Nenda kwa yaliyomo

Isilandi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Iceland)
Lýðveldið Ísland
Jamhuri ya Isilandi
Bendera ya Isilandi Nembo ya Isilandi
Bendera Nembo
Kaulimbiu ya taifa: (hakuna)
Wimbo wa taifa: Lofsöngur
Lokeshen ya Isilandi
Mji mkuu Reykjavík
64°08′ N 21°56′ W
Mji mkubwa nchini Reykjavík
Lugha rasmi Kiisilandi
Serikali Jamhuri
Guðni Th. Jóhannesson
Katrín Jakobsdóttir
Uhuru
kujitawala
Jamhuri

1. 12. 1918
17. 06. 1944
Eneo
 - Jumla
 - Maji (%)
 
102,775 km² (ya 108)
2.7
Idadi ya watu
 - Januari 2016 kadirio
 - Desemba 1970 sensa
 - Msongamano wa watu
 
332,529 (ya 182)
204,930
3.2/km² (ya 235)
Fedha Króna ya Iceland (ISK)
Saa za eneo
 - Kiangazi (DST)
GMT (UTC+0)
None (UTC)
Intaneti TLD .is
Kodi ya simu +354

-


Ramani ya Isilandi

Isilandi (pia: Aisilandi; maana kwa Kiisilandi: "Nchi ya barafu") ni nchi ya Ulaya kwenye kisiwa cha Bahari ya Atlantiki ya kaskazini. Iko km 300 kutoka Grinilandi upande wa magharibi na km 1,000 kutoka Norwei upande wa mashariki.

Eneo lake ni km² 103,000 lakini idadi ya watu ni laki tatu pekee.

Ingawa Isilandi si sehemu ya rasi ya Skandinavia, inahesabiwa kati ya nchi za Skandinavia.

Jiografia

[hariri | hariri chanzo]
Vatnajökull ni barafuto kubwa kabisa ya Ulaya

Isilandi ina asili ya kivolkeno. Ni kisiwa kikubwa cha safu ya mgongo kati wa Atlantiki mahali ambako mabamba ya Amerika ya Kaskazini na Ulaya-Asia yanakutana. Kwa sababu hiyo kuna milima mingi, hasa volkeno ni nyingi. Kati ya volkeno mashuhuri za Isilandi kuna Hekla, Eldgjá, Herðubreið na Eldfell.

Kwa ujumla hali ya hewa ni baridi na barafuto zinafunika sehemu kubwa ya nchi. Hasa nyanda za juu ni baridi mno, hivyo hakuna mimea. Karibu makazi yote ya watu ni karibu na pwani.

Kusini mwa kisiwa haikuwa baridi mno kwa sababu ya mkondo wa ghuba linaloendelea kusukuma maji ya ghuba ya Meksiko hadi Atlantiki ya kaskazini. Mkondo huo unapofikia Isilandi si ya moto tena lakini vuguvugu kidogo hivyo inazuia baridi kali sana.

Volkeno zimesababisha kuwepo kwa maji ya moto mahali pengi. Waisilandi wanapenda kuogelea nje katika mabwawa hata wakati wa theluji katika maji ya moto kutokana na joto la kivolkeno. Joto hilo linatumika kidogo hata kwa kilimo; linapasha moto nyumba za kioo na kuwezesha mimea kuzaa matunda mwaka wote, hata wakati wa baridi kali. Kwa njia hiyo Isilandi inavuna ndizi na machungwa yake!

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Historia ya awali

[hariri | hariri chanzo]

Isilandi iko mbali na bara la Ulaya na la Amerika tena katika mazingira ya baridi. Hivyo inaaminika haikuwa na watu kabisa hadi mwaka 800 BK. Wataalamu hawakubaliani kama ni mabaharia kutoka Norwei au Eire waliobahatika kufika kisiwani na kujenga makao ya kwanza.

Hakika waliofika wengi kidogo walikuwa Waviking au Wanorwei wa kale katika karne ya 9. Kama Waeire walikuwepo walifukuzwa au kuwa sehemu za Waviking. Mtu wa kwanza aliyekumbukwa kwa jina alikuwa Flóki Vilgerðarson.

Waviking waliofika walikuja pamoja na familia na watumishi au watumwa wao. Mnamo mwaka 930 machifu na wasimamizi wa familia zilizokuwepo walipatana kuhusu aina ya katiba kwa Isilandi. Walianzisha bunge la Althing. Ulikuwa mkutano wa watu 36 walioitwa "Godi" wakiwa na cheo cha kuunganisha madaraka ya chifu, hakimu na kuhani. Utaratibu huu wa kuwa na bunge umeendelea hadi leo bila kusimama. Hivyo Isilandi ni nchi ya pekee ambako utaratibu wa kidemokrasia wa kale umeendelea wakati katika nchi za Ulaya nafasi ya wafalme au watawala wengine iliongezeka na kumeza haki zote za watu wa kawaida.

