Maiti
Maiti ni mwili wa binadamu aliyekufa. Mwili wa mnyama aliyekufa huitwa mzoga.
Maiti ikitazamiwa kisayansi
[hariri | hariri chanzo]Kifo kinaenda sambamba na mwisho wa michakato ya uhai katika seli za mwili. Molekuli zinazojenga mwili zinaaza kuoza na kuachana. Kuoza kunasababishwa mara nyingi na vyembehai au bakteria ndogo zinazoanza kula sehemu za miili iliyokufa na kupotea uwezo wa kujikinga dhidi ya bakteria hizi zinazopatikana muda wote lakini huzuiliwa na kinga la mwili hai. Mchakato wa kuoza unavunja molekuli na kuacha kampaundi mbalimbali zisizotokea katika dunia pekee yao isipokuwa kwa njia ya viumbehai.
Kikemia sehemu za mwili wa awali huwa mata ogania inayoingia tena katika mzunguko wa maisha duniani na kuwa lishe ya viumbehai. Mara nyingi ni mifupa pekee inayoweza kubaki kwa sababu sehemu kubwa ya mifupa si tena seli hai bali mata anogania. Lakini hata mifupa inaweza kupotea kama inakaa katika mazingira kama ardhi penye kemikali inayoingia katika mmemenyuko wa kikemia na kemikali za mfupa. Kinyume inaweza kutokea katika mazingira kavu sana ya kwamba maiti inakauka tu bila kuoza kabisa na kuwa mumia.
Maiti katika hali ya kuoza ni hatari ya afya kwa wanadamu wengine kwa sababu ina bakteria nyingi zinazoweza kusababisha magonjwa. Kwa hiyo maiti si vema kubaki karibu na watu walio hai. Inawezekana ya kwamba hapa ni asili moja ya desturi ya kuzika maiti kwenye ardhi au kuichoma motoni. Hatari hii ni pia sababu ya kuwepo kwa sheria mbalimbali zinazoratibu mahali pa pekee pa mazishi.
Utamaduni na dini
[hariri | hariri chanzo]Tangu kale jamii mbalimbali walitumia mbinu tofauti kushughulika maiti. Mara nyingi maiti ilitazamiwa kuwa najisi kwa sababu ya mauti iliyochafusha uhai. Hapo kuna amri na miiko mingi katika dini mbalimbali kuhusu kugusa maiti pamoja na masharti ya kujitakasa.
Katika imani ya wengine ni muhimu kutunza maiti kwa namna fulani kwa sababu wanategemea kuwa mwili utarudishwa tena katika namna ya uhai. Imani hii ilikuwa msingi wa jitihada za watu wa Misri ya Kale waliokausha maiti kama mumia na kuyazika kiangalifu sana kwa sababu zilihitajika kwa maisha ya baadaye. Ilikuwa pia na nguvu katika dini zinazoamini ufufuo wa mwili kama Uyahudi na Ukristo. Katika Uyahudi kaburi lapaswa kukaa na kutosumbuliwa kamwe ili maiti isiharibike kabla ya ufufuo. Mafundisho ya kufanana yalikuwepo pia katika Ukristo ambako wanatheolojia walijadili kama maiti iliyokatwakatwa vitani au kwenye ajali inaweza kufufushwa siku ya ufufuo.
Katika maeneo mengine njia ya kawaida ilikuwa kuchoma maiti. Kwa Wahindu hii ni njia ya kurudisha mwili katika umoja wa elementi 4 za dunia yaani hewa, moto, ardhi na maji. Kinyume chake Waajemi wa Kale walitaka kulinda utakatifu wa ardhi, moto na maji dhidi ya unajisi wa maiti kwa waliacha maiti juu ya milima (baadaye juu ya minara iliyojengwa kwa kusudi hii) ili waliwe na ndege wa angani, baadaye wakakusanya mifupa na kuyatunza shimoni.
Kuna pia taarifa ya jamii mbalimbali walioacha maiti porini tu kwa ajili ya wanyamapori.
Maiti ikitazamiwa kisheria
[hariri | hariri chanzo]Katika sheria maiti si mwanadamu tena lakini vilevile si kitu kama vitu vingine. Inaendelea kustahili sehemu za heshima ya kibinadamu. Kwa hiyo maiti haiwezi kutupwa hovyo kama takataka bali kuna sheria zinazodai mazishi au namna nyingine za kuondoa maiti katika mazingira ya jamii ya watu.
Leo hii kuna hasa njia za mazishi na kuchoma maiti zinazokubaliwa duniani. Mahali pachache kama Uhindini kuna bado nafasi kwa uzikaji wa hewani.
Sheria za nchi kwa kawaida zinafuata hapo utamaduni na dini za wananchi. Hii inahusu pia maazimo kuhusu mahali, tarehe na namna ya mazishi pamoja na swali ni nani anayewajibika kwa gharama.
Jambo la pekee ni swali la madaraka juu ya maiti kama hakuna ndugu wala agano. Wanasayansi kama matabibu wanatafuta maiti kwa ajili ya mafunzo ya wanafunzi wao.
Katika nchi zilizoendelea kuna swali la kutumia sehemu za maiti kama moyo, maini na kadhalika kwa tiba ya wagonjwa kama kuna maiti za watu wenye afya au vijana waliokufa baada ya ajali zinazoweza kutunzwa na kunchunguliwa kabla ya kuoza.