeneo haya yamekuwa nchi huru. Kati ya mifano yake ni Falme za Kiarabu na Botswana iliyokaa nchi ya pekee nje ya Afrika Kusini ingawa serikali ya Afrika Kusini ilitaka iwe chini yake.

Kwa jumla Uingereza ulipendelea mara nyingi utawala kupitia wenyeji kuliko kuwatawala moja kwa moja. Utawala wa moja kwa moja ulipendelewa kwa mfano na Ufaransa katika koloni zake.

Hourglass.svg Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Koloni kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.