Nenda kwa yaliyomo

Mwezi mpevu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mwezi mpevu jinsi inavyoonekana kwa darubini ya 9.25 ".
Mwezi mpevu jinsi ulivyoonekana wakati wa kupatwa tarehe 26 Juni 2010

Mwezi mpevu (ing. full moon) ni hali jinsi tunavyouona Mwezi wakati unaonyesha umbo la duara kamili.

Masharti ya kuona Mwezi mpevu[hariri | hariri chanzo]

Hali hii inatokea wakati:

  1. Dunia iko katikati ya Jua na Mwezi, katika hali ya Jua - Dunia - Mwezi.
  2. Mwezi uko kwenye nyuzi 5 au chini ya mstari wa Dunia - Jua.[1][2]

Katika hali hii nusutufe ya Mwezi inayotazama Dunia inaangazwa kabisa na mwanga wa Jua ikionekana kama duara kamili.

Kama Mwezi ukifika katikati ya mstari Jua - Dunia (yaani ekliptiki) unaingia katika kivuli cha Dunia na kusababisha kuonekana kwa kupatwa kwa Mwezi. Kwa hiyo kupatwa kwa Mwezi hutokea tu wakati wa Mwezi mpevu lakini hakutokei kila Mwezi.

Mwezi mpevu na pande za Mwezi[hariri | hariri chanzo]

Mwezi una umbo la tufe na wakati wote tunaangalia upande wake uleule. Mwezi huzunguka Dunia yetu wakati uleule hujizungusha wenyewe kwenye muhimili wake.Muda unaotumika kwenye mizunguko hii miwili unalingana.Hivyo muda wote tunaona upande uleule wa Mwezi. Kwahiyo inawezekana kuongea juu ya "upande wa mbele" na "upande wa nyuma" wa Mwezi. Upande wa nyuma hatuwezi kuuona kamwe kutoka Dunia.

Kinyume cha Mwezi mpevu[hariri | hariri chanzo]

Kinyume cha Mwezi mpevu ni Mwezi mwandamo ambapo nusutufe ya Mwezi tunayoona haipokei nuru na hivyo Mwezi hauonekani Duniani. Hapo Mwezi unakuwa katika mstari mmoja baina ya Jua na Dunia, yaani hali ya Jua - Mwezi - Dunia. Katika hali hii nusutufe ya Mwezi isiyoonekana kutoka Duniani inaangazwa. Mwezi ukiwa katikati kabisa kwenye mstari Jua - Dunia wakati wa mchana unafunika Jua na [kupatwa kwa Jua]] kunatokea.

Mwezi mpevu katika kalenda[hariri | hariri chanzo]

Kipindi cha kuanzia Mwezi mpevu hadi Mwezi mpevu ufuatao ni siku 29.53 ambacho ni kipindi cha mwezi wa kalenda katika mfumo wa kalenda ya Mwezi (kwa mfano kalenda ya Kiislamu). Katika kalenda ya aina hii Mwezi mpevu hutokea mnamo tarehe 14 au 15 ya Mwezi. Sababu yake ni kuwa kalenda ya Mwezi kama ya Kiislamu huanza kipindi cha Mwezi kipya kwenye siku baada ya Mwezi mwandamo ambapo hilali hilali mchanga inaanza kuonekana.

Uangavu wa Mwezi mpevu kubadilika[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa kuwa mpevu Mwezi hutoa nuru kubwa. Kwa kulinganisha na magimba mengine angani Jua linang'aa mara 400,000 kuliko Mwezi, na Mwezi unaang'aa mara 250 kuliko nuru ya nyota zote angani.

Ung'avu wa Mwezi mpevu unategemea umbali na Dunia. Obiti yaani njia ya Mwezi unapozunguka Dunia si umbo la duara lakini la duaradufu ambako umbali wake kutoka Dunia unabadilika.Palipo karibu zaidi pana umbali wa kilomita 362,600, mahali pa mbali pana kilomita 405,400. Hivyo Mwezi mpevu unaotokea wakati Mwezi uko karibu zaidi na Dunia unaonekana uking'aa zaidi kuliko Mwezi mpevu unaotokea wakati Mwezi ni mbali zaidi. Kila baada ya miaka kadhaa Mwezi unafikia mahali pa njia yake ambapo ni karibu sana na Dunia na hapa Mwezi unaonekana mkubwa pia uking'aa kuliko kawaida. Hali hii ilianza kuitwa kwa Kiingereza "supermoon" au Mwezi mpevu sana.[3]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. "Celestial Alignment without Lunar Eclipse; from google (full moon earth block sunlight) result 2". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2016-10-07. Iliwekwa mnamo 2016-11-14. {{cite web}}: Cite has empty unknown parameter: |3= (help)
  2. "tiled from the ecliptic by about 5 degrees; from google (full moon earth block sunlight) result 3". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-06-28. Iliwekwa mnamo 2016-11-14. {{cite web}}: Cite has empty unknown parameter: |3= (help)
  3. Mwezi mpevu ajabu Jumatatu Novemba 14 Archived 21 Oktoba 2020 at the Wayback Machine., tovuti ya "Astronomy in Tanzania" (Dr. Noorali T. Jiwaji), iliangaliwa 13 Novemba 2016