Mwaka 985 Mwisilandi aligundua njia ya kufika Grinilandi na baadaye Amerika ya Kaskazini. Mviking "Erik Mwekundu" alifukuzwa kisiwani kwa sababu alikuwa mwuaji. Alielekea magharibi kwa jahazi yake na kufika kwanza Grinilandi halafu pwani ya Kanada ya leo. Aliita bara jipya "nchi ya mzabibu" kwa sababu alikuta aina ya mizabibu isipokuwa bila matunda.

Chini ya Norwei na Udeni

[hariri | hariri chanzo]

Tangu 1262 uhuru wa Isilandi ulikwisha kwa sababu viongozi walijiunga na Ufalme wa Norwei. Isilandi iliendelea kuwa na bunge lake na madaraka mbalimbali - hasa kwa sababu usafiri uliendelea kuwa mgumu - lakini mabwana wakuu walikuwa sasa wafalme wa Skandinavia, kwanza Wanorwei, baadaye Wadeni.

Mwaka 1918 Udeni ilirudisha madaraka yote ya serikali kwa Waisilandi wenyewe isipokuwa mfalme wa Udeni aliendelea kama Mkuu wa nchi.

Kuanzia uhuru

[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa Vita Kuu ya Dunia ya Pili Udeni ilivamiwa na Ujerumani na Althing iliamua ya kwamba kuanzia sasa kisiwa kitajitawala kabisa. Mwaka 1944 Isilandi ilipata uhuru kamili.

Baada ya vita kwisha Isilandi ilipata kuwa nchi mwanachama ya NATO lakini haina wanajeshi hadi leo. Ilifanya mkataba na Marekani ya kuwa Wamarekani wanapewa haki ya kutumia kituo cha ndege kisiwani na kwa upande mwingine wanaahidi kutetea Isilandi.

Mji wa Reykyavik

Reykjavík ni mji mkuu wa Isilandi pia bandari kubwa na kitovu cha uchumi na utamaduni wa nchi.

Miji mingine ni pamoja na Akureyri, Kópavogur, Hafnarfjördhur, Keflavík na Vestmannaeyjar.

Watu wa Isilandi karibu wote (92.61%) ni Waskandinavia. Kati ya wengine, Wapolandi ndio wengi (3.36%).

Lugha ya Kiisilandi bado inafanana sana na ile ya Kinorwei cha kale kilicholetwa kisiwani na wakazi wa kwanza miaka 1000 iliyopita. Watu bado wanaelewa mashairi yaliyotunzwa tangu zamani ile.

Kanisa la kitaifa la Kilutheri ni dini rasmi ya nchi. Hivyo Waisilandi wengi (73.8%) wanahesabiwa kuwa Wakristo Walutheri, ingawa wengi hawafuati dini. Wakristo wa madhehebu mengine, kama vile Wakatoliki, wanafikia 11.7%. Kuna wafuasi wachache sana wa imani nyingine mbalimbali. Kwa jumla Isilandi ni kati ya nchi ambazo zina wakazi wengi wasiomuamini Mungu.

Utamaduni

[hariri | hariri chanzo]

Hadi leo Waisilandi hawana majina ya pili au ya familia. Kila mtoto anapewa jina lake la kwanza halafu jina la baba - wakati mwingine pia jina la mama. Kama mtoto ni wa kiume "-son" (=mwana) itaongezwa, kama ni binti "-dottir" (binti).

Kwa mfano mwimbaji mashuhuri wa kike Björk Guðmundsdóttir alipewa jina la "Björk". Baba yake alikuwa Guðmund hivyo anatumia jina hili pamoja na "-dottir": Guðmundsdottir: "Björk binti Guðmund". Kama mwenyewe atamzaa binti anaweza kuitwa "Björkdottir" lakini mara nyingi jina la baba hutumiwa. Wanawake wanaendelea na jina hili, hawaliachi wakati wa kuolewa.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  • Jonsson, Asgeir (2008). Why Iceland? How One of the World's Smallest Countries Became the Meltdown's Biggest Casualty. McGraw–Hill Professional. ISBN 978-0-07-163284-3.
  • Jonsson, Ivar (2012) 'Explaining the Crisis of Iceland – A Realist Approach' in Journal of Critical Realism, 11,1.
  • Heiðarsson, Jakob Oskar (2015) 'Iceland - My Small Island'.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Isilandi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.