Nenda kwa yaliyomo

Kambisi II

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kambisi alivyomkamata Farao Psamtik; uchoraji kwenye mhuri wa Kiajemi, karne ya 6 KK

Kambisi II (Kiajemi: کمبوجيه دوم ‎kambujie dovom) (*mnamo 558 KK; + Machi 522 KK) alikuwa mfalme wa wafalme wa milki ya Uajemi. Alikuwa mwana wa Koreshi Mkuu aliyeanzisha nasaba ya Akhameni.

Kambisi alipanusha milki aliyorithi kutoka babake Koreshi kwa kuvamia Misri na kuiunganisha na dola yake.

Kambisi alikuwa mwana wa kwanza wa Koreshi alipokea jina lake kutokana babu yake Kambisi I. Baada ya kutwaa Babeli Koreshi alitaka kumfanya mwanawe kuwa mfalme mdogo juu ya Babeli. Lakini hapa tunasikia kutoka Herodoti ya kwamba mpango huu ulishindikana; wakati alipotaka kushuhudia mara ya kwanza sherehe ya mwaka mpya alifika akivaa sare za kijeshi. Tendo hili lilikasirisha makuhani wa Babeli na Koreshi alimwondoa katika nafasi kama mfalme mdogo. Lakini baadaye alimtangaza rasmi kama mfuasi wake na baada ya kifo cha Koreshi Kambisi alikuwa mfalme wa wafalme mwaka 529.

Katika miaka iliyofuata alipanga vita dhidi ya Misri iliyokuwa dola kubwa la mwisho katika sehemu zile za dunia zisizotawaliwa bado na Uajemi. Kabla ya kuanza vita alifanya mapatano na watawala kadhaa Wagiriki waliomsadia jahazi na pia na Waarabu wa Sinai waliompatia maji wakati wa kuvuka jangwa.

Mwaka 526 KK ulifuata uvamizi wa Misri. Kambisi alimshinda Farao Psamtik III mnamo mwaka 525 KK katika mapigano ya Pelusium na mji mkuu Memphis ilitwaliwa mara baadaye.

Kambisi alikuwa Fara mpya wa Misri akakaa hapa miaka mitatu. Akamwoa binti wa mfalme wa Misri. Alijaribu pia kuvamia Nubia upande wa kusini lakini hakufaulu. Katika kipindi hiki kilitokea uasi dhidi mfalme huko Uajemi na Kambisi aliamua kurudi haraka. Njiani alikufa. Taarifa zinatofautiana ama alijiua aliposikia ya kwamba wapinzani wake wameshinda lakini Herodoti anaandika ya kwamba alijijeruhi kwa ajali na kufa kutokana na homa ya kidonda.