Kalenda ya Kiislamu
Sehemu ya mfululizo wa makala juu ya |
Imani na ibada zake |
Umoja wa Mungu |
Waislamu muhimu |
Abu Bakr • Ali |
Maandiko na Sheria |
Qur'an • Sunnah • Hadithi |
Historia ya Uislamu |
Historia |
Tamaduni za Kiislamu |
Shule • Madrasa |
Tazama pia |
Kalenda ya Kiislamu ni mtindo wa kuratibu wakati unaopatikana katika nchi mbalimbali za Kiislamu. Tofauti na kalenda ya kawaida inayofuata jua hii ni kalenda ya mwezi inayofuata kuandama kwa mwezi.
Pia Waislamu wanaoishi katika mazingira yasiyo ya Kiislamu hutumia kalenda hii kwa ajili ya kupanga maisha yao ya kidini, hasa sikukuu na saumu.
Kalenda hii ilianza kutumika rasmi kutokana na tukio la mtume Muhammad kuhama Makka kwenda Madina, tukio ambalo linajulikana kama Hijra.
Mahali pengi Kalenda ya Kiislamu hutumika pamoja na kalenda zinazofuata mwendo wa jua, hasa kalenda ya Gregori ambayo ndiyo iliyoenea zaidi duniani.
Miezi na mwaka
Kalenda ya Kiislamu imepokea kawaida ya mwaka wa Waarabu wa kale wenye miezi 12. Hesabu ya vipindi hivi 12 hufuata muonekano wa Mwezi angani, ambayo ni tofauti na "miezi" katika kalenda ya kimataifa ambayo hayana uhusiano na kuonekana kwa Mwezi kwenye anga.
"Mwezi" humaanisha kipindi kamili kati ya kuonekana kwa mwezi wa hilali mara ya kwanza hadi kurudia kwa kuonekana kwake. Kwa sababu muda huo ni siku 29.5, mwezi huhesabiwa kuwa na siku 29 au 30.
Waislamu wanaofuata mfano wa Kisaudi hukubali kwamba mwezi mpya umeanza kama umeonekana kwa macho. Kwa sababu desturi hii imeleta matatizo ya kutokubaliana, pia ni rahisi kukadiria mwendo wa mwezi, nchi mbalimbali za Kiislamu hutumia makadirio ya kitaalamu kupanga tarehe za miezi.
Idadi ya siku katika mwaka wa Kiislamu ni 354, kwa hiyo ni mfupi kuliko mwaka wa Jua wenye siku 3651/4. Kwa sababu hiyo sherehe zote za mwaka wa Kiislamu husogea polepole katika majira ya mwaka wa kalenda ya kiraia inayofuata Jua.
Hesabu ya miaka
Taz. makala "Miaka baada ya hijra"
Hesabu ya miaka katika kalenda ya Kiislamu hufuta utaratibu wa "miaka baada ya hijra" yaani tangu kuhamia kwake Mtume Muhammad kutoka Makka kwenda Madina. Hijra ilitokea mwaka 622 BK au katika mwaka 1 wa hesabu yenyewe.
Njia inayofuata inasaidia kujua takriban tarehe gani ya Kiislamu inalingana na tarehe ipi katika kalenda ya kawaida:
- K = (32H : 33) + 622
- H = (33*(K - 622)): 32
- mfano mwaka K= 2017 - 622 = 1395 * 33 = 46035 : 32 = 1438.6
K (Mwaka "baada ya Kristo" katika kalenda ya Kikristo), H (Mwaka "Baada ya Hijra" katika kalenda ya Kiislamu)
Kalenda ya Kiislamu ya "Shamsi" ya Iran
Huko Uajemi (Iran) na Afghanistan kuna mfumo tofauti wa kupanga wakati. Huko wanatumia kalenda ya jua wakihesabu muda wa mwaka ni siku 365 jinsi ilivyo katika kalenda ya Gregori. Kila mwaka unaanza mnamo tarehe 20 Machi ambayo ni sikusare ya machipuo yaani usawa wa muda wa usiku na mchana kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia.
Ni kalenda ya Kiislamu kwa sababu inaanza kuhesabu miaka tangu hijra. Kalenda hii huitwa "Shamsi" (kutoka neno la Kiarabu / Kifarsi شمس shams = Jua). Kwa mfano, mwaka 1396 shamsi ya Iran inalingana na mwaka 1438 wa kalenda ya kawaida ya Kiislamu.
