Nenda kwa yaliyomo

Jumamosi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Jumamosi ni siku ya saba katika juma (wiki) ya siku saba yenye asili ya kiyahudi-kikristo. Iko kati ya siku za Ijumaa na Jumapili. Katika hesabu ya kimataifa ya ISO 8601 ni siku ya sita.

Katika kawaida ya utamaduni wa magharibi Jumamosi imekuwa siku ya kuanza wikendi ikiwa ni siku ambako wafanyakazi wengi hupunzika au hufanya kazi nusu siku tu.

Katika Israeli Jumamosi huheshimiwa kama Sabato ya kibiblia. Wikendi ya Israel inaanza siku ya Ijumaa na kuendelea Jumamosi.

Siku ya saba au siku ya sita?

Katika muundo wa juma wa kibiblia Jumamosi ni siku ya saba. Kanuni ya ISO 8601 ilibadilisha hesabu ya juma kufuatana na kawaida ya mapumziko ya "wikendi" kwenye siku za Jumamosi/Jumapili. Katika muundo huu Jumatatu hutazamiwa kama siku ya kwanza katika juma ya kazi hivyo inahesabiwa kama siku namba "1" ya wiki katika kalenda hivyo Jumamosi kuwa namba 6. Jumuiya za kidini zinasisitiza hesabu ya kibiblia na kawaida katika tamaduni nyingi inaendelea kutumia hesabu ya kale.

Jina la siku kwa Kiswahili na kwa lugha mbalimbali

Katika lugha ya Kiswahili jina la siku lina namba "mosi" (moja) ndani yake. Hii ni dokezo la asili ya Kiswahili katika utamaduni wa Kiislamu pasipo na athira ya Uyahudi. Hesabu inaanza baada ya sikukuu ya Kiislamu ya Ijumaa ambayo ni siku ya sala ya pamoja: Jumamosi kuwa siku ya kwanza baada ya Ijumaa, Jumapili kama siku ya pili, Jumatatu kama siku ya tatu n.k.. Tabia hii katika Kiswahili ni ya pekee hasa kwa sababu Kiarabu ambacho ni lugha ya Korani takatifu na lugha ya kimataifa ya Waislamu kinatumia jina la Kiyahudi na kuiita siku ya سبت (sabat) yaani Sabato.

Lugha nyingi za nchi za Kiislamu zafuata kawaida ya Kiarabu na kuiita vilevile "Sabato" kwa mfano Kiindonesia (Sabtu) au Kiajemi (Farsi) (شنبه - shanbe, kutoka "shabat").

Katika lugha kadhaa za Ulaya jina la siku hutunza kumbukumbu ya mungu aliyeabudiwa zamani za dini ya Kiroma kama vile Kiholanzi "Zaterdag" au Kiingereza "Saturday" (yote: siku ya Saturnus). Lakini lugha zaidi za Ulaya hutumia pia jina la Sabato kwa namna mbalimbali kwa mfano Kifaransa "samedi" (kutoka Kilatini sambati dies - siku ya Sabato), Kihispania "Sábado", Kirusi Суббота (subbota - Sabato).

Siku za juma (wiki)
Jumapili - Jumatatu - Jumanne - Jumatano - Alhamisi - Ijumaa - Jumamosi