Nenda kwa yaliyomo

Akiolojia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Wanaakiolojia wakichimba kwenye misingi ya maghofu ya monasteri huko Uswidi.
Barabara hii ya Pompei (Italia) ilifunikwa mwaka 79 na majivu ya volkeno kwa muda wa miaka 1800 hadi kufunuliwa tena na wanaakiolojia kuanzia mwaka 1863.

Akiolojia (kutoka Kiyunani αρχαίος = zamani na λόγος = neno, usemi) ni somo linalohusu mabaki ya tamaduni za watu wa nyakati zilizopita. Wanaakiolojia wanatafuta vitu vilivyobaki, kwa mfano kwa kuchimba ardhi na kutafuta mabaki ya majengo, makaburi, silaha, vifaa, vyombo na mifupa ya watu.

Akiolojia na historia

[hariri | hariri chanzo]

Tofauti na somo la Historia, akiolojia haichunguzi sana maandishi hasa ili kupata ufafanuzi wa mambo ya kale. Historia inatazama zaidi habari zilizoandikwa lakini akiolojia inatazama vitu vilivyobaki kutoka zamani. Wanaakiolojia wanaweza kutumia maandishi na habari za historia wakiamua jinsi gani waendelee na utafiti wao, kwa mfano wachimbe wapi. Lakini hutumia mitindo ya sayansi mbalimbali kuchunguza vitu vinavyopatikana kwa njia ya akiolojia.

Kinyume chake, matokeo ya akiolojia ni chanzo muhimu kwa wachunguzi wa historia. Mara nyingi matokeo ya akiolojia yanaweza kupinga au kuthibitisha habari zilizoandikwa au kufungua macho kwa kuzielewa tofauti.

Mfano wa Pompei

[hariri | hariri chanzo]

Mfano bora wa akiolojia ni utafiti wa mji wa Pompei huko Italia. Habari za Pompei zimepatikana katika maandishi mbalimbali ya Kiroma, lakini mji uliharibika kabisa na kufunikwa na majivu ya volkeno Vesuvio mwaka 79 B.K.

Kuanzia mwaka 1748 wataalamu walianza kuchimba mahali pa mji mpotevu wakaupata. Hadi leo sehemu kubwa ya mji umefunuliwa tena. Chini ya majivu na udongo wa karne nyingi vitu vingi vimehifadhiwa vizuri ambavyo vingepotea kabisa visingefunikwa, kwa mfano picha za Kiroma zenye rangi nzuri kabisa kwenye kuta za nyumba. Hata mabaki ya chakula yamepatikana yakachunguzwa.

Afrika na akiolojia

[hariri | hariri chanzo]

Ujuzi wa akiolojia ni muhimu sana kwa ajili ya historia ya Afrika. Tamaduni nyingi za Afrika ziliendela bila maandishi hadi juzi au hata leo. Habari zetu kuhusu utamaduni wa Zimbabwe Kuu au kuhusu uenezi wa Wabantu hutegemea akiolojia kwa kiasi kikubwa sana.

Hivyo akiolojia huongeza ujuzi wetu kwa kufunua ushahidi wa nyakati za kale; wakati huohuo kazi ya akiolojia inahatarisha ushahidi huo kwa sababu kazi yake huondoa hifadhi ya udongo. Katika karne za kwanza za akiolojia mabaki mengi ya tamaduni za kale yameharibika kutokana na kufunuliwa kwao. Kuepukana na tatizo hilo ni jukumu muhimu la akiolojia ya kisasa.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Akiolojia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.