Hammurabi
Hammurabi (takr. 1810 KK - 1750 KK) alikuwa mfalme wa sita wa mji wa Babeli akapanua eneo lake na kuunda milki ya kwanza ya Babeli. Anajulikana hasa kwa mkusanyo wa sheria za Hammurabi ambazo ni kati ya sheria za kwanza za dunia zilizoandikwa.
Hammurabi alirithi ufalme kutoka kwa baba yake akitawala eneo la mji wa Babeli kama dola-mji tu. Katika miaka ya utawala wake alifaulu kupanua himaya yake hadi kutawala Mesopotamia yote. Hivyo alianzisha milki ya kwanza ya Babeli.
Sheria za Hammurabi
[hariri | hariri chanzo]Umaarufu wake watokana na sheria zake. Hakuwa mtawala wa kwanza wa Mesopotamia aliyetunza sheria za milki kimaandishi. Lakini sheria nyingine zimepotea au kuhifadhiwa kwa sehemu tu. Mkusanyo wa sheria za Hammurabi ni wa kwanza uliosambazwa kiasi cha kuwa na nakala nyingi, hivyo nakala kadhaa zimehifadhiwa hadi leo na kutupa picha ya jamii ile ya kale sana.
Nakala maarufu ni nguzo ya jiwe kubwa lenye kimo cha mita 2.25 inayomwonyesha mfalme mbele ya mungu Marduk na chini yake ziko sheria katika mwandiko wa kikabari.
Sheria hizi zilikuwa kali sana. Mfano wake ni vipengele vifuatavyo:
- na. 3: Anayesimama mahakamani na kutoa ushuhuda katika kesi yenye adhabu ya kifo lakini hawezi kuthibitisha maneno yake atakufa
- na. 195: Mwana anayempiga baba yake atakatwa mkono
- na. 196: Anayeharibu jicho la mtu huru atang'olewa jicho lake.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Hammurabi kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |