Maporomoko ya maji
Kwa matumizi mengine ya jina angalia maporomoko



Maporomoko ya maji ni mahali ambako maji yanateremka juu ya kona kwenye mteremko na kuelekea chini. Kwa kawaida ni sehemu ya njia ya mto au kijito pale ambako maji yanateremka juu ya ukingo wa mwamba. Lakini inaweza kutokea pia kwenye ukingo wa barafuto pale ambako maji ya myeyuko yanateremka.
Kutokea na kubadilika kwa maporomoko ya maji
[hariri | hariri chanzo]Maporomoko ya maji hutokea kwa kawaida katika sehemu za juu ya njia ya mto.[1] Hapa mteremko kwa jumla ni mkubwa zaidi na mwendo wa maji haraka zaidi. Kwa hiyo nguvu ya maji ni kubwa zaidi kiasi kwamba yanaweza kuchimba lalio hadi kuwa mfereji kama korongo mrefu.
Pale ambako mwendo wa maji ni juu ya mwamba mgumu mmomonyoko hutokea polepole tu. Pale yanapofikia mahali ambako mwamba mgumu wa juu unakwisha nguvu ya maji yakiteremka kwenye ukingo inachimba lalio ya chini. Chini ya ukingo hutokea dimbwi yenye kizingia cha maji. Maji yanayozunguka humo pamoja na mawe na mchanga ndani yake yanasuguana kwenye ukuta wa mwamba. Kwa njia upenyo au nusu pango hutokea. Kama kuna mwamba laini chini ya tabaka la mwamba mgumu wa juu upanuzi wa pango huendelea haraka zaidi. Baada ya muda upenyo unakatika na kuanguka.[2]
Kwa njia hii ukingo wa maporomoko unarudi nyuma na kurudisha njia ya korongo nyuma. Kasi ya harakati inategemea na tabia za mwamba unaopatikana. Kuna maporomoko yanayorudi nyuma mita na nusu kila mwaka.[3]
Baada ya muda wa kutosha (wakati mwingine miaka milioni) nguvu ya maji inakuwa imeondoa mwamba wa kutosha hali hakuna maporomoko tena na ngazi katika njia inakuwa mteremko tu.
Picha
[hariri | hariri chanzo]- Maporomoko ya Boti, Ghana
- Maporomoko yanatelemka kwenye Atlantiki (Madeira, Hispania)
- Black Waterfalls, West Virginia
- Purakaunui Falls, Newzealand
- Maporomoko ya Kreealmwasserfall, Austria
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Carreck, Rosalind, ed. (1982). The Family Encyclopedia of Natural History. The Hamlyn Publishing Group. pp. 246–248. ISBN 0711202257.
- ↑ "How waterfalls work". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2010-09-21. Iliwekwa mnamo 2015-05-18.
- ↑ "Observe river erosion creating waterfalls and chasms". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-05-17. Iliwekwa mnamo 2015-05-18.