Waarya

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Arya ni neno ambalo awali lilikuwa linatumika kama jina la kujitaja kwa wasemaji wa lugha za Kihindi-Kiajemi. Ufafanuzi wa kuwa mmoja wa Waarya ulikuwa wa kidini, kitamaduni na kilugha, sio kimbari[1] au kirangi. [2]

Jina la kale[hariri | hariri chanzo]

Kwenye mwisho wa karne ya 18 ilitambuliwa kwamba kuna uhusiano baina ya lugha za Ulaya na lugha za Uhindi na Iran. Elimu hii ilileta kuziainisha lugha hizo katika familia ya lugha za Kihindi-Kiulaya (Indoeuropean languages). Watafiti walitambua ushahidi katika vitabu vya kale vya Uhindi na Iran kwamba wasemaji wa kwanza walijiita "Waarya" (Arian). Watafiti kadhaa walichukua jina hili kama jina la wasemaji wa kiasili kwa lugha za Kiulaya-Kihindi kwa jumla, hivyo pia kama jina la watu asilia wa Ulaya.

Gobineau na Waarya katika Ulaya[hariri | hariri chanzo]

Katika karne ya 19 neno "Arya" lilianza kutumiwa kwa maana ya kimbari. Mwaka 1850 mwandishi Mfaransa Arthur de Gobineau aliwaza kwamba kundi la Waarya walikuwa kiasili Wazungu weupe wenye macho ya buluu na nywele ya manjano waliohamahama sehemu nyingi duniani na kuanzisha staarabu zote za juu ilhali wakichangyana na watu wa kila mahali; Gobineau aliwagawa binadamu katika mbari tatu za weupe, wanjano na weusi. Waarya watupu walibaki tu katika Ulaya ya kaskazini yaani Wagermanik. Wazungu wa Ulaya Kusini (pamoja na Wahispania na Wafaransa wa kusini), wazungu wa Ulaya ya Mashariki, watu wa Afrika ya kaskazin, wakazi wa Mashariki ya Kati, wa Asia ya Kati na Wahindi walikuwa matokeo ya mchanganyiko na hivyo mbali na asili ya "Kiarya".

Gobineau alizaliwa katika familia ya kikabaila; aliamini kwamba makabaila wa Ufaransa walikuwa wajukuu wa Wafaranki waliokuwa Wagermanik na kuvamia eneo la Gallia (jina la Ufaransa zamani ya Kiroma ya Kale), ilhali wakazi wa kawaida katika Ufaransa walikuwa tokeo la michanganyiko mbalimbali waliofaa kutawaliwa na mabwana wenye asili ya Kigermanik. Hata hivyo, aliona kuongezeka kwa mchanganyiko wa kimbari hadi koo za makabaila wa nchi yake na mchanganyiko huo ulikuwa sababu ya kushuka chini kwa Ufaransa machoni pake.

Waarya katika mafundisho ya kimbari[hariri | hariri chanzo]

Baada ya Gobineau wataalamu wengine wa Ulaya walipenda hoja lake wakaiendeleza na kutunga nadharia ya "mbari ya kaskazini" (Nordic Race) wakianza hata kutafuta asili ya Waarya katika Skandinavia.

Tofauti na Gobineau, aliyejumuisha pia watu wa Mashariki ya Kati katika "mbari nyeupe", walitenganisha Wayahudi kutoka "weupe" na kuwapanga kama mchanganyiko wa kimbari yenye tabia hasi kushinda watu wote.

Ushawishi mkubwa ulitokana na maandiko ya Mwingereza Houston Stewart Chamberlain aliyeunganisha mawazo ya Chamberlain na chuki dhidi ya Wayahudi ya Richard Wagner. Kitabu chake "Misingi ya Karne ya 19" kilimshawishi Adolf Hitler na itikadi ya Wanazi.

Chamberlain aliandika mnamo 1899: "Mbari za ubinadamu zinatofautiana katika tabia zao na pia katika kiwango vya uwezo wao, na mbari za Wagermanik ziko katika kundi lenye uwezo wa juu kabisa, kundi linaloitwa "Waarya". ..Kimwili na kiakili Waarya ni bora kati ya watu wote duniani; kwa sababu hiyo ndio mabwana wa Dunia."[3]

Kinyume chake aliona Wayahudi kama hatari kubwa kwa tamaduni za Ulaya kwa sababu waliendelea kutunza urithi wa kigeni na kujitenga na wote wengine; wenyewe alikuw machoni pake tokeo la mchanganyiko wa mbari mbalimbali zisizoweza kupatana (Wasiria na Waarabu) na hapo aliona msingi wa tabia yao mbaya.

Waarya chini ya Wanazi wa Adolf Hitler[hariri | hariri chanzo]

Katika karne ya 20 wafuasi wa Chamberlain pamoja na Hitler walisambaza itikadi hiyo na kuipanusha. Baada ya Wanazi kutwaa serikali ya Ujerumani mnamo 1933, walitangaza mara moja kwamba watumishi wote wa serikali walipaswa kuonyesha asili yao ya "Kiarya"[4]; hali halisi kila mwajiriwa wa serikali alitkiwa kuonyesha hati za ubatizo wa wazazi wake hadi mababu na mabibi; hati hizo zilonyesha kwa kawaida kama mtu alikuwa Myahudi au Mkristo. Kwa njia hiyo makumi elfu walifukuzwa kazini, hata kama walikuwa tayari Wakristo katika kizazi cha pili. Mkwaka 1935 sheria mpya iliunda ulazima kwamba kila raia alitakiwa kuonyesha asili yake ya "Kiarya".

Sheria hizi zilikuwa msingi wa kuwatenga Wayahudi pamoja na Wakristo wenye ukoo wa Kiyahudi katika jamii, kupora mali yao na kuwakamata wakati wa Vita Kuu ya Pili na kuwapeleka katika makambi ya mauti.

Matumizi ya neno "Arya" leo[hariri | hariri chanzo]

Kwa jumla mafundisho ya Chamberlain na Wanazi kuhusu mbari na hasa kuhusu "Waarya" yameonekana kuwa ya uwongo. Hakuna ushahidi wowote kwamba watu wa Ulaya walitumia jina hili kati yao. Leo hii wanahistoria wanatumia istilahi "Arya" pekee kwa makundi katika kipindi cha historia ya Iran na Uhindi walioitumia kufuatana na vyanzo katika vitabu vyao vya kale.

Shirika ya ndege ya Afghanistan inaitwa "Arya", na jina la nchi ya Iran linatokana na neno "Arya".

Ukatili uliofanywa kwa jina la itikadi hii ya kimbari umesababisha wasomi wa lugha kuepuka neno "Arya", ambalo limebadilishwa mara nyingi na " Indo-Iranian ", na tawi tu la Asia Kusini bado linaitwa " Indo- Aryan . "

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Katika makala hii, "mbari" hutumiwa kwa maana ya Kiingereza "race"
  2. Reza Zia-Ebrahimi, Iranian Identity, the 'Aryan Race,' and Jake Gyllenhaal, PBS (Public Broadcasting Service), 6 August 2010.
  3. The races of mankind are markedly different in the nature and also in the extent of their gifts, and the Germanic races belong to the most highly gifted group, the group usually termed Aryan ... Physically and mentally the Aryans are pre-eminent among all peoples; for that reason they are by right ... the lords of the world.
  4. Sheria ya 1933 "Sheria kuhusu kurudisha utumishi wa Umma" asiye Mwariya alifafanuliwa kuwa "mtu aliyetokana na wazazi au mababu wasio Waarya (hasa wazazi au mababu Wayahudi)" (Campt 2004, p. 143).