Huko wanaita kalenda ya kidini "kalenda qamari" (yaani ya mwezi) na mara nyingi kuchapisha namba ya "mwaka qamari" kando ya "mwaka shamsi". Katika kupanga sikukuu za kidini hufuata kalenda qamari lakini sikukuu za serikali hufuata kalenda shamsi.
Mwaka mpya katika kalenda hii inaanza kikamilifu wakati wa sikusare machipuo yaani tarehe 21 au 20 Machi ambayo ni maarufu kama sikuu ya Nowruz[1].
Miezi
Miezi yenye sikukuu muhimu ni hasa
- mwezi wa saumu wa Ramadhani,
- mwezi wa Haj wenye tarehe 10 ndiyo Idd el Hajj na
- mwezi wa Rabi' ul-auwali wenye tarehe 12 Idd-ul-maulidi yaani sikukuu ya kuzaliwa kwake Mtume Muhammad (Maulidi-an-Nabii).
Mwezi wa Muharram ni muhimu sana kati ya Washia wanaokumbuka mateso na kifo cha Imam Husain wakati wa mapigano ya Karbala.
Majina na mfuatano wa miezi ni hivi:
- Muharram محرّم
- Safar صفر
- Rabi`-ul-Awwal (Rabi' I) ربيع الأول
- Rabi`-ul-Akhir (Rabi' II) ربيع الآخر أو ربيع الثاني
- Jumaada-ul-Awwal (Jumaada I) جمادى الأول
- Jumaada-ul-Akhir (Jumaada II) جمادى الآخر أو جمادى الثاني
- Rajab رجب
- Shaaban شعبان
- Ramadan رمضان
- Shawwal شوّال
- Dhul Qaadah ذو القعدة
- Dhul Hijjah ذو الحجة
Siku za Juma au Wiki
Kalenda ya Kiislamu hutumia juma au wiki ya siku saba jinsi ilivyo kawaida kwa Wayahudi na Wakristo. Siku muhimu zaidi ni Ijumaa ambako Waislamu hukusanyika kwa ajili ya sala ya pamoja.
Kwa Kiarabu majina ya siku za juma hufuata hesabu ya Kiyahudi jinsi inavyoonekana katika Biblia. Jumapili inaitwa "siku ya kwanza", Jumatatu "siku ya pili" hadi "siku ya tano" = Alhamisi. Siku ya sita pekee imepewa jina jipya la Kiislamu kutokana na mkutano wa sala ya pamoja.
Siku ya saba tena imebaki na jina lake la Kibiblia "Sabato" au siku ya saba. Hii ni kwa sababu utamaduni wa Kiarabu kabla ya Uislamu uliwahi kupokea athira nyingi kutoka kwa Wayahudi na Wakristo, pia walikuwepo Waarabu ambao upande wa dini walikuwa Wakristo na Wayahudi.
Majina ya siku katika lugha ya Kiswahili yanaonyesha ya kwamba lugha ilianza katika mazingira ya Kiislamu kabisa, bila athira za moja kwa moja kutoka Uyahudi au Ukristo. Majina ya siku yamepangwa kufuatana na Ijumaa ambayo ni siku muhimu hasa katika maisha ya Kiislamu. Maana ya Jumamosi, Jumapili n.k. ni "Siku ya kwanza, pili, tatu" baada ya Ijumaa. Alhamisi imebaki na jina la Kiarabu.
- Jumapili: yaum al-ahad (siku ya kwanza) يوم الأحد
- Jumatatu: yaum al-ithnayna (siku ya pili) يوم الإثنين
- Jumanne: yaum ath-thalatha (siku ya tatu) يوم الثلاثاء
- Jumatano: yaum al-arba`a (siku ya nne) يوم الأَربعاء
- Alhamisi: yaum al-khamis (siku ya tano) يوم خميس
- Ijumaa: yaum al-jum`a (siku ya mkutano) يوم الجمعة
- Jumamosi: yaum as-sabt (siku ya sabato) يوم السبت
Tanbihi
- ↑ Neno hili lilikuwa chanzo cha neno la Kiswahili "Nairuzi" ambalo ni jina mbadala kwa Siku ya Mwaka au Mwaka kogwa katika utamaduni wa Uswahilini.
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |