Nenda kwa yaliyomo

Marduk

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Marduk na Mušḫuššu - uchoraji kufuatana na mhuri kutoka Babeli

Marduk ni jina la mungu mlinzi wa mji wa Babeli (Mesopotamia, leo Iraki). Pamoja na uenezi wa mamlaka ya Babeli katika Mesopotamia ya kale Marduk aliongezewa ibada na heshima na kuitwa mungu mkuu kuliko miungu wote katika dini ya Babeli. Ishara zake zilikuwa joka lake na aina ya jembe.

Kiasili Marduk alikuwa mungu mlinzi wa mji Babeli tu. Mfalme Hammurapi I alifaulu kupanua utawala wake juu ya madola-miji mingine ya Mesopotamia. Hapo alimtangaza Marduk kama mungu mkuu juu ya miungu yote mingine.

Wafalme wote wa Babeli walipaswa kushika mikono ya sanamu ya Marduk wakati wa kusimikwa.

Mfalme wa mwisho wa Babeli hakukubaliwa na makuhani wa Marduk kwa sababu alitaka kubadilisha ibada, lakini mfalme Koreshi II wa Uajemi aliyetwaa mji alishika mikono ya sanamu akapokewa kama mfalme wao.

Katika masimulizi ya Enūma elish kuna maelezo yafuatayo juu ya Marduk:

Mungu Ea alimzaa Marduk akampaa tabia za kimungu na bao za maandiko zinazotunza siri zote za wakati ujao.

Miungu wazee walisumbuliwa wakati ule na makelele ya miungu vijana; hivyo Tiamat mama wa miungu na Abzu baba wa miungu wote waliamua kuamgamiza miungu vijana wote. Lakini Ea aliwazuia akamwua Apsu.

Tiamat alizaa majoka mengi kama wasaidizi dhidi ya watoto wake. Hapa kulikuwa na mkutano wa miungu vijana waliomchagua Marduk kama mkuu wao wakamwahidi atakuwa bwana wao akiwaokoa.

Hivyo Marduk alimshambulia Tiamat akampasua pande mbili. Kutokana na nusu zake alianzisha mbingu na nchi. Miungu wengine walimfanya mfalme wao. Marduk alijenga kiti chake cha enzi mjini Babeli ambayo sasa ikawa kitovu cha ulimwengu.

Baada ya kuanzisha dunia Marduk pamoja na babaye Ea walimwumba mwanadamu kwa udongo na damu ya joka.

Wataalamu wanafikiri ya kwamba masimulizi yale yalitungwa na makuhani wa Babeli kwa lengo la kumtangaza Marduk kama mungu mkuu kwa miungu mingi iliyoabudiwa katika miji ya Mesopotamia iliyokuja chini ya mamlaka ya Babeli na kuchukua nafasi ya mitholojia mbalimbali za miji ile

Majina ya miungu mingi katika masimulizi yalijulikana tayari kutoka dini ya Sumeri iliotangulia kutawala Mesopotamia kabla ya Babeli.